Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika taarifa zote mbili za Kamati zilizotolewa leo hii. Kwa hakika Wenyeviti wetu wamefanya kazi nzuri ya kutengeneza ripoti nzuri na kuzisoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, nitangulie kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kupitishwa na Chama chetu cha Mapinduzi kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Oktoba hapa nchini. Kwa hakika hii nafasi hatukumpa kwa upendeleo, kwa kweli tumempa kwa sababu ya vigezo vya msingi ambavyo amevifikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu amefanya juhudi kubwa za kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga hatua katika sekta zote zikiwemo hizi ambazo zimezungumzwa leo hapa na Wenyeviti wetu wa Kamati. Kwa kweli kazi imefanyika kubwa. Nami napenda nitoe ushahidi katika Jimbo langu la Kilwa Kaskazini na Wilaya yetu ya Kilwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika sekta ya elimu tu, mwaka huu vijana wetu wa elimu ya sekondari wamefanya vizuri sana. Wale waliomaliza mwaka 2024, tumetokomeza zero kwa kiwango cha kutosha. Mwaka juzi tulikuwa na zero 137, mwaka huu tumepata zero 82 tu, lakini kwa mara ya kwanza katika Wilaya ya Kilwa tumetoa division one ya point saba kutoka shule ya Sekondari ya Kilwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kijana wetu anaitwa Sylivatory Gustavu Mangosongo amepata division one ya point saba kwa mara ya kwanza katika Wilaya ya Kilwa. Kwa hiyo, hii inatokana na juhudi ambazo zimefanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia na Mawaziri wa Wizara za kisekta ambazo leo zimezungumzwa hapa, tukianzia na Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza Mawaziri wote lakini, sana nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ya uwekezaji katika sekta ya elimu na sekta zote ambazo zimezungumzwa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, napenda kubainisha baadhi ya maeneo ambayo naona yanapaswa kuongezewa nguvu ili kuhakikisha kwamba sekta hizi ambazo zimezungumzwa leo katika taarifa mbalimbali ambazo zimetolewa ziweze kuwa na ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya elimu, ningependa kuiomba Serikali kuongeza juhudi za kuajiri walimu wengi ili waweze kutosha kufundisha vijana wetu na kuwawezesha kupata maarifa kwa sababu kuna upungufu mkubwa wa walimu. Kwa Wilaya ya Kilwa peke yake, kuna upungufu wa mamia ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kumekuwa na changamoto katika usimamizi wa taratibu za uhamisho. Leo ukienda katika Halmashauri zote za Wilaya, kuna upungufu mkubwa wa walimu unaotokana na kwamba walimu wakishaajiriwa tu, baada ya mwaka mmoja au miaka miwili, wengine wanatoa sababu za kuugua na kadhalika. Waliajiriwa wakiwa hawana magonjwa wala nini, lakini wakishapata ajira, basi wanatafuta sababu mbalimbali kama za ugonjwa ili kuhamia kwenye Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji. Kwa hiyo, naomba Serikali idhibiti hili jambo ili basi hata kule kwenye halmashauri za wilaya tuwe na walimu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la ujenzi wa nyumba za walimu, madaktari, ma-nurse na wote ambao wanahusika na hizi sekta ambazo nimezitaja. Nyumba ni tatizo, hivyo, baadhi ya walimu wanalazimika kukimbia maeneo mbalimbali ya kule vijijini kwa sababu hali ya maisha ni ngumu, hata makazi ya uhakika hakuna. Kwa hiyo, nilifikiri pia Serikali pamoja na kwamba imefanya kazi kubwa kwenye miundombinu ya madarasa, maabara na kadhalika, basi iangalie pia katika hili eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye usimamizi wa miradi kumekuwa na shida na changamoto kubwa, kuna wakati niliwahi kuwasiliana na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa TAMISEMI, kuna shule yangu pale inaitwa Namatungutungu, ile shule kwa kweli fedha zilikuja shilingi milioni 560 mwaka 2023, lakini mpaka hapa tunapozungumza ule mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na timu nyingi za uchunguzi zilizoletwa, hatujapata matokeo, hatua muhimu hazijachukuliwa juu ya wale waliohusika na ufisadi katika ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali irudi ikaangalie kwenye zile taarifa ambazo zimetolewa na zile timu, basi watupe majibu na wachukue hatua madhubuti katika kudhibiti masuala kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa VETA sasa hivi umesimama. Ulianza mwaka 2023, tukapewa matumaini utaisha ndani ya mwaka mmoja, lakini haujakamilika pale Namatungutungu katika Kijiji cha Njia Nne. Naomba Serikali kuangalia suala hili kwa makini na kuweka fedha za kutosha ili kukamilisha mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye zahanati na nyumba za waganga, jambo hili pia liangaliwe. Kuna maboma mengi ambayo hayajakamilika, hivyo katika bajeti ijayo, naomba Serikali waangalie waweze kuleta fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara za vijijini, kwa kweli barabara zangu zote katika jimbo zima zina hali mbaya. Juzi tulifanya tathmini, jumla ya kilometa 162 zimeharibiwa vibaya sana, madaraja yamevunjika, na mwisho wa siku hizo barabara hazipitiki. Kwa maana hiyo, zimesababisha ugumu katika utekelezaji wa miradi mingine kama ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hali ya maisha imepanda kwa sababu watu wanatumia bodaboda tu na vyombo ambavyo havina uhakika, lakini pia usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara umekwama au unafanyika kwa kuchelewa sana, na kwa maana hiyo hali imekuwa mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iziangalie barabara kutoka Kipatimu mpaka Pungutini, barabara kutoka Namayuni mpaka Namakolo - Mt. Kimwaga mpaka Kandawale - Njinjo mpaka Kandawale na hadi Ngalambi, na pia Kinjumbi hadi Mteramboko. Juzi tumefanya tathmini na watu wa TARURA zina jumla ya gharama ya shilingi bilioni 9.87 inahitajika kwa ajili ya matengenezao ya hizo barabara ambazo zimekufa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)