Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, na kama alivyoleta hoja ya kupewa fedha zinazofikia shilingi trilioni 2.4 kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya Wizara hii, kadiri nitakavyochangia naunga mkono hoja, lakini nikisema kwamba kama ingewezekana basi tutakapokuja kwenye mchakato wa mwisho wa bajeti, bado anahitaji fedha kwa sababu ya mambo mapya na mazuri ambayo tumeyakubali na kuyaanzisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtaala unawataka wanafunzi wasome masomo ya amali. Ni hitaji la sasa baada ya nchi kufanya tathmini na kuona kwamba wanafunzi wetu wanamaliza vyuo na shule bila kuwa na ujuzi na kingi wanachokipata ni nadharia.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri ni kwamba mwelekeo huu tunauchukua ukiwa ni mchakato ambao umekuwa ni jumuishi. Watu wengi wametoa maoni na wote tukafikia mahali tukakubali kwamba uelekeo huu ndiyo tunaoutaka kama nchi na kwa jinsi hiyo sitegemei tena kuweze kuwa na kupinduka pinduka hapo mbele kidogo. Tumekubali kwamba ndiyo uelekeo wetu, basi twende na uelekeo huo hata kama kutakuwa na mabadiliko, ni mabadiliko ndani ya uelekeo tuliouchukua kama nchi ili tusije kuwa tunakwenda mbele, tunarudi nyuma kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja yangu ninaijenga kwamba ili tuweze kupata wahitimu ambao tunawakusudia katika uelekeo wetu huu mpya na ndiyo maana nikasema yawezekana tukahitaji bajeti zaidi katika jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza natamani sisi kama nchi tujifunze kwa nchi ambazo zimefanya vizuri zaidi katika mwelekeo huu huko nje ya dunia. Unapopitia katika watu waliofanya vizuri zaidi hutaacha nchi ya Finland, Canada, na China, waliofanya vizuri katika upande wa mtaala huu wa amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukitaka tujifunze kwa waliofanya vizuri, maana ili ufanikiwe learn from the best, huo ndiyo unapaswa kuwa ndiyo uelekeo, yaani huwezi ukataka kuanzisha kitu kizuri halafu usijifunze, just learn from the best. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuanza vizuri bila unyonge, bila udhaifu, hoja yangu na pendekezo langu ni kwamba walimu watakaofundisha mtaala mpya wasiwe walimu ambao hawakufunzwa vizuri. Wakiwa ni walimu ambao wametokana na mtaala wa zamani, lakini ukawa-remodel kidogo tu watapeleka ujuzi wao wa zamani katika mtaala mpya. Kwa hiyo, lazima tuwape mafunzo ya muda mfupi, na ya muda mrefu kwa wale ambao wamefanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ushirikiano wetu, na hizo nchi ambazo tutaziainisha, aina ya mafunzo, na muda wa mafunzo waende wakapikwe vizuri. Wakishaiva, warudi ili cream ya kwanza ya watoto wetu katika mtaala huu wawe wamepikwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tutahitaji kujenga karakana, maabara na studio kwa ajili ya mafunzo hayo. Nimeona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amedokeza jinsi ambavyo karakana hizi, maabara hizi na studio hizi zitajengwa. Sasa hoja yangu hapa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, siku za karibu ni mtakumbuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna video clip ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje ambayo alionesha kwamba tulikuwa na madereva waliomaliza Chuo chetu cha Usafirishaji (NIT), wamefunza vizuri, walipokwenda kupata kazi nje wakakuta teknolojia imebadilika, wakashindwa kuendesha, lakini kwa hapa ni madereva walioiva vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapojenga karakana, maabara, na studio hizi lazima tuzingatie teknolojia ya sasa ili tusije tukakuta kwamba tunaanzisha mtaala wa amali, halafu tukaenda kuwafunza vitu vya kizamani ambavyo kumbe haitoleta tofauti na VETA zilizopo. Kwa hiyo, hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo la kuwa tunajifunza teknolojia za zamani yawezekana pia ndiyo shida inayopatikana katika vyuo vyetu vikuu, kwa sababu tuna maabara za zamani, hatujawa-equip watu wetu kwa teknolojia za kisasa. Kwa hiyo, unakuta kwamba hata sayansi, engineering, ICT, na medicine bado tunakwenda kwa teknolojia za kizamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni eneo ambalo kama Taifa na ukiangalia ICT inakua haraka sana kiasi kwamba muda wetu ambao huwa tunaweka kwamba tutafanya review ya mitaala baada ya miaka mitano upande wa ICT unakuta umebaki nyuma nyuma kabisa. Maana ndani ya miaka mitano hata laptop versions zinakuja aina tatu ndani ya miaka mitano; wewe unatumia ya zamani unajikuta