Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyopo Mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, pia nawashukuru wananchi wa Urambo kwa jinsi ambavyo wananipa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuipongeza sana Wizara ambayo inasimamia shughuli zote za TAMISEMI kuanzia Waziri mwenyewe, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote, na Wakuu wa Idara wote, wanafanya kazi kubwa. Hii Wizara ina kazi nyingi sana, tunawaombea kila la heri ili kazi ziendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nichukuwe nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia, Rais wetu kwa kazi kubwa aliyofanya. Kwetu Urambo kama alivyofanya kwingine, tumepata shule nyingi za msingi, za sekondari, na tumepata hospitali. Kwa kweli tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijikita zaidi sasa hivi kwa upande wa elimu, kwa kweli kutokana na wingi wa shule tulizopata mpya, tunahitaji waalimu wengi zaidi kama walivyosema Mwenyekiti wetu ambaye nampongeza, amesoma kwenye taarifa yake kwamba tunategemea kupata waalimu zaidi ya 500. Sasa hivi tunao waalimu 273,736, lakini kutokana na taarifa niliyoisikia leo, tunategemea kupata zaidi ya 500,000 kutokana na wingi wa shule zilizojengwa nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na wingi wa waalimu, Serikali ilidhamiria tangu mwanzo kwamba kutokana na idadi kubwa ya waalimu lazima wawe na chombo kinachohudumia waalimu na ndiyo maana wakaja na Tanzania Teachers Service Commission (TSC) ambayo ilianzishwa mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sheria yao ambayo ninayo hapa, Kifungu cha Tano kuanzia (a) mpaka (l) ni majukumu ambayo wamepewa TSC pamoja na kuajiri, kusambaza, kuwapa mafunzo. Walijua kwamba idadi hii kubwa, inahitaji chombo maalumu cha kuwahudumia, ndiyo wakaunda TSC na ikawapa majukumu makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, je, Serikali ilikaa na kutathmini kwamba hiki chombo kikubwa walichokiunda kinafanya kazi iliyokusudiwa? Nina wasiwasi sana, kama tathmini haijafanyika, tuiombe Serikali ifanye tathmini ya chombo hiki, kwani ni kikubwa lakini utashangaa, sehemu nyingine kuna Ofisa wa TSC. Sitaki kutaja hapa, lakini ukinibana naweza kukutajia. TSC maeneo mengine yanakuwa na wafanyakazi wawili, au mmoja. Kweli inatimiza wajibu iliyopewa kutokana na sheria hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoa wito kwa Serikali, wafanye tathmini ya chombo hiki ambacho ni muhimu sana kutokana na idadi kubwa ya waalimu waliopo na idadi kubwa tunayotegemea kupatikana kutokana na Mheshimiwa Dkt. Samia alivyofanya ya kuongeza shule nyingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nataka waangalie kama majukumu yanatimizwa, pia waangalie hasa wanavyopeleka watendaji kazi kwenye Wilaya wanafanya kama ilivyokusudiwa? Kwa sababu ilitegemea kuwe na mtu wa TSC ambaye anafahamu vizuri sana masuala ya watumishi, halafu anayefahamu sana masuala ya waalimu na sheria pia. Je, wapo kama ilivyokusudiwa? Kama haikukusudiwa, basi waangalie waone jinsi gani tunavyoweza kuboresha (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia na idadi ya fedha, kiasi cha kinachopelekwa hakiendani na makusudio ya kuiunda hii TSC. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kabisa, ili kweli wafanyakazi wafanye kazi vizuri; waalimu waliopo vijijini, waliopo mjini wafanye kazi vizuri, lazima wahudumiwe kikamilifu. Waalimu wengi wanalalamika kutokana na kutokupata haki zao kwa wakati lakini chombo hiki kipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti nataka niulize swali moja. Ukiangalia kwa upande wa afya, wale Makatibu Afya waliopo kwenye hospitali wanaangalia vyote, wanaangalia utumishi wa Madaktari, wanangalia upatikanaji wa dawa, wanaangalia kila kitu, lakini kwa nini yule Katibu wa TSC pale amebanwa? Kwa hiyo, nilikuwa natoa wito kwa Serikali kuiangalia TSC upya ili ifanye kazi iliyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee kwa mambo mengine. Pia namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia kwa jinsi ambavyo ametupa barabara kwa kupitia TARURA, TANROADS, na kadhalika, kwa leo nijikite zaidi kwa TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri sana kutokana na viongozi wote, Mkuu wa Idara, watumishi wote na kadhalika, lakini fedha ndiyo shida. Tunaiomba Serikali yetu iwape fedha TARURA watengeneze barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru TBC, juzi ilitoa taarifa ya Urambo tena nikashtuka kweli, wakaonesha barabara zilizopo vijijini zilivyoharibika. Ahsanteni sana TBC. Sasa naiomba Serikali kwa kupitia Wizara hii ya TAMISEMI itusaidie fedha ziende zikatengeneze barabara za vijijini ambazo mvua imeharibu kiasi ambacho sasa hata kupeleka tumbaku sokoni au kupeleka mahindi na bidhaa nyingine itakuwa shida kwa sababu barabara hazipitiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliomba kwa niaba ya wananchi wa Urambo mpaka sasa hivi, nadhani pengine tumebaki sijui Wilaya ngapi, sisi ambao Mkuu wa Wilaya yupo ndani ya Halmashauri ya Wilaya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kuna Waziri alikuwa anajibu swali. naomba lile jibu alivyojibu akawapa matumaini wananchi wa Urambo kwamba tujengewe nasi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya peke yake tena ya ghorofa, za kisasa na Ofisi ya Halmashauri ambayo ilijengwa mwaka 1974 ijengwe upya ili nasi twende na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nisingependa kumaliza kabla kulizungumzia ni suala la watumishi kudai haki zao. Imekuwa tatizo sasa hivi waalimu wakistaafu wanastaafu kabla hawajarekebishiwa madaraja yao na kwa msingi huo, hata kufanya mahesabu ya pension inakuwa ni vigumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba wafanyakazi warekebishiwe mishahara yao kabla hawajastaafu ili waweze kupata pension wanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)