Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona na kunipatia nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wana-CCM wenzangu nchini Tanzania kwa maamuzi mazuri waliyoyafanya ya kumteua na kumchagua Mwenyekiti wetu na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura nyingi sana za kuongoza 2025/2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Wana-CCM kwa kumpa Dkt. Nchimbi kuwa mgombea mwenza na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wa Zanzibar 2025/2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu wengine wanasema hamkufanya vizuri. Mimi nadhani nafasi zipo kule, sisi wana-CCM tumeamua kwa kauli moja. Wale ambao wanashauri vingine, vipo vyama kule bado havijateua, waende wakashauri huko. Sisi kwa kauli moja Wana-CCM tumeamua kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiye atakuwa Rais wetu kwa sababu ya mambo makubwa aliyowafanyia Watanzania hii Awamu ya Sita. Amefanya mambo makubwa ambayo hayajapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo yaliyofanyika na watu wengine, lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa. Waheshimiwa Wabunge hapa mmesema miundombinu mbalimbali kama afya, elimu na kadhalika. Mambo ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu ambao wamejizima data wanasema kila kitu tunasema amejenga Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivi hawaelewi kwamba mwenye fedha, mwenye idhini hapa ya kila kitu; Waheshimiwa Wabunge wanachangia na wanatoa maombi hapa kwa Waheshimiwa Mawaziri ambao wapo hapa; na cheni ya mnyororo sisi ndiyo kiungo, tunawaambia Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Mawaziri wanamwendea boss Mheshimiwa Rais ndiye anayefanya shughuli hizi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukikuta kutoka kule Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji anamwambia Diwani, Diwani ananiambia mimi Mbunge, mimi naiambia Serikali, ndiyo Waheshimiwa Mawaziri wapo hapa na ndiyo sasa inafika kwa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, mambo yote anayefanya ni Mheshimiwa Rais. Wasijizime data kwamba kila kitu tunasema amefanya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ndio jemedari anayefanya mambo yote hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, anafanya kazi kubwa sana pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wasaidizi wake wote katika Wizara ya TAMISEMI. Kwa kweli Waheshimiwa Wabunge sisi wote hapa umeona Mheshimiwa Mchengerwa anafanya kazi kubwa, na huo ndiyo ukweli. Amekuwa akifika katika maeneo kuangalia shughuli zinavyoendelea pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wenzake, tunampongeza sana. Aendelee kuchapa kazi, tunamwamini, achape kazi pamoja na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri zilizofanywa, ombi langu ni kwamba, yapo maboma ambayo wananchi wamejenga. Sasa nizungumzie kwenye Jimbo la Makambako. Upande wa afya lipo boma la kule Mkolango, naomba sana tupate fedha tuweze kuwapelekea hao watu kule Mkolango, boma hili walishajenga, limeshaezekwa na limebakia tu kumalizia. Pia, lipo boma lingine la zahanati katika Kata ya Mjimwema, Mtaa wa Mjimwema nalo limefikia hatua wananchi wamefanya, tunaomba Serikali iweze kunena. Lipo boma lingine pale Kivavi, tunaomba na yenyewe zahanati hiyo iweze kumaliziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine linamwendea Mheshimiwa Prof. Mkenda, anafanya kazi kubwa sana. Alipokuja aliwaambia wananchi wa Wilaya ya Njombe hususan Mji wa Makambako, Halmashauri ya Makambako kwamba zipo fedha ambazo atatupatia za kujenga shule ya ufundi. Nimekuwa nikiwasiliana naye, fedha hizo tunazisubiri kwa hamu. Tunaomba fedha hizo ziende kwa wakati ili wananchi waweze kupata shule ya ufundi katika ukanda ule, kwani itawasaidia sana wananchi wa Jimbo la Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo ombi lingine kuhusu Hospitali yetu ya Halmashauri. Kutoka Mjini Makambako kwenda mahali ilipojengwa hospitali ni kilometa nane, na barabara siyo nzuri sana. Tunaiomba Serikali itutengee fedha kwa ajili ya kujenga barabara ya lami kutoka Makambako kwenda pale Mlowa ambapo ipo Hospitali ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miji ile 45 ambayo tulipata awamu hii ya 2025/2026 ya kujengewa soko, stendi na lami tunaomba tuongezewe. Tulipewa kilometa 20, lakini awamu ya kwanza wamesema watatupatia kilometa tano. Tunaomba tuongezewe kilometa mbili ziwe saba ili kusudi tuweze kufika kule kwenye Hospitali hii ambayo nimekuwa nikiizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine katika Mji wa Makambako kuhusu fidia ambayo imezungumzwa kwa muda mrefu kwenye suala la umeme wa upepo. Wananchi wa Makambako wamekuwa wakizuiliwa kwa takribani miaka zaidi ya 16 hadi 18. Katika maeneo yao hakuna kitu ambacho wanakifanya, na wanasubiri kulipwa fidia katika maeneo yao kwa ajili ya umeme wa upepo. Tumekuwa tukiahidiwa kwamba watalipwa mwezi huu au mwezi huu. Tunaomba sasa mwaka huu angalau Serikali ione namna ya kuwalipa fidia wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la soko na stendi. Namwomba sana Mheshimiwa Mchengerwa, wananchi wanasubiri kwa hamu. Katika miji ile 45 na Makambako ipo, soko na stendi na eneo ambalo tunajengewa la garden. Unajua garden ni muhimu sana kwa mjini kwa watu hasa wenye stress na kadhalika, na nini, waende mahali ili waweze kutulia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa soko na kutupa hiyo stendi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Deo Sanga, ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja. Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wote. Wachape kazi, mambo ni mazuri, ahsanteni sana. (Makofi)