Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kutoa mchango wangu katika Hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Wiki mbili zilizopita nilitoa mchango kuhusu mageuzi ya mfumo wa ufundishaji katika vyuo vikuu. Leo nataka nihitimishe hoja yangu kwa kuzungumzia ufundishaji katika shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba, katika shule zetu, hasa za msingi, kuna msongamano mkubwa sana wa wanafunzi katika madarasa. Kwa uzoefu wangu wa ualimu hata kama mwalimu ungekuwa hodari kiasi gani, hakuna mwalimu ambaye anaweza kufundisha darasa lenye zaidi ya wanafunzi 50. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo hili, naomba nipendekeze jambo moja ambalo halina gharama kwa Serikali. Jambo hilo ni kwamba katika shule ambazo kuna msongamano mkubwa wa wanafunzi madarasani, walimu wakuu wa shule wapewe maelekezo maalum ya kuwagawa wanafunzi katika makundi mawili makubwa kama ninavyopendekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kundi la kwanza liwe na wanafunzi wa darasa la kwanza, la pili na la tatu. Hawa waingine madarasani kwa utaratibu wa kawaida kuanzia saa moja mpaka saa nne kamili, wasome masomo kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kundi la pili lenye wa wanafunzi wa darasa la nne, tano na sita, hawa wawekwe kwenye ukumbi mkubwa wa mikutano, huko waoneshwe filamu mbalimbali za kujifunza Kiingereza, Sayansi, wafanye midahalo, majadiliano, drama, michezo ya ndani, mashindano ya usanifu na ubunifu na utengenezaji wa vitu mbalimbali. Itakapofika saa nne na nusu, wabadilishane.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale walioko katika ukumbi wa mikutano, wataingia darasani kama kawaida kuanzia saa nne na nusu mpaka saa saba kamili watakapomaliza masomo na wale waliokuwa madarasani, waendelee na utaratibu wa kufanya shughuli mbalimbali nje ya mitaala, kama nilivyopendekeza hapo awali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nini mantiki ya kupendekeza jambo hili? Elimu yoyote iliyo bora na inayotakiwa kukidhi mahitaji ya mwanafunzi ni lazima ijielekeze kumkuza mwanafunzi katika maeneo matatu ya msingi. La kwanza, uwezo wa akili kufikiri, sisi walimu tunaita cognitive domain. Uwezo wa kukuza maadili mema, tabia njema na mitazamo ambayo tunaita affective domain. Tatu, ni kukuza uwezo wa michezo na kufanya kazi mbalimbali za mikono. Hii ndiyo elimu iliyokamilika, jambo ambalo silioni likifanyika katika shule za sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kasoro nyingine ninayoiona kwenye mfumo wetu wa elimu, watoto wanapomaliza masomo ya siku na kurudi nyumbani, wanapewa kazi nyingi za nyumbani na wazazi wao kutakiwa wawasimamie. Hoja yangu ni, tupunguze kazi nyingi nyumbani. Kama kuna ulazima wa kuwapa wanafunzi kazi, tuwape kazi zenye lengo la kupima uwezo wa ufahamu na udadisi badala ya kukariri majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wazazi wengine wanakwenda mbali zaidi, wanawapeleka watoto wa shule za msingi kwenye masomo ya ziada. Hili ni jambo la hatari sana katika makuzi ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sayansi ya ukuaji wa watoto inasema hivi, ”mtoto chini ya umri wa miaka 15 ubongo wake unakuwa dhaifu sana. Huwezi kumudu kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja. Unataka kutunzwa na kulelewa kwa umakini wa hali ya juu sana.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yuko mwanafalsafa mmoja mwenye busara aliwahi kusema, “kusoma sana, hasa kwa watoto wadogo, kunadumaza akili na uwezo wa kufikiri.” Prof. Howard Gardner wa Chuo Kikuu cha Harvard Marekani katika kitabu chake maarufu “Friends of Mine, Theory of Multiple Intelligences”, aliwahi kusema, malezi na mifumo ya shule inadumaza uwezo wa watoto kufikiri na vipaji vingine vya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, akasema, ”mkazo mkubwa sana wa malezi, wazazi na walimu ni kusoma, kuandika na kuzungumza peke yake.” Vipaji vingine havipewi uzito unaostahiki. Mimi nimekuwa nikijiuliza hivi, kwa nini wazazi wetu ambao walikuwa hawajui kusoma na kuandika na walikuwa masikini wa kutupa, wametulea sisi tukafikia hatua hii tuliyonayo katika mazingira haya?

