Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupembe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi na Naibu Waziri wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayofanya katika kutatua migogoro. Ni kweli migogoro imepungua sana ukilinganisha na siku za nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze na jambo moja hasa kuhusu property tax (kodi za majengo). Kodi hizi ni kubwa mno ukilinganisha na kipato cha wananchi hasa wastaafu na wale wenye kipato cha chini, inakuwa vigumu sana kwao kuilipa. Kwa mfano, mfanyakazi ambaye amestaafu alikuwa anapata kima cha chini amejenga nyumba yake yenye thamani ya shilingi milioni 40, anatakiwa kulipia kodi Sh. 46,000 kwa mwaka na ukigawa kwa mwezi ni kama Sh. 3,840 hivi, kodi hii ni kubwa. Kwa hiyo, tuombe Serikali ijaribu kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hizi za majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Sheria ile ya Ardhi hasa inayosema juu ya vyanzo vya maji kwamba mwananchi haruhusiwi kujenga mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji au kwenye kingo za mto. Hii sheria kwenye maeneo mengine hasa ya nyanda za juu (highlands) haitusaidii sana au inawaathiri sana wananchi. Kwa mfano, utakuta kuna milima midogo na kutoka mlima mmoja mpaka mwingine au kutoka bonde mpaka bonde, ukipima kutoka kwenye kingo za maji mpaka unapoishia mlima utakuta unafika kwenye mlima pale katikati kwenye kigongo cha mlima. Kwa hiyo, maana yake hilo eneo utakuta milima miwili au mitatu hawaruhusiwi wananchi kujenga maeneo hayo kwa sababu ya sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Sheria hii ya Ardhi iwe applicable kwenye baadhi ya maeneo lakini kwenye maeneo ya milimani angalau waweze kupunguziwa zile mita 60 ziende kwenye mita 30 au 20 hivi ili wananchi nao waweze kujenga kwenye maeneo hayo vizuri zaidi kama ilivyo katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia jambo lingine ni migogoro hii ya mipaka. Kwangu kule kuna migogoro hasa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Njombe na Halmashauri ya Jimbo la Mlimba. Naomba ule mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa maana ya Jimbo la Lupembe na Jimbo la Mlimba uweze kutatuliwa haraka ili tuendelee kufanya shughuli za kimaendeleo. Kwa sababu ukiwauliza watu wa Njombe wanasema mpaka wao unaenda mpaka kwenye mto, lakini watu wa Mlimba nao wanasema hapana siyo mto ni ndani zaidi ya Njombe. Kwa hiyo, bado ule mgogoro unatuathiri sana katika maendeleo kwa hiyo tunaomba muutatue ili tuweze kujua mpaka halisi upo sehemu gani maana umedumu kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hizi nyumba za National Housing, bei yake ni kubwa mno. Lengo la nyumba za National Housing tukimrejea Mwalimu Nyerere alikuwa na lengo la kuwasaidia watu maskini na wafanyakazi na watu wenye kipato cha chini. Sasa hivi zile nyumba mwananchi wa kawaida au mfanyakazi wa kima cha chini hawezi kununua, nyumba ya vyumba viwili kwa shilingi milioni 70, kwa kweli hawawezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuombe wajaribu kurekebisha baadhi ya taratibu, inawezekana pengine ni Sheria ya Manunuzi ndiyo inayopandisha bei, basi tuirekebishe ili wananchi hata wale wa kipato kidogo waweze kunufaika. Ilivyo sasa hivi hizi nyumba za National Housing na hata zile zinazojengwa na NSSF sehemu kubwa wanaoweza kununua ni watu wenye kipato kikubwa, ni matajiri na wafanyakazi wenye kipato kikubwa ndiyo wanaoweza kumudu kununua nyumba hizi tofauti na lile lengo hasa la msingi la kujenga hizi nyumba kwa ajili ya watu wa kipato cha chini. Otherwise hawa watu wenye kipato cha chini wataendelea kuwa wapangaji na hawataweza kumiliki nyumba zao kwa sababu bei ya nyumba hizi ipo juu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia Idara ya Ardhi kwenye Jimbo langu la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, hatuna Afisa Ardhi Mteule. Kwa hiyo, kunapotokea migogoro ya ardhi tunashindwa kuitatua wakati mwingine inabidi twende kwa wenzetu wa Halmashauri ya Mji waweze kutusaidia kwenye baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, tuombe Halmashauri zote ambazo hazina Maafisa Ardhi Wateule basi waajiriwe ili tuweze kutatua migogoro ya ardhi na mipaka ambayo inajitokeza huko kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme jambo moja juu ya ucheleweshwaji wa hati miliki, inachukua muda mrefu sana kupata hati miliki ya ardhi au ya viwanja. Tunaomba basi kwa kuwa sasa hivi ni ulimwengu au ni wakati wa sayansi na teknolojia, basi ziwe printed haraka ili zisiwe zinachukua muda mrefu sana ili wananchi waweze kunufanika na hili suala la kupata hati miliki kwa maana ya mashamba madogo na makubwa na viwanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu wananchi walishapimiwa ardhi ili kupata hati miliki za mashamba ya chai, lakini imechukua muda mrefu sana na ukiuliza sababu wanasema hatuna Afisa Ardhi Mteule ambaye anaweza akasaini hati hizo. Sasa hivi baada ya kumwona Afisa Ardhi wa Mji ndiye anatusaidia angalau ku-process zile hati miliki ili kuwawezesha wananchi wangu wa Lupembe kupata hati zao kwa ajili ya mashamba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa nafasi hii, naunga tena mkono kwa mara ya pili kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.