Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kutengeneza hotuba nzuri na pia na taasisi yake kiujumla, wameweza kutupatia makabrasha ambayo yatakuwa ni msaada kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kulichangia ni masuala mazima ya kuhusu vijiji. Vijiji vyetu ambavyo vilitangazwa mwaka 1974 tuna matatizo ya mipaka; tunaomba Mheshimiwa Waziri kwa kupitia Halmashauri zetu na taasisi zilizopo mipaka mingi kwa sasa hivi haijulikani, kwa hiyo, kumekuwa na uingiliano na matumizi ya kilimo. Hii inasababisha mpaka wananchi wetu wanapata matatizo. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Jimbo la Nsimbo, Mkoa wa Katavi, eneo la kwenda Kata ya Ugala limekuwa na matatizo sana ya kujua mipaka ya kijiji iliishia wapi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika upande wa ardhi tunajua wamefanya kazi yao na wanafanya vizuri, lakini kuna mamlaka ambazo wanaingiliana! Tutahitaji waweze kukaa kwa pamoja ili tu wapate ufafanuzi na wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuishi. Mamlaka ya Hifadhi ya Misitu; tunahitaji wawe na mawasiliano ya karibu ili mipaka ambayo Mamlaka hii ya Hifadhi ya Misitu ambayo inaitoa na wakihusisha pia na Wizara ya Ardhi kwa kupitia hizi Halmashauri zetu waweze kuwa pamoja kwa sababu, sehemu nyingi kumetokea mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jinsi anavyoshughulikia migogoro. Halmashauri yangu na mimi binafsi nitaleta maombi, tumekuwa na migogoro kutokana na idadi ya watu kuongezeka. Maeneo mengi ya nchi ya Tanzania yamekuwa sasa hivi yanavamiwa kwa sababu ya ongezeko la watu. Watu wameongezeka na hasa wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Halmashauri ya Jimbo la Nsimbo maeneo mengi yameingiliwa na hasa ya hifadhi za misitu, ardhi imekuwa ni haba. Sasa kuna mpango ambao Mheshimiwa Waziri ameuzungumza wa matumizi bora ya ardhi, lakini tuna tatizo la bajeti katika hizi Halmashauri zetu. Sasa tungeomba kwa upande wa Wizara waweze kusaidia, kwa kuwa wanaweza kupata mafungu aidha, kupitia taasisi nyinginezo. Tunajua kwenye bajeti itakuwa haitoshi, lakini kama Waziri anavyotumia jitihada kuwapata wafadhili mbalimbali, ili fedha ipatikane kwa ajili ya huu mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa sababu, kuna maelekezo mengi ametoa kwamba Halmashauri zetu ziweze kupima maeneo, lakini shida ni bajeti iko finyu kwelikweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, bajeti ya mwaka 2016/2017 ni shilingi bilioni 14 na bajeti inayoishia 2015/2016 ni shilingi bilioni 14, kwa hiyo, hatujapiga hatua! Matokeo yake ni kwamba, miradi mingi haiwezi kuja kufanyika. Sasa kama Wizara itaweza kusaidia Halmashauri zetu kwa kupata fedha sehemu nyingine, litakuwa ni jambo bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni masuala ya utapeli kuhusu viwanja vyetu. Tunaomba Wizara iangalie mpango ambao utakuwa ni mzuri kwa watu wanaohitaji kununua au kuuza viwanja. Ni kweli, Wizara inatoa huduma mtu akitaka kufanya searching anafanya na anaona jina kabisa pale, Mheshimiwa Richard Philipo Mbogo, lakini kuna tatizo Hati hizi zinavyotoka hazina picha moja kwa moja, sasa zingeweza kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kesi nyingi sana za watu wametapeliwa kuhusu uuzaji wa nyumba au viwanja katika maeneo mengi sana ya nchi yetu. Sasa tuombe Wizara itengeneze mpango mzuri ambao utasaidia kupunguza watu kutapeliwa na ndio maana ukipita sehemu nyingi mijini unakuta imeandikwa “Nyumba Haiuzwi” kwa sababu, watu wengi tayari wameshaingia katika hali ya utapeli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Wizara imeweka suala la TEHAMA, maana yake hutumia teknolojia katika kupata taarifa zake na kufanya kazi sehemu mbalimbali. Kwa sababu, sehemu nyingi Mkongo wa Taifa bado haujaanza kufanya kazi, basi tunaomba Serikali iweze kuhakikisha kwamba, Mkongo huu unafanya kazi ili tuweze kuhakikisha kwamba, Halmashauri zetu zinakidhi mahitaji ambayo Wizara inaweza kuagiza katika Hotuba ya Waziri ambayo ameitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba sasa kwa upande wa Wizara tuongezewe huduma mikoani, watu waweze kupata Hati. Tuna makazi mengi ya vijiji, watu wengi hawana Hati, kwa hiyo, ikitokea pale mtu anahitaji dhamana Mahakamani, anahitaji apate mkopo, watu wengi hawana Hati. Kwa hiyo, tutaomba zile gharama kwa upande wa vijijini zishushwe ili watu waweze kupata Hati na hata hizo za category karibu tatu ambazo ameweza kuzieleza Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naunga mkono hoja na naomba Wizara iendelee kutimiza wajibu wa Serikali. Ahsante sana.