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi ambao tuna elimu ya kutosha na uwezo mkubwa sana wa kiuchumi hatuwezi kulea watoto kama wazazi wetu. Kwa nini? Kwa sababu mifumo ya malezi, mifumo ya elimu imedumaza haya mambo. Darasani watoto wetu hawapewi nafasi ya kutosha kujifunza stadi za maisha na stadi za kazi. Nyumbani, mkazo mkubwa kama nilivyosema, kusoma, kuandika hakuna kucheza, wanafungiwa mageti. Huwezi kutayarisha vijana imara kama nilivyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malezi ya watoto ni kama vile unavyotunza mimea. Leo ukichukua mimea miwili inayofanana, ya aina moja, mmoja unapanda kwenye ndoo unauweka sebuleni na mwingine unauchukua unaupanda shambani, baada ya miezi sita ukitembelea, ule wa sebuleni utadumaa, ule wa shambani utakuwa imara sana. Kwa nini? Kwa sababu mazingira magumu yanatengeneza vitu imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, mmea ukiwa shambani unajenga uwezo wa kuhimiLi hali ya hewa, mvua, jua, na wadudu waharibifu. Sasa sisi wazazi na walimu wa leo, watoto wetu wanalelewa na televisheni na dada wa kazi muda wote. utatengenezaje vijana makini na imara kwa utaratibu kama huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanafundishwa mambo ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na maisha wanayoyaishi. Wanafundishwa mada nyingi kupita kiasi, mambo ambayo wao wenyewe wangejifunza katika vitabu vyao na kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano hapa. Kwenye somo la Hisabati, walimu wanatumia muda mwingi sana kufundisha kukokotoa namna ya kutafuta square roots na quadratic equation. Sasa najiuliza, ni nini uhusiano kati ya quadratic equation na maisha halisi ya mwanadamu? Wale wa Kemia wanafundishwa periodic table. Ni nini uhusiano wa periodic table na maisha ya kawaida ya mwanadamu? Mimi siuoni. Kwa mawazo yangu, walimu walitakiwa kuwaeleza wanafunzi, nini umuhimu wa periodic equation katika maisha ya kawaida ili waone uhusiano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, watoto wanapoingia kidato cha nne, wanatakiwa kufanya uchaguzi wa kuchagua masomo watakayobobea mbele ya safari. Sasa uchaguzi huu siyo jambo rahisi sana, wanapaswa kuangalia malengo yao, wanapaswa kuangalia vipaji vyao, wanapaswa kuangalia uwezo wao wa kumudu masomo watakayoyachagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mnasaba huu, basi napendekeza, sioni kama kuna umuhimu kwa mwanafunzi ambaye anatamani kufanya kazi ya upishi au ufundi kutakiwa kujiunga na kidato cha tano na sita badala ya kwenda shule ya ufundi. Udongo upate, ulimaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la busara, mtoto anapenda michezo. Badala ya kumpeleka kwenye academy ya michezo anatakiwa kwenda kidato cha tano na sita. Mimi naona kama ni kuwapotezea muda, na kwa bahati mbaya sana vipaji vina muda, muda ukipita vipaji vya mwanadamu vinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijana au wanafunzi ambao wanatamani kusoma masomo ya utaalamu kama vile Udaktari, Sheria, Ufamasia, Sayansi ya Kilimo, na Ualimu. Hawa ni lazima wafuate utaratibu wa kawaida wa kwenda kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa maoni yangu masomo ya kidato cha tano na sita yana uhitaji wa kufanyiwa mapinduzi ya hali ya juu sana. Utaratibu huu wa sasa hautusaidii kuwatengeneza vijana mahiri sana. Kwa maoni yangu, badala ya kuendelea kuwafundisha vijana masomo ya jumla jumla, wafundishwe masuala ya ujuzi na utaalamu ili waweze kuoanisha nadharia waliyojifunza kidato cha nne na hali halisi ya mafunzo ya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazazi wenye asili ya Kiasia, wanatupatia funzo kubwa katika hili jambo. Watoto wao wanapomaliza kidato cha nne wanapelekwa katika vyuo ambavyo vinatoa mafunzo ya utaalamu katika kiwango cha diploma ili wajifunze ujuzi wa kazi. Huko wanajifunza sayansi ya kilimo, utaalamu wa masuala mbalimbali, udaktari, ufamasia ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nahodha, kengele ya pili. Kwanza nikushukuru kwa mchango mzuri sana.

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, ahsante.