ukiwa nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya ni maeneo ambayo lazima kama Taifa tuwe na alert kwamba teknolojia inabadilika sana, hivyo lazima katika vyuo vyetu tusiendelee na mwendo ule wa zamani tukajikuta kumbe kinachotokea nje ya nchi sisi bado tuko nyuma. Ili hili liwezekane, ni kweli kwamba lazima kila wakati wataalamu wetu waende waka-brush nje ya nchi kuona kwamba kinachobadilika kule, hapa pia kinapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ili tuweze kufanya vizuri bado hatuna muunganiko mzuri baina ya Wizara, Taasisi za Serikali, sekta binafsi na vitu vinavyofunzwa kule vyuoni. Kwa hiyo, unakuta wanafunzi wanasoma hiki, katika sekta binafsi watu wanafanya hiki, halafu hatuwapi muda mzuri wa kwenda kujifunza kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ndani ya nchi hii tumekuwa na miradi mingi ya ujenzi wa SGR, maji, bwawa la umeme, ujenzi wa meli, na ujenzi wa barabara. Sasa jiulize ni wanafunzi wangapi ambao huwa wanapata access ya kuwa interns katika miradi hii mikubwa? Hardly no. Kwa hiyo, tunatamani kwamba kuwe na muunganiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanachokifanya Wizara fulani, basi kiwe reflected katika mafunzo ambayo watoto wetu wanayapata kule vyuoni na wanawezaje kufanya hivyo? Ni kuwaongezea bajeti. Wakati mwingine watoto wanatamani kwenda kufanya internship au kwenda kufanya mafunzo ya vitendo, kinakuja kikwazo kimoja kinaitwa bajeti ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mradi upo, wanafunzi wapo radhi lakini chuo au taasisi husika haiwezi kuwapeleka pale kwa sababu bajeti ni ndogo. Aliyepaswa kukaa wiki nane anaambiwa sasa wewe kulingana na bajeti wanafunzi mmekuwa wengi, utakaa wiki mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi hiyo, tunakuja hatu-impact ujuzi ambao ulikuwa unakusudiwa, na ndiyo maana nikatangulia kusema kwamba yawezekana tukahitaji more budget mahali hapa kwa sababu kama tunataka watu bora, lazima ni wale ambao pia wanapata mafunzo na muda wa intern au practical training wa kutosha kwa bajeti ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tunaipongeza Serikali yetu kwamba imeweza kufanya watu wengi wakapata access na elimu ya juu kwa kutoa mikopo na Bodi ya Mikopo imeendelea kufanya vizuri. Hata hivyo, tunatamani watafiti wa mambo ambao wanatafiti changamoto zilizo katika jamii yetu ya Kitanzania, lakini Serikali haitoi ufadhili kwa Shahada za Uzamili hapa nchini. Kwa hiyo, mara nyingi product ya watu wote unaowaona aliyesoma Masters na Ph.D ni zao la miradi ya wafadhili kutoka nje au alipata scholarship akaenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama wewe una changamoto katika jamii yako ya Kitanzania, lakini hupeleki fedha ili kuwaandaa hawa watafiti ambao ni ngazi ya Masters na Ph.D, sasa unakuta wale wafadhili wanaotaka ku-fund wanapoleta miradi hapa nchini, wana ajenda yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, japo ndiyo watakwambia kwamba unajua lazima tu-align na malengo ya SDG na yale ya kwenu, lakini mara nyingi wana ajenda yao. Sasa sisi kama tuna ajenda yetu kama nchi, kwa nini tusitenge fedha katika maeneo maalumu, tukasema kwamba tunahitaji suluhisho katika eneo fulani na kwa jinsi hiyo tunatamani kwamba tuweze kuwapa wanafunzi wa Masters katika maeneo husika ili hao sasa waweze kufanya mafunzo hayo ya uzamili, baadaye walete suluhisho la changamoto zilizo katika jamii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, matokeo ya tafiti zao yaweze ku-inform policy yaani mara nyingi sera zetu hazitokani na utafiti mkubwa uliyofanywa na watu wetu. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo nadhani pia lazima tukubaliane kama Taifa ili tuweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aliongea Mheshimiwa Prof. Muhongo alipokuwa anachangia kwamba mara nyingi tunapopeleka watu nje ni kwa sababu tu ya opportunity imepatikana katika nchi husika, siyo kwa sababu ya malengo yetu kama Taifa kwamba tunatamani kupata watu gani? Lazima tuwe objective katika eneo hili, kwamba tunatamani watu fulani, utaalamu fulani. Sasa huo tunaanda watu, na tunawasiliana na nchi husika ili tuwapeleke watu katika kufanya utaalamu husika, siyo kwa sababu rafiki yetu India ana opportunity 10 au mko wapi 10 mwende India.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Profesa ni kengele ya pili. Nikupongeze kwa mchango mzuri, mengine mwandikie Mheshimiwa Waziri.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)