Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami nichangie Wizara hizi mbili. Kwanza kabisa, naunga mkono hoja za Wizara zote mbili, lakini pia nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa katika Mkutano Maalum wa Chama cha Mapinduzi kuwa mgombea pekee wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nataka nielekee kwenye eneo la michezo, lakini mwishoni kama muda utaruhusu nitagusia elimu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tupate maendeleo ya michezo nchini na duniani kote ni lazima tuwe na vitu vitatu. Jambo la kwanza ni miundombinu ya michezo kwa maana ya viwanja na kadhalika. Jambo la pili, ni kuzalisha wataalam watakaofundisha michezo, na jambo la tatu ni kutengeneza wanamichezo wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili, kwenye eneo la miundombinu ni lazima kama Serikali tuwe na mkakati madhubuti ambao utakuwa na time frame, ambapo tutaweza kuweka miundombinu nchi nzima. Kwa sasa tunao uwanja mmoja tu. Tunao Uwanja wa Taifa ambao umekidhi vigezo vya kucheza michezo ya Kimataifa. Tunaamini sisi sote uwanja ule uko katika ukarabati mkubwa ambapo unachukua takribani zaidi ya shilingi bilioni 31. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tumefikia kule? Ni kwa sababu uwanja ule unakosa matengenezo ya mara kwa mara na unakosa ukarabati wa mara kwa mara. Ni lazima tuwe na mkakati, ama Wizara kupitia Serikali tutengeneze kitu ambacho kitaweza kuwa kinabakiza sehemu ya fedha inayopatikana kupitia ule uwanja ili sasa kukitokea kuharibika katika uwanja ule, basi ukarabatiwe kwa haraka (retention). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefikia kukarabati kwa fedha nyingi kwa sababu ya kulimbikiza matatizo, kwa sababu fedha zote zinazoingia zinakwenda kwanza Serikali Kuu, then kukitokea uharibifu, inatakiwa liandikwe dokezo, nani asaini, nani asaini, nani asaini mpaka ije ipatikane hiyo fedha, tayari uwanja ule unakuwa umeshaharibika zaidi. Kwa hiyo, kuwa na retention ni jambo muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la kutengeneza wataalam wa kufundisha michezo, ni lazima tuweke mikakati ya kuwa na vyuo vya kutosha ambavyo vitafundisha michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mheshimiwa Mbunge alisema hapa, Chuo cha Malya kinakwenda kwa kusuasua. Chuo cha Malya ni mkombozi wa michezo Tanzania, kwa sababu, ndiyo chuo pekee kinachofundisha waalimu wa kwenda kufundisha michezo kwenye majimbo yetu na wilaya zetu. Kwa hiyo, ni lazima kiishe kwa haraka zaidi na hatimaye twende kuinua michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la wanamichezo, hili ni lazima lifundishwe shuleni, nyumbani na kwenye maeneo mengine. Ni lazima Serikali iwe na mkakati kama vile ilivyokuwa Serikali ya China. Serikali ya China imeweka mkakati. Tangu mwaka 2016 Rais wake alizindua mkakati ama programu ya michezo inayoitwa The Fifty Point Plan, ambapo plan yao ni kwamba ifikapo mwaka 2050 waweze kushiriki Kombe la Dunia la FIFA na waweze kutwaa lile Kombe la Dunia la FIFA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika mkakati ule wamejiwekea mikakati kadhaa ndani yake. Mmojawapo, wamejiwekea mkakati wa kujenga shule 20,000 kwa ajili ya kufundisha michezo tu, hususan mpira wa miguu. Pia, wamejiwekea mkakati wa kujenga viwanja 70,000 ambavyo ni kwa ajili ya soka pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2016 hadi mwaka 2020 tayari zile shule zimeshaanza kufundisha michezo. Wanalenga mwaka 2050 wacheze Kombe la Dunia na watwae ubingwa. Wamejiwekea hiyo timeframe ili waweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara, maana kupitia Wizara ya Michezo, tayari kuna mkakati wa shule 56 ambapo shule zile zinakwenda kujengwa kwenye kila mkoa shule mbili kwa ajili ya michezo. Je, kama Tanzania kwenye zile shule 56 tunayo timeframe, kwamba mwisho mwaka fulani shule hizi zitakuwa zimekamilika zote na zitakuwa tayari zimeanza kufundisha michezo hiyo?! Ni lazima tuwe na timeframe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nikienda kwenye suala la elimu, ni kama ilivyokuwa tu kwenye michezo. Ili tuweze kuwa na maendeleo kwenye elimu, ni lazima tuwe na miundombinu ya elimu ya kutosha, tuwe na wataalam wenyewe wa kufundisha elimu yenyewe, kwa maana ya walimu, na ni lazima tuwe na watu ambao wanakwenda kupata ile elimu yenyewe, kwa maana ya wanafunzi. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la miundombinu, nampengeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli kwenye eneo la elimu sekondari tulikuwa tuna shida kubwa sana ya shule, lakini hivi sasa hakuna mwanafunzi ambaye anakosa kukaa darasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, upande wa elimu msingi nilikuwa naiomba sana Serikali, utaratibu ule ule uliotumika kwenye elimu sekondari, basi utumike na kwenye elimu msingi ili shule zetu ziweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuhusu wale wazalishaji ama wataalam wa elimu, kwa maana ya walimu, naipongeza Serikali, tumezalisha walimu wengi sana nchini, lakini baada ya kuzalisha walimu wengi nchini, je, tumewaajiri ili waweze kwenda kufundisha elimu sawasawa? Naomba walimu wa kutosha waajiriwe na shule zetu ziweze kupata walimu wa kutosha na hatimaye vijana wetu wapate elimu sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)