Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyoletwa hasa na Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, naomba nilishukuru Bunge lako Tukufu na Wabunge wote kwa namna mbalimbali waliyotufariji wakati wa msiba wa mama yangu mzazi, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwashukuru sana Wabunge wote waliochangia na hasa Kamati yetu. Tumepitia taarifa yao, tumeangalia maazimio, sisi tuko tayari kufanyia kazi. Kwa kweli wanatuongoza vizuri sana. Niseme kweli kabisa, Kamati yetu hii ya Elimu, Utamaduni na Michezo, wanatusimamia kweli kweli, lakini wanatusimamia vizuri na hasa kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya elimu hapa nchini. Kwa hiyo, tunapenda sana kuwashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la mageuzi ya elimu, suala moja ambalo limezungumzwa hapa na ambalo Mheshimiwa Rais alizungumza wakati anazindua Sera ya Elimu na Mafunzo, ni suala la walimu. Mheshimiwa Rais, alizungumza na ninadhani walimu wote nchini walimsikia, alisema katika mageuzi haya katika mduara huu katikati wako walimu. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa kuwa na walimu wa kutosha, na pia alizungumzia maslahi ya walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi kupitia wenzetu wa TAMISEMI na Utumishi, kasi ya kuajiri walimu imeanza kushika mwendo. Tunakwenda vile kwa sababu tunakubaliana na Wabunge wote, na kama alivyosema Mheshimiwa Rais wetu kwamba lazima tuongeze idadi ya walimu, na nilirudie tena, hili walimu wote hapa nchini walisikie. Alisema ni muhimu sana kuangalia maslahi ya walimu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, walimu wote hapa nchini wanasikia, na wengi wamenitumia message kwamba tuwasilishe shukrani zetu kwa Rais wetu kwa sababu anaonesha kujali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili la walimu, kuna suala moja ambalo ningependa nilifafanue, limezungumzwa hapa kwamba katika kuajiri walimu tuchukue aliyekaa mtaani muda mrefu zaidi au tuchukue ambaye amemaliza karibuni? Tuajiri tu bila kufanya usaili na mtihani au tuwalete wale walimu tuwapime tuangalie ni walimu gani ambao sasa hivi ni bora kufundisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala kubwa linazungumzwa, lina maumivu yake makubwa tunalielewa. Tunaelewa umuhimu wa watu waliyosomea ualimu kupata ajira, na tuna uchungu kwamba tungependa wapate ajira. Tunaelewa umuhimu wa wanafunzi kupata walimu bora, na tungependa wanafunzi wapate walimu walio bora na siyo tu bora walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya kuhakikisha kwamba walimu wanafanyiwa usaili, wanafanya mtihani, wala siyo ya Tanzania tu, iko katika nchi nyingine kama Ghana na nchi nyingine ambazo zimepiga hatua kubwa sana katika maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufikirie, wewe tunataka kwenda kumchukua mwanafunzi ajifunze Kiingereza, tunamtaka Mwalimu anayeweza kusema Kiingereza vizuri akafundishe. Wote wamesoma darasani, vyuo hivyo hivyo, na wakati wanasoma kwenye vyuo wamepishana. Kila wakifanya mtihani kuna aliye bora zaidi na ambaye siyo bora kama wengine, japo wote wamefaulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wengine wamemaliza miaka kumi iliyopita, mwingine amemaliza juzi. Ukiangalia maslahi ya yule mwanafunzi, utagundua unahitaji mwalimu bora. Ukiangalia huyu amekaa sana mtaani miaka kumi, kweli unaweza kutaka kutumia Mwalimu aliyekaa miaka kumi? Kwa hiyo, mageuzi haya ya elimu yanahitaji tuwe na walimu bora ili tuweze kufanikisha malengo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa wito kwa walimu wote waliosoma popote walipo, umekaa miaka kumi endelea kujiendeleza kwa sababu ukiitwa ukasailiwa, Mwalimu wa Kiingereza, natoa mfano wa Kiingereza, tukikuta huwezi kuongea Kiingereza, hatuwezi kukuajiri kwa sababu umekaa miaka kumi mtaani, itatuuma sana; lakini inauma zaidi kumpelekea wanafunzi Mwalimu ambaye kwa kweli hajaandaliwa vizuri. Suala hili ni la kisera, lipo katika sera kwamba utaajiriwa kwa kupitia mchujo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ukumbuke, walimu wanaoomba ajira ni wengi kuliko fursa zilizopo. Sasa unawachaguaje? Tuchague vipi walimu hao? Vigezo kwamba wamekaa muda mrefu zaidi; na hata waliokaa muda mrefu zaidi tunaweza tukaajiri wote? Kama hatuwezi kuwaajiri wote, walipokuwa wakikaa darasani