Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia, nawashukuru sana wachangiaji wote waliochangia. Takribani wachangiaji wote waliosimama waligusia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, wachangiaji wote walio kwenye orodha, wamechangia kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye hoja, kwanza namshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Sisi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tumepita maeneo mengi sana kwa sababu, tunagusa wananchi. Kwa hiyo, tumeona jinsi ambavyo miradi mingi mikubwa inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali, na kauli ya kinafiki na kauli ya ukweli ni rahisi sana kuijua kwenye nyuso za watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye nyuso za wananchi wa Tanzania tumeona mioyo ya dhati ya upendo kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ndiyo maana hata maamuzi ya Mkutano Mkuu yaliyofanyika ya kumpitisha yeye pamoja na mgombea mwenza hayana upinzani wowote kwa wananchi kwa sababu ya kazi zake ambazo amezifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutembea kule na kujionea, tuna uhakika wa kwamba kazi ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejiuza yenyewe. Hata uchaguzi wenyewe hautakuwa mgumu kwa sababu tayari impact imeonekana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni fahari kwangu, kama Mwenyekiti wa Kamati, kuwa na Waziri anayeelewa kazi yake na ambaye ameweza kuelezea hapa mambo mbalimbali ambayo yanafanyika. Katika Kamati, hatupati ugumu wa utendaji wa majukumu yetu kutokana na umahiri wa Wizara hii inayoongozwa na Waziri, Mheshimiwa Mchengerwa, Manaibu wake wote wawili na pia, Makatibu Wakuu na viongozi walioko kwenye Wizara hii. Tunapata urahisi kwa sababu, tunasikilizana, tunaelewana na ushauri wetu tukiutoa unakubalika. Tunaamini hayo yataendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhitimisha, wengi waliochangia wamezungumzia mambo ambayo tayari yameshapata maelezo ya kutosha ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa hiyo, kama nikirudia, nitakuwa narudia mambo ambayo tayari yameshasemwa na wakati mwingine naweza nikaharibu ule utamu ambao wameyatolea maelezo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Kamati, tunaendelea kusisitiza kwamba, ikiwa mambo yote haya yaliyoahidiwa hapa yatatekelezwa, basi tuna uhakika kwamba, wananchi wataendelea kupata manufaa, wataendelea kufaidika na wataendelea kuipenda Serikali yao ya Chama cha Mapinduzi, ambacho hakitarajii kuondoka madarakani siku za karibuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe na maneno mengi. Baada ya maelezo hayo ya kina na uhitimishaji wangu wa hoja ambayo niliitoa, sasa naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kuikubali Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)