Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie hoja iliyopo Mezani kwetu. Niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Prof. Mkenda; Naibu Waziri; Katibu Mkuu, Prof. Nombo; Naibu Makatibu Wakuu; Kamishina wa Elimu; na Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi mbalimbali zilizopo kwenye Wizara hii ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye sekta hii ya elimu. Tumeona bilioni nyingi za fedha zinakwenda katika programu zetu hizi zilizopo katika level ya shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ule mradi wa BOOST kuna bilioni za fedha zinakwenda kule. Tuna mradi wa SEQUIP kwa elimu ya sekondari, lakini kwa elimu ya juu tuna mradi wa HEET. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji huo mkubwa ambao anaufanya kwenye sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha Waziri kimejaa takwimu, tena zenye matumaini makubwa sana kwa nchi yetu. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. Mchana huu nimepitia kitabu hiki mara mbili, nikaona kwamba yale yaliyomo yakipata fedha kutoka Wizara ya Fedha, basi tutakuwa tumeingia kwenye hatua nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu Wizara ya Fedha kama walivyosema wenzangu, tutoe fedha ambazo zimeombwa na Mheshimiwa Waziri ili wakatekeleze yale ambayo yamepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna matumaini mengi kwenye taarifa hii, nimekuja na mengi ya kupongeza na kushauri. Kwanza, kwa miaka mitatu hivi tulikuwa tunazungumzia Chuo Kikuu; University College ya Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema kwamba wakati wa miaka 2000 tunapotekeleza mipango mikubwa ya elimu, ule Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MEM) na ule Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MES), kulikuwa na andiko lilitolewa pale kwamba ili kukabiliana na changamoto ya walimu wa sayansi, vyuo vitatu vibadilishwe, badala ya kupewa mafunzo ya ngazi ya kati, basi iwe sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ualimu Dar es Salaam, Chuo cha Ualimu Mkwawa na Chuo cha Ualimu Mtwara.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitekeleza vyuo viwili, DUCE ilianza pale Dar es Salaam tukaona Mkwawa nayo ilibadilishwa, lakini Mtwara ikawa kimya. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba ile document ambayo kwa miaka 20 haikutekelezwa, sasa anaitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa, sasa Chuo cha Ufundi Mtwara na Chuo cha Ualimu Mtwara vitabadilishwa sasa na kuwa University College ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya. Tunamshukuru sana kwa usikivu, tunaishukuru timu ya wataalam, Prof. Nombo na timu yake kwa kusikiliza kile ambacho tumekuwa tunakisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yetu sasa kwa sababu vyuo hivi viwili majengo yake yamechakaa, havina majengo ya kutosha, na tumeona kwenye bajeti wamesema wametenga fedha kwa ajili ya kuongeza majengo na vifaa kwa vyuo hivi ili sasa viwe kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na specifically kwa ajili ya kuandaa walimu kwa ajili ya ule Mkondo wa Amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna kitu kinaitwa skill over effect. Kila palipo na chuo kikuu lazima majirani zake waathirike. Kwa hiyo, nina ushauri kwamba, Profesa na timu yake watengeneze programu za muda mfupi hasa za kutoa ujuzi na maarifa kwa vijana na wakazi wa maeneo yale ili nao wapate ufundi ambao utatolewa wakati wanatayarisha wale walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, ni matarajio yetu sasa shule ambazo zipo katika maeneo hayo zinufaike kama sehemu ya training, kwamba kwenye block teaching, shule za jirani za amali zinafaidika na kile kitakachopikwa kwenye vyuo hivi viwili vya Mtwara kawaida na Mtwara Ufundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakushukuru kwa kusikiliza kilio chetu na ninamtakia kila la heri katika utekelezaji na nimwahidi Wabunge wa Mtwara tutampa support katika utekelezaji wa kufanya mabadiliko hayo makubwa ya kubadilisha vyuo hivyo viwili kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia kule Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili, kama walivyosema wenzangu, tumeshaanza kutekeleza mtaala mpya kwa maana ya utekelezaji wa Sera yetu ya Elimu ya Mwaka 2014, lile Toleo la 2023 tunafanya mambo mengi katika utekelezaji wa mtaala huu ikiwemo ongezeko la miumdombinu na mambo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapoanza utekelezaji wa mtaala huu, vilevile tujikite au tujitayarishe na namna ya upimaji wa mtaala huu. Upimaji ni sehemu muhimu sana, kwa sababu mtaala wetu ni competence based, hatutarajii upimaji wetu uwe kama tulivyofanya kwenye mtaala uliopita. Kwa hiyo, naomba tufanye matayarisho, na upimaji siyo suala la bahati mbaya ni suala ambalo linahitaji matayarisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, walimu katika ngazi zote watayarishwe namna ya kuwapima wanafunzi wao, walimu wa awali, walimu wa shule za msingi na walimu wa sekondari, lazima watayarishwe namna ya kutayarisha yale maswali kwa sababu tunatarajia upimaji wetu ujikite kwenye ujuzi na ufundi na siyo kumbukumbu ya kile alichojifundisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mitihani yetu mingi sasa hivi ukiipitia inamtayarisha mtoto kukariri ili kesho akayamwage kwenye chumba cha mtihani. Hatutarajii kwamba upimaji tutakaokwenda nao uwe wa namna hiyo. Ni lazima Baraza la Mitihani lifanye review ya utayarishaji wa mitihani yake ili tupate mitihani ambayo kweli ina lengo la kupima kile ambacho tunakikusudia, lakini tukifanya mitihani kama mazoea, kwa kweli hatutapata kile ambacho tunakitarajia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hata muda wa upimaji hatutarajii unapotaka kupima ujuzi na ufundi aliyoupata mtahiniwa ukatumia dakika 40 kwenye chumba cha mtihani. Haiwezekani unapotaka kupima ujuzi na ufundi, ukatumia masaa mawili ukapima mwanafunzi. Kwa hiyo, ni lazima tufanye review tuangalie sasa tutawapima vipi wanafunzi wetu au wahitimu wetu katika ngazi mbalimbali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya tatu ni in service training, yaani mafunzo kazini kwa walimu wetu. Hiki ni kitu muhimu sana. Mafunzo kazini yana faida kubwa sana. Nitataja faida tano tu. Faida ya kwanza ni kukuza utendaji. Unapompa mafunzo mapya, basi unaimarisha utendaji wa yule mtumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, mtumishi anapata maarifa mapya, mwalimu anaongezewa maarifa, lakini unakuza uhusiano wa kupata marafiki wapya wakati wa training. Vilevile, unaongeza ufahamu wa kile unachokifahamu. Pia cha tano, hakuna in service training ambayo inakwenda bure, inaongeza kipato kwa mtumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri, nimeona hapo figure ambazo amezitoa katika kila ngazi. Kwa kuwa walimu ni jeshi kubwa na sehemu kubwa ya watumishi wa umma ni walimu, basi lazima tutafute fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo kazini ya walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuwekeze mafunzo kazini kwa walimu. Walimu lazima wapate taarifa na maarifa mapya. Tusipofanya hivyo tutakuwa na walimu ambao sio wa kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)