Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu linapita katika mageuzi makuu ya utekelezaji wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ikiwa ni ndoto za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyesema: “Uhuru bila kujitegemea hasa kwenye mambo ya msingi, unaweza kutumika vibaya kama silaha ya kutuangamiza na ukawa ni uhuru bandia.” Waziri wa Fedha ameshazungumza hapa kwa kina, na hili pia nilitamani Waheshimiwa Wabunge watuelewe kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, miradi mikuu ya kimkakati ambayo Serikali imeamua kuifanya yenyewe, pamoja na mambo yale ya msingi ambayo Baba wa Taifa alituusia kwamba haya siyo ya kuwaachia wengine wayatekeleze, ni sisi Serikali kujipanga na kuyatekeleza wenyewe. Hii ni pamoja na chaguzi zetu. Tumejionea Uchaguzi Mkuu huu unaokuja, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Serikali imefanya yenyewe kwa 100% na fedha hizo zimetafutwa na Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua vita ya mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi, imeshika kasi sana chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia na chini ya wasaidizi wake wa karibu ambao ni wawakilishi wa wananchi, Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo imefanyika ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Unapoizungumzia TAMISEMI, unaizungumzia Nchi, Wabunge, Wakuu wa Mikoa 26, Wakuu wa Wilaya 139, Wakurugenzi kwenye Halmashauri 189, Wabunge wa Majimbo 215 na Wabunge wa Viti Maalum, jumla 393. Unawazungumzia Maafisa Tarafa 570, Watendaji wa Kata 3,958, Wenyeviti wa Vijiji 12,333, Wenyeviti wa Mitaa 4,269 na Wenyeviti wa Vitongoji 64,274.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema niyaseme haya kwa sababu kila Mheshimiwa Mbunge hapa ni shahidi. Kazi iliyofanywa kwenye majimbo haya 215 yaliyopo Tanzania Bara ni kubwa sana. Kazi kubwa sana imefanyika kwenye kila halmashauri, wilaya na mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukiri, tunazungumza hapa ukarabati na ujenzi wa majengo mbalimbali ya miundombinu kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu ambayo Wabunge wengi wamechangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zilizojengwa, vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za halmashauri haukujengwa kwa bahati mbaya. Ni kwa sababu kwanza, kumekuwa na dhamira ya dhati kutoka Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia ya kwenda kuwahudumia Watanzania wa kawaida kabisa kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mafanikio haya ya Serikali ya Awamu ya Sita, hayawezi kuzungumzwa bila kutaja wawakilishi wa wananchi (Wabunge) ambao wamefanya kazi kubwa sana ya kuishauri Serikali, kutoa maoni, maelekezo ambayo Serikali imekwenda kuyatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iliposomwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wabumbe walikuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Wajumbe wengine, wakaamua. Hawakuamua kwa bahati mbaya, ni kwa sababu kazi imefanyika katika kila kona ya nchi yetu. Pia, hii ndiyo sababu tunayo miradi inayoendelea katika maeneo ya majimbo yetu. Kila kona ya nchi hii na kwenye kila tarafa, ipo miradi inayoendelea. Kama siyo mradi wa elimu, mradi wa afya; kama siyo ujenzi wa zahanati ni kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeona kwa kazi hii kubwa ambayo Waheshimiwa Wabunge wameifanya, na kwa muda tuliobaki nao ni dhahiri kwamba, Viongozi Wakuu wa Nchi na Waheshimiwa Mawaziri hawatakwenda kila jimbo kukagua na kufungua miradi ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue fursa hii, kuwapongeza watendaji ndani ya sekretarieti za mikoa, na halmashauri zetu. Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kwa sababu watendaji ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuanzia kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Kata na Maafisa Tarafa wamefanya kazi nzuri sana kwa Taifa letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawataja hawa kwa sababu Wizara zote hizi zinapokwenda kule zinawakuta watendaji hawa waliopo chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Inapokwenda kutekelezwa miradi ya maji, utawakuta kule watendaji ndio wasimamizi na ndio wanaofanya kazi nzuri. Tunapokwenda kwenye miradi ya umeme, utawakuta Watendaji Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, ndio wasimamizi na wanaosaidia kuhakikisha kwamba fikra za Rais wetu zimetimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa tunayo miradi mingi ambayo bado haijafunguliwa, na kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge hawa wamefanya kazi nzuri, nichukue fursa hii kuwaelekeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri, kuwapangia Wabunge hawa miradi yote ambayo haijazinduliwa, waende wakaizindue mara moja katika majimbo yetu yote 215. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa waandae utaratibu ule ule, kama anakwenda Waziri, kama anakwenda kiongozi wa juu kabisa, waende wakazindue miradi hii, kwa sababu Wabunge hawa ndio waliosemea miradi hii hadi ikashuka kule kwenye majimbo yetu. Wabunge hawa wamefanya kazi kubwa na nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo hoja hapa zimezungumzwa na Kamati na sisi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumezipokea hoja zote. Nikuhakikishie, tunakwenda kuzitekeleza hoja zote ambazo Kamati imeshauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kuhusu Shirika la Elimu Kibaha. Tunatambua umuhimu na historia ya Shirika hili la Elimu Kibaha. Niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, tayari tumeshapeleka maoni ya Wizara yetu kwa mwenye mamlaka kuona uwezekano wa kufanya mapitio upya, ili Shirika la Elimu Kibaha liendelee kufanya kazi kwa misingi ambayo tutakwenda kufanya maboresho makubwa katika Shirika la Elimu Kibaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu watumishi katika sekta ya ardhi. