Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Esther Edwin Maleko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa. Nianze kwa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Mkenda pamoja na Mheshimiwa Naibu wake Mheshimiwa Kipanga bila kumsahau Katibu Mkuu, Prof. Nombo na wataalamu wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa muda, naomba niende moja kwa moja kwenye zile mada ambazo nilikuwa nimekusudia kuzisemea siku ya leo. Nikianza na bajeti, nilikuwa naishauri sana Serikali kuangalia ni namna gani inaweza kuongeza bajeti ya sekta ya elimu ili iweze kufikia 15% ya Bajeti ya Taifa ya mwaka 2025/2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Wizara hii imebeba majukumu mengi na majukumu ya kimkakati ya kumwondoa na kumkomboa mwananchi au Mtanzania kutoka katika ile hali yake ya kutokuelewa jambo fulani na kumfundisha ili tuweze kuendana na soko la sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa hii ya Bajeti, wakati anasoma Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 16 aligusia suala la kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali, ufundi na ufundi stadi katika shule za sekondari na vyuo vya ufundi. Mimi ninataka kuongeza hapo ushauri wangu, kwamba hili jambo ni jema sana kwa nchi yetu kwa sababu jambo hili linaenda kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi, na pia kuwezesha vijana wetu kuweza kujipatia kipato na zaidi kuweza kushindana katika soko la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kuishauri Serikali ione ni namna gani na njia bora zaidi ya kuweza kuimarisha mafunzo haya hasa kwa kutuambia ni namna gani imejiandaa kwa ajili ya kuwa na vifaa, lakini na wataalamu ili hili lengo letu liweze kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamejiandaa tayari kwa ajili ya kujenga shule hizo za amali, na kuboresha vyuo vile vya VETA. Je, ni namna gani sasa tunaweza kupata vifaa vya kujifunzia tena vifaa vya kisasa na wataalamu ambao wataendana na teknolojia ya sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nilisemee kwa sasa, je, bajeti yetu inaenda vipi kuiangalia na kuwa na mkakati, yaani iwe ni bajeti ya kisekta katika Wizara hizi za kisekta ambazo zinahusiana na elimu? Ni namna gani itakuja na mpango madhubuti wa kuweza kuajiri walimu wa kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, shule zimejengwa, zipo za kutosha tunamshukuru Mungu, lakini ni namna gani ya kuweza kupata walimu au kuajiri walimu wa kutosha? Kwa sasa wanaajiriwa kwa mwaka walimu 10,000 mpaka 15,000. Tukienda kwa mtiririko huu tutamaliza zaidi ya miaka 15 tukiwa bado hatujaweza kuikamilisha changamoto hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba Serikali ione ni namna gani wataweza kujitahidi ajira zitolewe kwa mwaka 40,000 mpaka 45,000 ili tuweze kuondoa tatizo hili katika kipindi cha miaka mitano au miaka sita ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kushauri kwa wakati huu ni kuhusu uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. Tunaishukuru sana Serikali imeweza kupigania jambo hilo, lakini sisi tunaomba kushauri kama Kamati, Serikali ione namna gani basi itatenga bajeti ya kutosha pamoja na kusambaza vitabu hivi kwa wakati, kwa sababu jambo la kutenga bajeti ni lingine lakini kuhakikisha vitabu vinawafikia wanafunzi kwa wakati ni jambo lingine, na ni bora zaidi. Nilikuwa naishauri Serikali ione ni namna gani vitabu vitawafikia wanafunzi kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia iendelee kuangalia ni namna gani itaendelea kuchapisha vitabu kwa wakati, lakini kulingana na mahitaji, na wakati huo huo tuendelee kuangalia ni namna gani tutaenda kuwa na vitabu au kufundisha kidigiti ili kupunguza namna ile ya kwenda kuchapisha kitabu kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kusisitiza kwa mchango wangu wa leo ni namna Wizara hii itaweza kuangalia ni namna gani tunaweza kuifanya lugha ya alama kuwa ni somo la lazima shuleni na katika vyuo kwa kila mwanafunzi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Kenya na South Africa na baadhi ya shule wameanza kufanya jambo hili. Jambo hili linasaidia kuweza kuwasiliana na ndugu zetu hawa kwa sababu unakuta wakati mwingine inakuwa ni vigumu sana kwa sababu tunasema ni elimu jumuishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa inapokuwa ni elimu jumuishi, na hawawezi kuwasiliana na watu hawa inakuwa ni shida. Kwa hiyo, inapendekezwa kwamba Lugha ya Alama ifanywe kwamba kuwa somo la lazima shuleni ili watu wengi zaidi wawe wanajua namna gani ya kuwasiliana na ndugu zetu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nilitaka kuishauri Serikali kwa siku ya leo ni namna gani ya kuongeza ruzuku ili kuweza kuwapatia mabinti wa kike taulo za kike, kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa sana ambayo inawafanya mabinti wengi mpaka sasa kushindwa kwenda shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie ni namna gani inaweza kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia mabinti zetu hawa kupata taulo za kike? Pamoja na hayo, kuna vituo ambavyo ni vya kuimarisha utambuzi na upimaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashauri hivi vituo viwekwe kwenye kila halmashauri ili kuweza kusaidia walimu kutambua wale wanafunzi wenye matatizo kwa sababu kuna wakati mwingine wanafunzi wana matatizo ya kusikia, lakini hawajafanyiwa upimaji na utambuzi mapema, kwa hiyo, inakuwa ni changamoto kwa mwalimu kuweza kumfundisha kwa namna na yeye alivyo. Kwa hiyo, inakuwa inawawia vigumu wanafunzi hawa kuweza kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kufikia hapo nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)