Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim kwa ruzuku ya uhai, lakini kutujalia afya ya leo kupokea Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge, kwa taarifa yake nzuri na tunayapokea mapendekezo yote ambayo yametolewa na Kamati, ambayo imekuwa inatusimamia vizuri kuhakikisha kwamba sekta hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inafanya kazi kama inavyotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namshukuru sana Mheshimiwa sana Shaban Hamisi Taletale, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki kwa mchango wake mzuri kuhusu suala la michezo na wasanii; na hivyohivyo Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu Mbunge wa Tunduru Kaskazini kwa hayo aliyoyaeleza kuhusu sekta ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, ilimpendeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 8 Desemba, 2024 kuunda Wizara mpya ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa kuiondoa Idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuiunganisha na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake, lakini kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Tumeshuhudia mambo makubwa katika sekta hiyo ambayo yameifanya Tanzania kuaminiwa kuwa mwenyeji na mshiriki wa Mashindano ya CHAN, lakini kuwa mwenyeji na mshiriki wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kuliarifu Bunge lako kwamba Tanzania, mwezi huu sisi tulikuwa tayari kabisa kuwa wenyeji na washiriki wa mashindano ya CHAN, lakini tulishukuru Shirikisho la Michezo la Africa, CAF kwa maamuzi yake ya kuyapeleka mashindano haya hadi mwezi wa Nane kuanzia tarehe 02, mashindano ambayo sisi Tanzania, Uganda na Kenya tutakuwa wenyeji na tutashiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko sababu za msingi kabisa ambazo ningependa wote mzifahamu, hazitokani na Tanzania lakini hali halisi ya maandalizi yanapokuwa ya nchi tatu, lazima wote mwende pamoja. Hamwezi kumwacha mwingine nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, watu wa Afrika Mashariki, tujipongeze, wenzetu wote walioandaa mashindano ya CHAN walipewa miaka miwili kuyaandaa kama ambavyo sisi tumepewa miaka miwili kuyaandaa ya AFCON, lakini kwa CHAN tulikuwa tumepewa miezi mitano. Sasa ndani ya miezi mitano huwezi kufanya maandalizi. Cote d’Ivoire walipewa miaka miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu wako watu wanaodhani kwamba limefanyika kwa sababu ya uzembe, hapana. Uhalisia unahitaji maandalizi zaidi ya miundombinu ya wachezaji ili kuhakikisha Tanzania tunakuwa siyo tu wenyeji wa CHAN, lakini pia washiriki wa CHAN na siyo ikiwezekana; tuingie fainali na tuchukue kombe la CHAN ili libaki hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika miundombinu ya michezo kama ilivyoelezwa na Kamati, nasi hatuna budi kumshukuru sana kwa fedha nyingi ambazo ametoa kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vipya, lakini pia kwa ajili ya ukarabati wa Kiwanja cha Benjamini Mkapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba ujenzi wa uwanja wa Arusha ambao mpaka sasa mkandarasi ameshapewa malipo ya awali ya shilingi bilioni 92.7 unaendelea vizuri. Ndiyo, umefikia 25%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba mpaka itakapofika Desemba mwaka huu, majukwaa yote tayari yatakuwa yamekamilika na kufikia Juni, 2026 ujenzi wote utakuwa umekamilika, na ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaendana na kujenga Mji mpya wa Arusha unaozunguka uwanja huo. Kwa hiyo, utakuwa siyo uwanja tu lakini pia litakuwa ni eneo la biashara, litakuwa ni eneo la utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Benjamini Mkapa, naishukuru Kamati ya Bunge kwa ufuatiliaji wa karibu kabisa wa ukarabati wa Uwanja wa Benjamini Mkapa, na ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati, maelekezo mliyotupa kwamba ifikapo mwisho wa mwezi huu wa Nne, ukarabati wa uwanja uwe umekamilika, utakuwa umekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tumefikia 80%. Tumefanya ukarabati mkubwa, viti vyote 60,000 vitabadilishwa, na vilivyopo kwa utaratibu utakaopangwa vitapelekwa katika maeneo mengine. Tayari taa 320 za kisasa zimeshafungwa kwa kiwango cha FIFA, yaani Daraja A na mfumo wote wa maji, umeme, TEHAMA, ulinzi na zulia la eneo la riadha limeshabadilishwa. Yamebaki maeneo kama hayo ambayo