Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru kwa nafasi hii uliyonipa. Kabla ya yote, naomba niwashukuru Wenyeviti wote wa Kamati zote mbili kwa uwasilishaji mzuri walioutoa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuteuliwa au kuchaguliwa kwa kura nyingi na Chama Cha Mapinduzi ili kuweza kupeperusha bendera kwa Uchaguzi Mkuu huu wa Mwaka 2025; na kwa kumteua Dkt. Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza. Tunayo imani kubwa atakwenda kutupatia ushindi Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kuteuliwa kuweza kupeperusha bendera kwa ajili Urais wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufinyu wa muda, naomba niende kwenye eneo moja ambalo kwa kweli naona kama bado kuna shida. Naomba kuipongeza Serikali chini ya Mheshimiwa Rais wetu kwa kuweza kujenga shule nzuri za sekondari na kwa kuweza kujenga vyumba vya madarasa katika shule za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yale maeneo ya shule za msingi yaliyojengwa vyumba vizuri vya madarasa, yako madarasa mengine ambayo ni yale ya zamani. Sasa unaweza ukaona kwamba ni kama kumekuwa na ubaguzi kidogo. Wanafunzi wangependa kutumia vile vyumba ambavyo ni vipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niishauri Serikali, irudi kwenda kuangalia na kukamilisha madarasa ambayo yapo ni mazuri, mengine ni katika shule zile ambazo ni za zamani kabisa ambazo sisi tulisoma kule, ambazo bado hazijaangaliwa. Naomba sana niliseme hilo kwa sababu linaleta shida kidogo kwa wanafunzi. Pia kwenye miundombinu ya madarasa, sakafu na hata usafi wenyewe wa hayo madarasa, bado ni shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wanapotoka huko kwenye shule za msingi, wanapokwenda sekondari ambapo kule wanakuta madarasa ni mazuri, sehemu ya kujifunzia ni nzuri na sehemu ya kukaa ni nzuri, basi wawe wameanzia huko chini. Ninayo imani Serikali yetu sikivu italiona hilo kwamba nalo ni muhimu liende kufanyiwa kazi, likiwa ni sambamba na vyoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye nyumba za walimu. Kule kwenye vijiji shule zilikojengwa kidogo afadhali, kwamba, vijiji vile vina nyumba kwa maana ya wananchi kuweza kuwakodishia walimu kwa maana ya kupanga. Sehemu ambayo shule shikizi zimejengwa ni maeneo ambayo kidogo yako pembezoni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule ambako wananchi wa maeneo yale, nyumba zao kwa kweli haziko katika hali nzuri, kiasi kwamba walimu hawawezi kupanga kwenye zile nyumba. Kwa kweli mazingira ni magumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iwekeze kwenye eneo hili, ipeleke fedha kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu ili walimu hawa waweze kufanya kazi katika mazingira yaliyoboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda kwenye shule moja, na shule ile ni shikizi ambayo sasa imeshasajiliwa. Shule ile imejengewa madarasa saba, lakini bahati mbaya hakuna nyumba za walimu, na pale ni sehemu ambayo wananchi wake ni watu wa hali duni kidogo ambao nyumba zao kwa kweli ni za hali ya chini sana. Walimu wamejiazimia vyumba hivyo hivyo ambavyo ni madarasa, wamekata partition ili waweze kujikimu katika kuishi. Sasa hiyo siyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Mheshimiwa Rais, madarasa ni kwa ajili ya wanafunzi kusomea na walimu kufundishia. Sasa hilo likikaa hivyo haliwezi kuwa zuri, lakini wanafanya hivyo kwa sababu ya dharura na kwa sababu hakuna nyumba za walimu. Naomba Serikali iweze kuliona hilo na hivyo ipeleke fedha kwa ajili ya nyumba za walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu TARURA. Unafahamu kabisa kwamba kwenye zile barabara za TARURA ndiko mazao yanakotoka. Sasa zisipotengenezwa vizuri, maana yake mazao hayawezi kutoka kule vijijini kuja mjini. Kwa hiyo, wananchi wale kila wanachokifanya kwa ajili ya kujikimu, kwa maana wamepata mazao yao, lakini yanashindwa kufika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, TARURA wameweza kujenga baadhi ya Barabara, lakini wameishia kwenye culvert. Sasa ni vema fedha ipelekwe ili kusudi ikamilishe eneo hilo. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamelalamika sana, nami nalalamika, naomba kwa kweli eneo hilo lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kwenye Kituo cha Afya cha Nguruka. Mheshimiwa Waziri anajua, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda pale Nguruka. Aliona Kituo cha Afya cha Nguruka ni chakavu, na aliahidi kwamba Mheshimiwa Rais amekwisha ahidi shilingi milioni 500 pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize hili, Mheshimiwa Mchengerwa, peleke shilingi milioni 500 kwenye Kituo cha Afya Nguruka. Nimekutaja ili uweze kushtuka... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Nashon.
MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naona umeshawasha mic. Nakushukuru sana.