Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika hii Wizara muhimu kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, na Ndugu zangu Wabunge, hii Wizara ndiyo roho ya nchi, na ni lazima tuipitishe. Vilevile umuhimu wake ni kwamba inatutoa kwenye dira iliyokwisha inatupeleka kwenye dira ya 2025 – 2050.
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kidogo Jimbo langu. Sisi Musoma Vijijini, tuko mbele kabisa kwenye kutekeleza haya mabadiliko yanayofanywa Wizarani. Kwanza, Mheshimiwa Profesa na timu yake wanafanya kazi nzuri sana. Ukweli ndiyo huo. Nimemsikiliza anayoyasema na mengine, nami ndio nataka kuchangia hapa, tutaongezea tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Musoma Vijijini kwa kusema darasa la mwisho la shule ya msingi, ni darasa la sita na kwamba wote watasoma mpaka kidato cha nne. Sisi tunaendelea kujenga kila kijiji kiwe na sekondari moja, ndivyo tunavyokwenda. Hivi juzi, mwaka huu tumefungua sekondari nne. Salamu zangu ziende Wizarani, lakini sana kwa Mheshimiwa Rais, tunafungua sekondari nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa aendelee kwa sababu vilevile tunamuenzi aliyekuwa Gwiji la Kiswahili Nchini, Profesa David Massamba, tumempatia sekondari yake. Tulianza kujenga kwa fedha kidogo, lakini Wizara na Serikali imetusaidia. Kwa hiyo, Musoma Vijijini tunaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije katika mambo ambayo kidogo yanatoka jimboni na yanashika Taifa zima, ni kuhusu hali ya elimu nchini kwetu. Maana ya hali ya elimu tuna vitu vinne vya msingi hapa, navyo ni suala la ufundishaji, suala la ujifunzaji, uelewa, na ufaulu. Vyote vinne ni lazima viende pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vinne kwenda pamoja sisi tumelisaidia Taifa, Musoma Vijijini, tumefanya mjadala kwa ngazi ya mkoa, halafu mimi mwenyewe nilikaa na ma-head masters wangu wote, na juzi tumefanya kwenye ngazi ya halmashauri, na hiyo ripoti nitawapatia Wizara ya Elimu, TAMISEMI, na Utumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili hii bajeti iende vizuri, namwambia webmaster aiweke kwenye tovuti ya jimbo kuanzia Jumatano, siyo leo. Kwa hiyo, hayo sina sababu ya kuyaongea, mtayapata huko, na yote yanafanana fanana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote aliyoyaongea hapa Mheshimiwa Waziri namwomba sana, sisi Tanzania tumefanya vizuri kwenye nchi zinazoendelea na ndiyo maana tumepata fedha nyingi kutoka World Bank. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri asisahau ile SDG No. 04 (Quality Education for All by The Year 2030) ya Umoja wa Mataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri unakuja. Cha kwanza, ni ujenzi wa shule zetu kwa sasa. Dira yetu ya Maendeleo inaanzia mwaka huu. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na wanaonisikiliza, ikifika Juni mwezi ujao Watanzania tutakuwa milioni 70.55. Eneo letu la ardhi (Tanzania Bara na Visiwani) ukiliweka pamoja ni kilometre square 947,303, kwa hiyo, inamaanisha kwamba population density, yaani watu wanaoishi kwenye kilometre square ni watu 75 kwa mwaka 2025, tukifika mwaka 2050, Watanzania tutakuwa 137. Eneo la nchi yetu litakuwa hilo hilo, population density itakuwa ya watu 155 kwa kilometre square moja. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Elimu, na TAMISEMI, ujenzi wa shule ni lazima ubadilike. Ni lazima twende kwenye kujenga ghorofa sasa, twende juu kwa sababu ardhi haitatosha. Hilo ni pendekezo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni lazima tujue kuwa elimu ni ajira. Sasa hivi duniani kuna upungufu wa wafanyakazi wengi sana. Nikichukua World Health Organisation (Shirika la Afya Duniani), linasema ikifika mwaka 2030 upungufu wa wataalamu wa afya Duniani utakuwa 10,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukua Taifa kubwa kiuchumi duniani, Marekani, leo hii wana upungufu wa watu milioni 3.5 kwenye mambo ya uzalishaji viwandani na mambo ya sayansi na teknolojia. Nikichukua Ujerumani ambayo ndiyo ina uchumi mkubwa kwa nchi za Ulaya, leo hii wanapungukiwa watu 200,000 kila mwaka kwenye maeneo ya engineering, IT, na construction.