Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU, UTAMADUNI NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuja kuhitimisha hoja yetu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kwenye hoja, nitumie fursa hii kuungana na wachangiaji wote waliochangia hivi leo kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta zote za maendeleo nchini. Naomba nitumie muda mfupi kutoa mifano miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani, aliikuta Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwa na bajeti ya takribani shilingi bilioni 35, lakini tunavyozungumza, ameipandisha mpaka kufikia takribani shilingi bilioni 285. Ongezeko hili ni kubwa, la makusudi na tunaiona political will kwa Mheshimiwa Rais katika kuleta mapinduzi ndani ya sekta ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa eneo la Bodi ya Mikopo peke yake nchini, mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu, Rais alikuta bajeti ya takribani shilingi bilioni 400, lakini tunavyozungumza sasa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipandisha bajeti mpaka kufikia takribani shilingi bilioni 800. Ni takribani mara mbili ya bajeti ambayo ameikuta. Ongezeko hili ni kubwa na tunaiona nia ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa dhati ya moyo Wangu, kwanza kuwashukuru wachangiaji wote ambao wamechangia katika hoja yetu ya Kamati katika maeneo mawili; kwanza upande wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na pili, upande wa Habari Utamaduni na Michezo. Mheshimiwa Kamamba, Mheshimiwa Dkt. Ntara, Mheshimiwa Hamisi Taletale, Mheshimiwa Kungu, Mheshimiwa Prof. Mkenda na Mheshimiwa Prof. Kabudi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee sana nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Prof. Kabudi na Mheshimiwa Prof. Mkenda, kwa kutusaidia kutoa ufafanuzi wa kina kwa hoja za Waheshimiwa Wabunge. Kwa kweli, wamerahisisha kazi yangu ya kuhitimisha hoja, na sitatumia muda mrefu sana kwa sababu mengi ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge, Mawaziri, hawa wawili wameyatolea ufafanuzi. Nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile namshukuru sana Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ameahidi kuendelea kutoa fedha. Kwa kweli, tuna imani kubwa na Serikali kwamba fedha ambazo zimeahidiwa zitatoka na zitakwenda kutekeleza mambo yote ambayo yamewekwa katika taarifa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ambazo zimezungumzwa zaidi na Waheshimiwa Wabunge, hoja ya ajira ya walimu na sisi tunaiona na Mheshimiwa Profesa Mkenda ameitolea ufafanuzi, lakini Kamati tuna shauku ya kuona tunaanza ule utaratibu wa internship ya walimu ambao wamehitimu vyuo kwa muda mrefu, ili kuendelea kuwaimarisha walimu ambao wapo mtaani waweze kuwa bora na hata ikitokea interview, nao wawe katika nafasi nzuri ya kuweza kufaulu na kupata ajira kama ambavyo wanapata walimu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumziwa masuala ya maslahi ya Walimu na Wahadhiri. Sisi kama Kamati, tumeyaona na tungependa kuendelea kuishauri Serikali kama ambavyo ametamka Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba, anakwenda kuboresha maslahi ya Walimu. Basi na sisi shauku yetu ni kwenda kuona kweli maslahi yametekelezwa na kazi kubwa tulionayo hapa ni kuwasilisha maoni ya wananchi kwa sababu, sisi ni wawakilishi wa wananchi katika nyumba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni kuhusu VETA yamefafanuliwa vizuri na Mheshimiwa Prof. Mkenda. Shauku yetu ni kuona kwamba, yanatekelezwa kama ambavyo yameahidiwa katika Bunge lako Tukufu. Miundombinu ya shule na vyuo vikuu vilevile tunaomba maoni yetu ya Kamati katika eneo hili yaweze kuzingatiwa, kama ambavyo yametolewa mapema asubuhi ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vifaa vya kufunzia na kujifunzia, maoni ya Kamati yamejitosheleza na tungependa tu Serikali iendelee kuyachukua na kuyafanyia kazi kama ambavyo yametolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Ujenzi wa Uwanja wa Dodoma na Uwanja wa Arusha, hili eneo ni mahususi kwa sababu, kwa bahati nzuri Mheshimiwa Prof. Kabudi amefafanua kwa upana zaidi, lakini tuna shauku kama Watanzania kuwa wenyeji wa Michuano ya CHAN na AFCON, tuna shauku siyo ya kushiriki, ila kwenda kwenye ushindani. Tunatamani kuona maandalizi yanafanyika vizuri, Timu yetu ya Taifa inaandaliwa vizuri na mwisho wa siku tuwe sehemu ya ushindani na siyo kushiriki, kama wenyeji wa michuano hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika maandalizi hayo viwanja, kama ambavyo amesema, vinajengwa na hali siyo mbaya. Ukarabati unafanyika Benjamin Mkapa na ujenzi unafanyika katika eneo la Arusha na hapa Dodoma tumesikia Mheshimiwa Waziri anakwenda kusaini mkataba. Yote hayo tuna imani yatafanyika katika muda uliopangwa, na mwisho wa siku sisi, tukiwa ni wawakilishi wa wananchi, tutafarijika katika utekelezaji wa maeneo yote hayo ambayo yamezungumziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa kuzingatia hoja zote ambazo zimezungumzwa hapa na kwa kuzingatia ahadi za Serikali zilizotolewa na viongozi, Waheshimiwa Mawaziri, ndani ya Bunge lako Tukufu, nashukuru sana kwa fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)