walikuwa wanafahamiana, kuna waliokuwa wakishika nafasi ya kwanza kila siku na mwingine anashika nafasi ya mwisho, lakini kafaulu, na wanajua. Halafu wanakuja kuangalia aliyekuwa wa mwisho ameajiriwa, wanauliza, hivi nyie mnaajirije watu? Where is the meritocracy katika nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa usaili huo, tunachukua wale ambao mwenyewe ukijua kwamba hapa nimesailiwa bwana, hapa nimeboronga, unajua hukujuariwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wito wangu, watu waendelee kujiendeleza. Kwa kweli hali ni ngumu, lakini vilevile tunaangalia sana maslahi ya hawa wanafunzi ambao wanakwenda kufundishwa wapate walimu bora na siyo tu bora walimu. Kwa hiyo, kwamba una Cheti cha Ualimu, ni jambo moja. Siyo kwa nchi hii tu, nenda Ghana, nadhani hata Japan na nchi nyingine wanafanya hivyo. Hatuwezi kupenda kujilinganisha na nchi nyingine, lakini tukashindwa kuchukua maamuzi magumu kwa ajili ya kuendeleza elimu hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende katika mageuzi ya elimu hapa. Labda niongeze moja kuhusu mageuzi ya elimu. Haya ni maono ya Mheshimiwa Rais wetu, kila mmoja anafahamu, na bahati nzuri wakati wa uzinduzi tulionyesha documentary ya jinsi alivyokuwa anatoa maagizo tangu mwanzoni kwa sababu watu wanazoea, ukisema Rais wetu kafanya kazi nzuri, wanasema, hapana mnasifia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi upo. Hata pale ambapo hatuna Ushahidi, si kazi yake; wote tunafanya kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kwenye hili ni maono yake personal. Yeye mwenyewe alianza kulisema mapema kabisa hata mwezi mmoja haujapita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nieleze katika mageuzi ya elimu ambapo pengine tutapata muda wa kuyazungumza sana. Sasa hivi tunaelekea katika kujenga Polytechnics. Mtakumbuka vitu hivi vilianza kutoweka duniani, China hawakuviondoa, tunaanza mchakato na Katibu Mkuu sasa hivi anakamilisha kujenga Polytechnics ambazo zitakuwa ni High School za ufundi za miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga moja Mwanza, nyingine tutajenga Kigoma, tutajenga nyingine Mtwara, tunajenga nyingine Zanzibar kwa utaratibu maalumu kupitia mkopo kutoka China. Nyingine tunajenga Morogoro kupitia Korea; nyingine tumekamilisha hapa Dodoma na ujenzi utaendelea, na hayo ni maelekezo ya Rais wetu ili wale wanafunzi wanaosoma mafunzo ya amali ambayo sasa hivi tunatekeleza kwa awamu, kama mnavyofahamu mwaka 2027 ndiyo utakuwa ni mwaka ambao tutaanza kuhakikisha kwamba kila mwanafunzi anasoma miaka kumi, anaposoma shuleni. Anaenda katika mkondo wa amali, akimaliza form four, form five na form six yake ni miaka mitatu na diploma ya ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tuna maandaalizi kwamba akitoka pale, Diploma yake atakwenda kuchukua Mwanza, Kigoma, Mtwara, Morogoro, au hapa Dodoma chuo chetu cha ufundi tumekamilisha au ataenda kuchukua Zanzibar. Hiyo yote ni kazi ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kidogo kuhusu VETA. Wakati wote tunaangalia changamoto, tuangalie na mafanikio. Hizi changamoto tulizoziona zimezungumzwa, sisi na Wizara ya Fedha tunafanyia kazi tutazikwamua. Tuko very confident, tutasonga mbele na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu yuko hapa, lakini yale tuliyofanikiwa tusisahau kuyazungumza sana, kwamba sasa hivi tumemaliza VETA za ngazi ya mikoa, Simiyu, Geita, Njombe na Rukwa na mmeziona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni VETA nzuri sana. Tunajenga pale Songwe; sasa hivi tusisahau kuangalia VETA ambazo zimeshaanza kufanya kazi zinavyokwenda vizuri kadiri kazi inavyokwenda. Kwa hiyo, zile changamoto nyingine ambazo tumeziona, watu wamezungumza ni changamoto ambazo zisije zikasababisha watu wakasahau mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, sisi wenyewe tunaweza kwenda kwa wananchi, tukawaeleza changamoto mbalimbali, lakini tukasahau kuwaeleza kwamba uamuzi wa kujenga VETA 64 kwa kila Wilaya ni jambo la kushangilia. Hata kama kutakuwa na mkwamo kidogo, tunatarajia kumalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mengi ya kuzungumza, lakini nami ningependa kuipongeza sana na kuishukuru Kamati yetu na sisi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tunaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)