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wizara ya Elimu ni lazima iweke maanani kwenye mitaala yetu kwamba elimu ni ajira. Nilishaongea hapa, na huwa sipendi kurudia yale yale. Nikasema watu kufanya kazi nje wanaleta fedha, imekuwa ni bidhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, elimu ni uchumi. Uchumi wa dunia wa sasa tukichukua GDP ya nchi zote duniani ni trilioni 116. Mwaka 2050 wakati tunamaliza Dira yetu mpya ya Maendeleo, uchumi wa dunia utakuwa trilioni 228; na kuna aina ya viwanda na biashara ambazo zitakuwa engine ya uchumi wa dunia toka sasa mpaka mwaka 2050.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano hapa, kwanza ni e-commerce (electronic commerce) yaani biashara ya kidigitali. Mwaka 2022 mapato duniani yalikuwa trilioni nne, na mwaka 2040 biashara ya e-commerce mapato duniani yatakuwa trilioni 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili, nimemsikia Mheshimiwa Waziri Profesa anaongea, na aweke mkazo kweli kweli hapa kuhusu Artificial Intelligence. Sasa Artificial Intelligence, software na services, mwaka 2022 mapato yalikuwa bilioni 85 duniani, lakini mwaka 2040 mapato yatakuwa trilioni 4.6. Maana yake ni nini? Ni lazima Tanzania tuwekeze kwenye science, technology, na Mathematics. Sasa Tanzania tufanyaje? Nitatoa mapendekezo yangu, mengine ameyataja, mimi naongezea tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, kama tunataka kwenda hivyo na hizo kazi duniani tuzipate, ni lazima sekondari zote Tanzania ziwe na maabara. Hii aichukue kama ambavyo wanajenga kwa nguvu maeneo mengi wanasahau kujenga maabara. Huu ndiyo msingi wa sayansi, ni lazima ufanye practicals toka form one. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la pili, Sekondari zote nchini ziwe na maktaba zenye kompyuta za kati. Inamaanisha kwamba ndugu zangu siku hizi vitabu vinatolewa bure. Sasa kama vinatolewa bure, ni lazima uweze kunyonya hivyo vitabu kupitia kwenye Kompyuta. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa na maktaba zenye vitabu na kompyuta ili vijana waweze kupata vitabu vya bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la tatu, kwa kuwa tumesema kwamba elimu ya nchini Tanzania itakuwa kidato cha nne. Ni lazima tuanze kuongeza kidato cha tano na cha sita, na tutaongeza kwa uwiano kwamba, kwenye kila Sekondari tano, tuweke High School moja ya Sayansi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mimi wa Musoma Vijijini ambaye sasa hivi nina sekondari 32, ninapaswa kuwa na High Schools sita za Masomo ya Sayansi. Hizi high schools tuachane na zote kukaa Wizara moja, hatutaenda kasi. Ni lazima tuzishushe kwenye halmashauri, ni lazima sasa high schools ziweze kusimamiwa na halmashauri zetu ndipo tutaweza kupata wasomi wengi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika na Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, pendekezo la nne, tujenge technical colleges za aina kama ilivyokuwa Dar Tech. Mnajua, VETA mtu anafanya kitu mechanically, anatengeneza kitu, lakini technical college mtu anauliza hata na sababu kwa nini hiki anakitengeneza? Kwa hiyo, kuna utofauti mkubwa sana. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na technical colleges, na hizi tuzifunge kwenye sheria zisibadilishwe kama ilivyobadilishwa ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la sita, tuwe na wanafunzi wengi. Nimemsikia Profesa anasema, ila tuongeze wanafunzi wengi wanaokwenda kusoma nje, na tunachagua vile vyuo vizuri, siyo kuhesabu tu huko nje, vyuo vizuri. Nadhani Wizarani wanavifahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri hapa, India inafanya maajabu na tunapeleka watoto kusoma India na China na bado wao wanawapeleka kusoma nje. Angalia mwaka 2016 India ilikuwa na wanafunzi 440,000 wanaosoma nchi za nje mwaka 2023. Wamekuwa na wanafunzi zaidi ya milioni 1.4. Kwa hiyo, nasi tupeleke wanafunzi nje. Hawa wa India wanaosoma Ujerumani, 60% wanafanya shahada za engineering na mambo ya Technology...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Profesa kwa mchango mzuri. Kengele ya pili tayari, ushauri wako uandike ili Mheshimiwa Waziri aweze kuupokea na Serikali iweze kupitia.
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, haya, ahsante.