Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Shabani Hamisi Taletale

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Kusini Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima siku ya leo. Pia, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuongoza vyema nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Yanga kwa suluhu yake ya jana. Najua kaka yangu Mwigulu atakuwa amefurahi angalau kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuanze na Wizara ya Michezo. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kwa kuileta hii sekta ya habari kwenye Wizara ya Michezo. Pia, kwa kutuletea Mheshimiwa Waziri ambaye ana taaluma ya michezo kidarasa, kaka yangu, baba yangu Mheshimiwa Prof. Mwaluko Kabudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kitu kikubwa sana kinakuja kwenye nchi yetu, hii Michezo ya CHAN na AFCON. Leo hii Uwanja wetu wa Arusha una 24%. Sijui Wizara mnatuambia nini kwenye hizi asilimia ilhali tayari michezo iko usoni? Mheshimiwa Rais ametoa fedha, lakini tunaanza kuona vitu vinasuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara isimame ituambie, nini kinasuasua? Sisi kama Kamati tumeweza kuwasukuma, na of course tumeenda pale kwenye viwanja, lakini mpaka sasa hivi tuna 24%. Ukimwuliza Mheshimiwa Waziri, ametuhakikishia kwamba ndani ya mwaka huu tunakwenda kukamikilisha vile viwanja. Tumeona mashindano ya hapa katikati, yamepelekwa mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Uwanja wetu wa Taifa wa Benjamin William Mkapa, yaani haujakamilika. Tukienda kwenye vyoo, juzi Prof. Kishimba alikuwa anazungumza, vyoo vya Uwanja wa Mkapa ni Hip Hop kama Naibu Waziri wake. Kwa hiyo, tuangalie, kama tunataka utaratibu wa kupokea watu, Mheshimiwa Rais anaonesha uwezo wa kutoa fedha kwenye Wizara hii, lakini kama tunataka kubadilika, basi tuwe wepesi, tuipunguze ile hali ya pale Kiwanja cha Benjamin Mkapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea zaidi, naomba kwanza nimpe pole Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Wanasema, kufiwa na mzazi hakuna umri. Mheshimiwa Waziri wa Elimu, kaka yangu Aldolf Mkenda pole sana. Sisi kama Kamati na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla tunakupa pole kwa kuondokewa na mzazi wako. Pia hili liende kwa kaka yangu Mheshimiwa Tarimba Abbas. Nampa pole vilevile kwa kumpoteza mzazi wake. Kupoteza mzazi, hakuna umri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudi kwenye sanaa. Leo hii unawaona wasanii wakiona kuna jambo la chama wanakuja wenyewe kwa gharama zao. Yote hii ni kwa sababu ya kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa yale ambayo ametufanyia. Mimi ni mmoja wa wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja nizungumze, kuna begi limetoka, ninamaanisha fedha ambazo zipo kwenye mirabaha. Hizi fedha ni nyingi kuliko miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba fedha hizi zigawiwe haraka kwa sababu wasanii wanataka kuona na kula matunda ya Mheshimiwa Rais wao ambaye leo hii wanatoka kifua mbele kuja kumsemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kidogo...

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

TAARIFA

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa kaka yangu Mheshimiwa Taletale, anavyochangia mchango wake, ni mzuri sana. Kwa kweli sasa hivi wasanii wanajitahidi sana hasa wa Kimila, wa Kisukuma. Kwa hiyo, Serikali ione kila sababu ya kuwawezesha, maana wanaimba vizuri nyimbo za Mheshimiwa Rais na kwa kweli wanaipa support sana Serikali yetu. Nilitaka kumpa taarifa hiyo tu kwenye mchango wake.

MWENYEKITI: Unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Maganga?

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante babu yangu wa Kisukuma. Nimepokea. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwa kaka yangu Mheshimiwa Mchengerwa. Leo hii tumepata matatizo ya mvua kwenye Kata yetu sisi ya Kiloka. Kuna Barabara ya Kiroka kwenda Mfumbwe daraja limevunjika tangu mwaka 2024 mwanzoni mpaka leo TARURA hawajasema chochote. Hali imekuwa ni mbaya. Ile barabara ilikuwa ndiyo chanzo cha watu kutoka kupishana kidogo na barabara yetu ya Bigwa Kisaki, lakini leo hii daraja limevunjika, hatuoni lolote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Elimu, kaka yangu Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda kwa kuniletea fedha ya kujenga shule ya sekondari na ufundi kwenye Kata yetu ya Tomondo, lakini kwenye hili tunaomba tupate walimu wa ufundi na vifaa ambavyo vitakwenda kuboresha kwenye ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwa kifupi sana, tunaona mabadiliko kwenye sekta ya elimu na tunaiona dhamira yake Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Tunaona kabisa kwamba tunakwenda kwenye elimu ambayo kile alichokisema Mheshimiwa Rais wetu ndicho tunachokwenda nacho. Sasa basi, sisi changamoto yetu kubwa ni walimu. Kila mtu akisimama hapa ni walimu. Sasa hatujui walimu wapo TAMISEMI au wapo kwenye Wizara yetu ya Elimu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya machache, nami naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)