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tayari Serikali imeridhia watumishi wote katika sekta ya ardhi kurejea Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili waweze kusimamiwa vyema na Madiwani katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kuhusu miradi ya Benki ya Dunia. Natambua ni fikra za Rais wetu kwenda kuboresha, kufanya miji kuwa majiji, na kupanua vijiji kuwa miji; na tunatambua kwamba miradi hii ya Benki ya Dunia yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.18, lakini tulikuwa na changamoto kidogo ndani ya Serikali, tumeshazikwamua. Niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kuwa wakandarasi wote kuanzia wiki ijayo wataanza kupata fedha za ujenzi wa miradi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu uharibifu wa barabara zetu. Kwenye miradi hii natambua wapo Waheshimiwa Wabunge ambao waliongoza kuhakikisha kwamba wanaleta ushauri wao ndani ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Hawa ni Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mheshimiwa Kanyasu na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao katika maeneo yao walifanya kazi nzuri ya kutushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwathibitishie kwamba utekelezaji wa miradi hii utaanza kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, yaani kuanzia mwezi wa Tatu miradi yote ambayo ilikuwa imebaki, itaanza kutekelezwa. Ni wakati wenu Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, ninyi mmefanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie. Mambo ni mengi, tumepokea hoja hii ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, namwelekeza hapa Katibu Mkuu kuhakikisha kwamba, anapeleka fedha kwenye Kituo cha Afya cha Maili Tano, kama ambavyo kimewasilishwa. Tunatambua Mheshimiwa Kingu amezungumza kuhusu Puma, Katibu Mkuu alishatuelekeza. Nawaelekeza TAMISEMI kuhakikisha kwamba, fedha hizo zinakwenda kuongeza madarasa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhusu Ngorongoro. Niwakumbushe wasaidizi wangu kwamba wahakikishe wamepeleka mabweni katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ngorongoro na kuhakikisha zahanati ambazo zilipaswa kujengwa zinajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie. Waheshimiwa Wabunge walilalamika sana hapa kuhusu miundombinu, kila kona miundombinu. Naomba niwathibitishie, Mheshimiwa Rais wetu kupitia fedha za Miradi ya Benki ya Dunia, tayari ametukabidhi takribani shilingi bilioni 247. Fedha hizi, kwa vilio vya Waheshimiwa Wabunge, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia TARURA tumepokea taarifa, waraka, kutoka kwenye kila Mkoa, maeneo ambako kuna changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, shilingi bilioni 247 zitakwenda kila jimbo la nchi hii kwa namna ile ile ambayo Mameneja wa TARURA kwenye kila mkoa wametuletea. Fedha hizi zitaanza kutumika kuanzia mwezi wa Tatu mwaka 2025. Kwa hiyo, naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kuwa tunapeleka fedha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vituo vya afya, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameshasema hapa kwamba, Ijumaa hii tutapitisha waraka ambao utaletwa ndani ya Bunge, na kuanzia wiki ijayo vituo vyote vya afya vya kimkakati ambavyo Mheshimiwa Rais aliwaahidi Waheshimiwa Wabunge, vitakwenda kwenye majimbo yenu. Tutaanza kutoa shilingi milioni 300, na pia tutakarabati zahanati na maeneo mengine ambayo yatakuwa yamebaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo, lakini nichukue fursa hii kuunga mkono hoja kama ilivyowasilishwa na Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana kwa Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie. Natambua inawezekana kabisa katika maeneo yetu kukawa na changamoto mbalimbali. Inawezekana kabisa Taifa letu ni changa, lakini lazima tukiri, Rais wetu amegusa kila kona ya nchi hii, kila sehemu ya nchi hii ameigusa, na mimi nina imani kwamba, Wajumbe hawatatuacha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge hawa wamefanya kazi nzuri maeneo yote. Pengine Mheshimiwa Mbunge ambaye hatafanya vizuri itakuwa ni nongwa tu za Wabunge, lakini Wabunge hawa wamewasemea wananchi katika maeneo yao yote. Wamezungumza kero za wananchi, na Rais wetu ametekeleza zile hoja zote ambazo Wabunge hawa, Wawakilishi, walikuja hapa Bungeni wakawasemea wananchi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Watanzania, kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambayo 76% ya Watendaji, wako chini ya Ofisi hii ya Rais, TAMISEMI, basi, wahakikishe yale maelekezo ambayo yamebaki katika maeneo yao wanayatekeleza, ili Wabunge hawa watakaporudi kule majimboni wakute maeneo yao yote waliyoyasemea yamekamilika, ili wananchi waweze kuona umuhimu wa kuwarejesha Waheshimiwa Wabunge hawa ambao wamefanya kazi nzuri sana kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie. Kama isingekuwa Katiba na Kanuni ndani ya chama, mimi ninaamini Wajumbe wa Mkutano Mkuu huko kwenye majimbo wangewarudisha Wabunge hawa hata kabla ya uchaguzi, kwa sababu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita yametekelezwa na yeye mwenyewe Rais Dkt. Samia, na wapo wasaidizi waliofanya kazi hii ambao ni Wawakilishi wa Wananchi, Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja (Makofi)