Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya kwenye Wizara hii ya Elimu pamoja na wasaidizi wake akiwemo Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu Prof. Nombo. Nampongeza sana na tunaendelea kumwombea katika kazi anazofanya za kuhakikisha elimu katika Taifa letu inaendelea kuwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kuwapongeza watumishi wa Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa ambazo wanafanya tukiamini kabisa kwamba elimu itaendelea kuimarika kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maeneo mawili ambayo nataka nichangie jioni hii. Eneo la kwanza, naendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuja na hoja kubwa kuanzia mwaka 2023 ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi ambavyo vinaendelea kujengwa katika wilaya zetu. Nakiri hata Busega tayari tumepata chuo hiki ambacho sasa kinaendelea kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, na Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambayo inaendelea kwenye majimbo yetu. Walianza na vyuo 29 na hapa katikati walikuwa na vyuo 64 plus one kwa maana ya 64 katika wilaya zetu na kimoja katika Mkoa wa Songwe kule kwa Mheshimiwa Hasunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili pamoja na kuwa ujenzi unaendelea, lakini hapa katikati ulikuwa unasuasua. Mwaka 2022/2023 tulipitisha hapa bajeti ya kupelekewa shilingi bilioni 100 katika Wizara yetu ya Elimu, lakini mpaka tunapozungumza hapa, zimeshapelekwa shilingi bilioni 74.6, bado shilingi bilioni 25.4 ambazo hazijapelekwa kwenye Wizara yetu ya Elimu ili kufanya utekelezaji wa ujenzi wa VETA hizi kwa awamu ile ya kwanza kwa maana ya majengo tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Fedha, bahati mbaya siwaoni hapa, lakini naomba sana Serikali kuchukulia maanani kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapelekwa kwa watu wetu hawa wa Wizara ya Elimu ili ujenzi wa VETA sasa uendelee kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, objectives za ujenzi wa VETA hizi ni nzuri sana, kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata mafunzo ili waweze kujiajiri na waweze pia kuajiriwa. Wanafunzi mbalimbali ambao wanatamani kwenda kwenye hivi vyuo ni wengi ambao bado hawajapata nafasi ya kwenda kwenye vyuo kwa sababu ya uchache wa vyuo vilivyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni muda mwafaka sasa Wizara ya Fedha ihakikishe kwamba inapeleka fedha hizi shilingi bilioni 25.4 zilizobaki ili Wizara ya Elimu iweze kukamilisha hatua ya kwanza ya majengo tisa ili yaweze kukamilika katika maeneo yetu. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Fedha ipeleke fedha hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, nimeona amesema kwenye hii bajeti kwamba kuna mwendelezo wa awamu ya pili ya majengo mengine nane kama sikosei. Niendelee kuiomba Serikali na niendelee kuiomba Wizara ya Fedha, watakapopitisha bajeti hii, basi wapelekewe. Nia yetu ni kuona watoto wanapata sehemu ya kwenda kusoma ili wapate ajira na waweze kujiajiri, hao ambao tutakuwa tumewapangia kwenye vyuo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru chuo kikikamilika kwa wakati ili wananchi wa Jimbo la Busega waweze kukitumia chuo hiki ambacho Mama Samia amewapa kwa ajili ya huko baadaye waweze kupata sehemu ya kupata elimu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Wizara ya Fedha ipeleke fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, hapo hapo kwenye eneo la VETA, sijajua ni namna gani Mheshimiwa Waziri amejipanga kupata wataalam, kwa sababu tunaamini vyuo hivi 64 vitakamilka, lakini vinaweza vikakamilika na vikakosa wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo lingine la pili ni kwa namna gani wanaenda kuandaa wataalam ili waje wahudumie vyuo vyetu kuhakikisha kwamba wanaenda kuwafundisha hawa Watoto? Ni eneo mojawapo ambalo pia lazima tulichukulie maanani ili tunapoenda, tuhakikishe vyuo hivi vimekamilika kwa maana ya majengo, basi na wataalam wawe tayari ili waweze kwenda kuwafundisha watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona tusiishie hapo. Kwenye eneo la vifaa, pia sasa hivi tunaweza kuwa tunasema majengo, kumbe mpango wa ununuzi wa vifaa ukachelewa. Ni vizuri zaidi mpango huu na wenyewe ukaendana kama tunavyoenda kujenga