Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii. Kwanza niungane na Wabunge wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia siku hii njema sana kwetu na wakati huu muafaka kwa ajili ya kulihutubia Taifa letu, na pia kujadili masuala ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani nyingine ni kwa Rais na kwa Serikali nzima ya Awamu ya Sita. Kwa namna ya pekee Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana, kila mmoja ni shahidi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za miradi kuhudumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri na timu yake kwa sababu ukizungumza TAMISEMI pia ni dude. Nchi nzima ndiyo TAMISEMI. Kila uendako hutaiacha TAMISEMI usiikute. Napongeza Kamati zetu zote mbili kwa ziara kubwa ziliofanywa mikoani, maana yake ni kwamba, tumefanya kupima utekelezaji wa Serikali kwa muda ule wote wa mwaka mzima wa kibajeti ambao unaisha mwaka huu tarehe 30 Juni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kwanza athari kubwa ya ukosefu wa fedha katika sekta hii ya TARURA nchi nzima. Wakati tunaanzisha TARURA tulikuwa na barabara chache sana, tukaanzisha TARURA, tukapanga mpango wa kuwapa bajeti, barabara nyingi zikafunguliwa na TARURA. Sasa hivi wamezidiwa, hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza 20%, baada ya miezi sita ya mwaka wa bajeti, tunaiomba sana Serikali, hiyo ni namna ya kuongeza fedha za TARURA, na zitolewe kwa wakati kwa jinsi ambavyo zimeombwa ili kusaidia barabara hizi ambazo ni unganishi kutoka kwenye Tarafa mbalimbali katika Majimbo yetu lakini kwenye Kata mbalimbali kuja kwenye Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Miji kwa ajili ya kuwaunganisha wananchi na huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango au hali halisi ipo pale Mbulu. Eneo la Mbulu Mjini tuna mradi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa anisikilize. Tuna mita 600 zimedumu karibu mwaka na zaidi sasa. Mradi huu wa mita 600 una barabara ya kiwango cha lami, lakini pia una daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umekuwa kero sana kwa wananchi wa Mbulu, yaani hasa wakati wa masika Mji unagawanyika pande mbili; upande wa pili na upande mwingine hakuna mawasiliano ya kuvuka kwa ajili ya kiungo hiki cha daraja na hakina lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wangekuwa wamelipa hawa wakandarasi kwa muda wa miezi yote waliyokaa, wangeshamaliza huu mradi wa mita 600, kwani ni mradi mdogo sana. Sasa huu ni mfano tu wa katikati ya mji, vijijini kule hutakwenda, barabara zote zilizofunguliwa na TARURA zimekuwa na hali mbaya sana kutokana na matokeo ya mvua, na pia mvua za El Nino na baadaye masika yalipokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali ni kwamba, timu ipite nchi nzima itazame upya, ilipe madeni ya wakandarasi ili warudi site, waweze kurudisha barabara zetu katika hali njema kwa sababu kila Jimbo tulikopita hata kwenye Kamati moja kwa moja barabara za TARURA zimekuwa na hali mbaya. Hali hii inasababishwa na upatikanaji wa fedha za bajeti ya kawaida na bajeti ya miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi uliopo Mbulu Mjini ni mradi wa fedha za Jimbo. Mradi wa fedha za Jimbo Mheshimiwa Waziri na timu yako ni mradi ambao Mheshimiwa Rais ameuanzisha mpango wa kila jimbo kuona sehemu gani muhimu sana utengewe fedha. Kwa sababu hiyo basi, mradi huu unapokaa wa mita 600 ndani ya miezi sita ama nane athari ni kubwa sana ya ucheleweshaji wa malipo kwa sababu baadaye tunaletewa bili ya ucheleweshwaji wa malipo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ambao unagharimu shilingi milioni pengine 600, kwa vyovyote vile katika ucheleweshaji na gharama za ucheleweshwaji unaweza ukaenda zaidi karibu ya shilingi milioni 800 ama shilingi bilioni moja kulingana na ucheleweshwaji. Angalieni athari ambazo tunapata kulingana na kucheleweshwa kwa certificates zisizolipwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hali ambayo siyo ya