Mheshimiwa Taletale ameyaeleza ya vyoo na mambo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka kuwahakikishia kabisa kwamba, Uwanja wa Benjamin Mkapa utakuwa tayari kwa mujibu wa maagizo ya Kamati ya Bunge, nasi tuko tayari kwenda na ninyi kwa tarehe iliyopangwa ili tuweze kuona kazi kubwa iliyofanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Uwanja wa Dodoma ambao umekuwa kizungumkuti kwa muda mrefu, nataka niwaambie sasa, Alhamisi ya wiki hii tarehe 13 Februari, 2025 tunasaini mkataba wa kuanza kujenga Uwanja wa Dodoma utakaojengwa katika eneo la Nzuguni. Mkandarasi amepatikana, na fedha ya kuanza ujenzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Waziri wa Fedha, ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ameshaiandaa check kwenye exchequer inayokuja ya kuhakikisha kwamba uwanja huo unanza kuajengwa. Utakuwa ni uwanja wenye uwezo wa kubeba watazamaji 32,000 kwa wakati mmoja. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameifanyia Tanzania mambo makubwa na ameifanyia Dodoma mambo makubwa. Kwa ujenzi wa uwanja huu, ni kweli sasa Dodoma ni Makao Makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli nyingine zinaendelea. Pale pale katika uwanja huo mkubwa utakaojengwa, tunajenga kituo cha michezo changamani (Sports and Recreation Center), ambacho kimefikia 67%. Kwa hiyo, michezo kama Basketball, Handball, Netball na uogeleaji itafanyika pale, pia na burudani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo hilo litakuwa na uwanja huo mkubwa, lakini pia na kituo changamani (Sports and Recreation Center). Wakati huo huo maendeleo mengine yanafanyika katika viwanja vingine vyote ambavyo vitatumika na CHAN na AFCON. Mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri, kila wiki tunafuatilia maendeleo ya ujenzi wa viwanja hivyo na ukarabati wa viwanja hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limezungumzwa na Kamati na wachangiaji, ni kuhusu Chuo cha Maendeleo ya Michezo, Malya. Ninavyozungumza hapa, tayari Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametuletea taarifa kuwa exchequer ya shilingi 1,500,000,000 imetoka kwenda Chuo cha Malya, kuendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo ya Michezo, Malya, kimejipanga kutoa mafunzo ya Wandishi wa Habari ya Michezo (Media and Sports Journalism). Kwa hiyo, nawaomba watu wote wanaopenda kuwa wachambuzi wa michezo na wanaoandika habari za michezo kutumia fursa hii sasa ili kwenda kujifunza Media and Sports Journalism kule katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo, Malya.
(Hapa kengele ililia kuashira kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako nimalizie moja. BAKITA wanafanya kazi kubwa sana na sasa tumeanza mchakato wa kuiunda upya BAKITA ili ifanane na majukumu iliyopewa ya kukipeleka Kiswahili duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, BAKITA wamefanya kazi kubwa sana, naomba nieleze. Wametoa Kamusi ya Kiswahili kwa Shule za Msingi. Kamusi hii ni Kamusi muhimu sana. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote wahamasishe shule za msingi zote zipate nakala ya Kamusi hii ya Kiswahili kwa Shule za Msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamusi hii ni ya aina yake kwa sababu kila neno imekupa jinsi ya kulitumia katika kila sentensi. Nimeongea hapa na Waziri wa TAMISEMI, naye ataizungumzia. Kamusi hii ni muhimu sana na ni vizuri sana wote wawe nayo. Kuhusu bei, tutatafuta bei ambayo TAMISEMI watamudu kuzinunua zote. Kwa hiyo, tutakaa tuongee ili TAMISEMI wazinunue zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mimi nina hakika kabisa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuipa BAKITA fedha ambayo imetoa Kamusi hii ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo ninamaliza nalo kuhusu Kamusi, ndugu zangu Watanzania, nchi ya jirani ndiyo inayonunua Kamusi kutoka Tanzania kuliko sisi wenyewe. Ndio wanaonunua Kamusi kwa mwaka takribani nakala 50,000 mpaka 100,000. Sisi tukiuza 100 tunamshukuru Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuhamasishe matumizi ya Kamusi, tuhamasishe kununua Kamusi ili Kamusi yetu itumike pia na watoto wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yalikuwepo mengi sikujua, kumbe muda unakwenda kasi. Basi mengine niyabakize Inshallah katika vikao vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)