majengo, na pia twende kwenye hatua ya pili ya ununuzi wa vifaa ili majengo yanapokamilika na vifaa viwe tayari ili watoto wetu waweze kupata sehemu ya kusoma, na majengo haya yasiendelee kuwa majengo tu, bali yapate vifaa ambavyo vinahitajika katika maeneo yetu ya VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo lingine la pili ambalo Mheshimiwa Waziri amelizungumzia kwenye bajeti yake, naomba Wizara ya Fedha iweke kipaumbele kwa sababu majengo yameshaanza, na vyuo hivi vimeshaanza kupata majengo, sasa yatakapokamilika, ni vizuri yapate vifaa, walimu wapatikane, ili tuweze kuhudumia vizuri majengo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni la mtaala mpya. Tumeona mwaka 2024 tumepitisha mtaala mpya ambao sasa elimu ya msingi itaishia darasa la sita, na ninafikiri itakuwa mwaka 2027 kama sikosei, lakini mwaka huo kutakuwa na darasa la sita na hapo hapo kutakuwa na darasa la saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu, sijaona mpango ni kwa namna gani madarasa haya mawili yote watakwenda kuya-accommodate mwaka 2028. Mpango huu unatakiwa uanze sasa. Tunavyozungumza nilitamani kuona kuna mpango wa namna gani madarasa mawili haya kwa mwaka mmoja 2028 yatakapokuwa yanaingia form one tuwe tayari na miundombinu ya kuwatosheleza watoto watakaoingia kupitia haya madarasa mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni eneo mojawapo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up kesho, natamani kumsikia akizungumzia ni kwa namna gani wamejiandaa kuhakikisha kwamba tunapofika mwaka 2028 haya madarasa yote mawili yatakuwa accommodated kuhakikisha kwamba miundombinu ipo, na ni salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye eneo hili la kubadilika kwa mtaala, nimeona tutakapoingia huku sekondari kwa maana ya kidato cha kwanza, wanafunzi watakuwa na option mbili, mwingine ataenda kusoma masomo haya ya kawaida kwa maana ya Physics, Chemistry na mambo mengine, lakini kuna wengine ambao wataenda kwenye vocational training skills pale pale kwenye shule zetu za sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ni zuri, tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maana ya Katibu Mkuu kwa kazi kubwa waliyofanya ya mtaala. Wasiwasi wangu kwa hao watoto ambao watakwenda kusoma skills za vocational training kwenye sekondari, sijaona mpango ambao amekuja nao wa kitu kinaitwa maabara, wanaita wataalam training factory. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo training factory itawasaidia watoto kama ambavyo tumekuwa tukiwasaidia watoto wanaosoma Physics wanapata darasa lao la practical, wanaosoma Chemistry wanapata darasa lao la practical na wanaosoma Biology wanapata darasa la practical.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatamani sasa watoto wetu ambao wataenda kwenye skills za vocation kwenye sekondari zetu, pia tuwe na darasa lao la practical. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba tunapeleka vifaa kwa ajili ya training factory na vifaa hivi, basi vinaweza kugawanywa katika shule zetu za kata na ikionekana bado tunasuasua, basi tuanze hata kwenye shule mojawapo kwenye tarafa ili tuweze kuwasaidia watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kwenye eneo hili la training factory ni lazima tuangalie, kulingana na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwenye eneo husika, tuhakikishe kwamba tunaenda kwenye eneo la kilimo, kwa maana ya Simiyu, sasa tunazungumzia pamba, ni training factory zipi ambazo zitaendana na uzalishaji wa pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda huko kwenye chai, tukienda huko kwenye kahawa, twende huko kwenye nini, tuhakikishe kwamba watoto hawa wanapokuwa wanajifunza, wakati hawa watu wa Physics wanaenda kwenye practical, hata hawa watu wa skills za vocation, waende kwenye practical yao ili anapomaliza form four awe na kitu ambacho anaweza kwenda kufanya kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii sasa ndiyo itakuwa tija kwa mtaala mpya ambao tumeutengeneza na ndiyo itakuwa tija kwa namna gani tumewekeza kwa hao watoto ili tuone mabadiliko chanya kwa Watanzania wetu na watoto wetu katika hali nzima ya ufaulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimesikia kengele, naunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)