kawaida, kila mmoja au kila Mbunge katika Jimbo lake anajua kwamba athari za mabadiliko ya tabianchi imeleta hali mbaya sana ya maporomoko, makorongo na pia barabara nyingi kuharibika, na mwisho wa siku wananchi wanakosa huduma za kijamii za afya, elimu na huduma nyingine kwa ajili ya kutoka eneo moja kwenda lingine. Kwa hiyo basi, tunaiomba sana Serikali itazame upya eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni upungufu wa watumishi katika mamlaka ya TARURA ama wakala wa TARURA nchi nzima. Kila tulipoenda, upungufu umekuwa mkubwa. Kila tunapokaa kwenye mabaraza yetu na pia katika maeneo yetu, upungufu wa watumishi hawa ni mkubwa sana. Ombi langu ni kuwa, angalau tuanze kupunguza idadi hiyo ya upungufu wa watumishi katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuzungumzie suala zima la upungufu wa watumishi hawa kwa sababu kadri ambavyo kazi zinachelewa, ufuatiliaji unakosekana na watumishi ni wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine naomba nimkaribishe sana Mbulu Mheshimiwa Waziri Mchengerwa aone jinsi ambavyo athari tunaipata. Ametuahidi sana kwa muda mrefu pamoja na maeneo mengine, aone jinsi ambavyo tuna hali mbaya ya miundombinu ya barabara ya TARURA. Kwa sababu hiyo, tatizo hilo halipo kwake, ni nchi nzima na sisi tunaiomba Serikali fedha kwa ajili ya kufanikisha mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ni ukamilishaji wa miradi viporo. Kamati yetu ilipotembelea nchi nzima, tumeona kumekuwa na miradi ambayo wananchi walianzisha kwa muda mrefu na sasa ni zaidi ya miaka nane hadi 10 kuna zahanati, kituo cha afya, nyumba ya mwalimu, jengo la ofisi ya kijiji na mambo kadhaa. Nguvu hizi za wananchi zinakosa kutoa huduma kwa sababu ya muda, lakini pia na fedha za umaliziaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni nini? Tunapopanga bajeti ya mwaka huu tutakaouanza, keshokutwa Serikali ione umuhimu mkubwa sana wa kutenga fedha kukamilisha miradi iliyoanzishwa na wananchi ili iweze kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na ili tuweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Tunaishukuru sana Serikali, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ilipata fedha awamu ya kwanza katika vyuo vya kwanza nchini tukafanya ukarabati na ujenzi wa majengo mapya. Mpaka leo ni miaka sita hatujapata fedha za kukamilisha yale majengo yaliyochakaa ambayo hayafai kwa matumizi pamoja na miundombinu mbalimbali inayohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa shule ya ufundi tunayoenda kuijenga kule Mbulu, lakini chuo kile tusipotenga fedha hali itakuwa mbaya sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu, kwa sababu ya hali hii tunayoiona, Mheshimiwa Waziri wa Elimu, naiomba Serikali, jambo hili la usaili wa vijana waalimu limeiathiri sana familia zetu kwa sababu wazazi wanatoa fedha vijana wanaenda kwenye usaili, lakini nafasi ni 100, wanaoitwa ni 1,000 na mwisho wake watoto wanarudi nyumbani hawajafanikiwa. Kama mwalimu aliandaliwa kuwa mwalimu, jambo hili halina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa mamlaka yako na kwa ushauri wa Bunge hili, tuondoe suala hili la usaili kwa waalimu. Wote tulioko hapa, tupo hapa tumefundishwa na Walimu wa UPE, wengine leo ni Madaktari, Maprofesa, wenye degree, lakini mjue kwamba waalimu ndio waliotufikisha hapa. Aliandaliwa kuwa Mwalimu, kama kuna sababu ya usaili, basi tukafanye usaili kwenye vyuo vyetu kama kweli hao waalimu hawajaandaliwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wanafunzi kuitwa 1,000 kwa nafasi 100, vijana wamepigika mikopo waliyokopa wakati wanasoma vyuo, haijalipwa. Saa hizi wanakopa tena nauli ya kwenda kwenye usaili siku tatu, nne mpaka wiki. Nadhani jambo hili kwa namna ya pekee wazazi wameumia. Tunaiomba Serikali itazame upya, iondoe suala hili la usaili kwa waalimu ili walimu wetu waende kwenye ajira kwa namna ambavyo itawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa 100%, naomba tuendelee. (Makofi)