Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kusimama mchana huu kuchangia hoja za Kamati zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuteuliwa kuwa mgombea pekee wa Chama cha Mapinduzi, nafasi ya Urais mwaka 2025 kwa kura nyingi za kishindo alizopata kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwekeza na kujenga kwenye miradi mingi Tanzania; miradi mikubwa na miradi midogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja zetu za Kamati hasa Kamati ya TAMISEMI. Kwenye taarifa yetu ya Kamati, tumeeleza hoja nyingi, lakini moja kati ya hoja ambazo tumeeleza, mimi nitachangia hoja chache. Hoja ya kwanza kabisa ni kuhusiana na Shirika la Elimu Kibaha. Kwenye taarifa yetu tumeeleza vizuri dhumuni hasa la kuanzishwa kwa shirika hili ambalo toka zamani ilikuwa ni kuja kutoa elimu kwa ajili ya kuendelea na mapambano ya mambo matatu: umaskini, maradhi na ujinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya bado yapo, hayajaisha, lakini cha kusikitisha, Shirika hili lilikuwa linataka kuvunjwa. Hata hivyo, Kamati yetu ilimshauri Mheshimiwa Waziri, tunaomba hebu ajaribu kuangalia tena Shirika hili lisivunjwe, isipokuwa changamoto zilizopo kwenye Shirika hili zijaribu kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Mheshimiwa Waziri hoja hii aliichukua na ataifanyia kazi. Moja kati ya taasisi zilizopo kwenye Shirika hili ni pamoja na Chuo cha Afya Kibaha. Chuo hiki miundombinu yake ni chakavu sana, sana, sana. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anatokea Mkoa wa Pwani. Kwa hiyo, sina shaka anakijua vizuri sana Chuo hiki. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa yupo hapa, hebu atafute fedha ili wakafanye ukarabati kwenye Chuo kile cha Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo kile ni kati ya vyuo bora Tanzania, na wanafunzi wanaoomba kila mwaka kujiunga na chuo kile ni wengi. Wanaomba zaidi ya wanafunzi 5,000 lakini kwa kuwa uwezo wa Chuo bado ni mdogo sana kutokana pia na miundombinu, wanafunzi wanaochukuliwa pale ni 100, hivyo wanafunzi zaidi ya 4,000 wanakosa nafasi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atafute fedha kwenda kukarabati chuo kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa chuo kile bado kipo TAMISEMI, bado hakijahama popote. Kwa hiyo, namwomba Waziri wa TAMISEMI atafute fedha. Chuo kile kile bado kina eneo kubwa, kina ekari karibia 4,000, lakini kipo mjini sana. Ekari zile 4,000 ni pori. Kama ukipita pale Kibaha, ile stendi mpya, pori lote lile la kushoto ni eneo la chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lile ni very prime. Kwa hiyo, kwa sababu sasa zile hati hati za kufutwa kwa lile Shirika la Elimu Kibaha, hawajapata bado kibali cha kutumia yale maeneo yao, namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kukaa na kushauriana, Shirika la Elimu Kibaha wapewe kibali cha kutumia yale maeneo yao kwa sababu, kwa mfano kama lile eneo la mbele wanaweza wakatafuta wawekezaji na sasa hivi pia kupitia hii njia ya PPP wanaweza wakawekeza, kwani eneo lile ni prime sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nyuma ya chuo wanaweza wakatumia pia kwa ajili ya matumizi mengine na hata kwa baadaye sasa wanaweza wenyewe wakapata fedha yao kwa ajili ya kuendesha chuo na kufanya mambo mengine kama ukarabati mdogo mdogo wa miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Chuo cha Utumishi wa Umma, Hombolo kipo nacho TAMISEMI. Chuo kile nacho kina changamoto nyingi. Kwanza kabisa hakina watumishi wa kutosha. Pili, nyumba za watumishi; Kamati tulifaya ziara pale tulikuta nyumba ni moja tu ya two in one. Kwa hiyo, watumishi hawana makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, barabara ile ya kuingia chuo ni mbaya sana na barabara ile ni kilometa 24 tu. Kwa hiyo, namwomba pia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, na kwa sababu pia barabara ile nafikiri ipo TARURA na TARURA ipo TAMISEMI, hebu Mheshimiwa Waziri ajaribu kutenga bajeti kwa ajili ya barabara ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna changamoto za chuo kile cha Hombolo. Chuo kile kinadahili wanafunzi zaidi ya 6,000 sasa hivi, lakini capacity ya hostel za chuo ni wanafunzi 1,200 tu. Kwa hiyo, wanafunzi wanaokaa ndani ya chuo ni kama 20%, 80% yote wanakaa nje ya Chuo. Kwa hiyo, niendelee pia kumwomba Mheshimiwa Waziri kuwekeza nguvu kwenye Chuo kile hasa kwa ujenzi wa hostel na jengo la utawala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)