Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hii Hotuba ya Waziri wa Elimu. Naendelea sana kuishukuru Serikali yangu kwa namna ambavyo imejitahidi sana kufanya mambo makubwa na mazuri hasa katika huu upande wa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka michache tu iliyopita tulikuwa na changamoto kubwa kwenye shule za sekondari, tulikuwa na changamoto kubwa kwamba wanafunzi wengi walikuwa wanafaulu lakini hakukuwa na vyuo. Pia kulikuwa na changamoto kubwa hata katika mikopo. Sasa ukiangalia katika hiki kipindi mambo mengi sana yameboreshwa na vijana wetu wengi sasa wanasoma vizuri zaidi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tunakoenda sasa walau hata yale matumaini makubwa yanaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wangu sasa, baada ya kuwa wanafunzi wengi wanaweza kusoma mpaka wakamaliza vyuo vikuu, changamoto kubwa ambayo iliyopo ni ya ajira. Leo ukiangalia watoto wengi wanamaliza vyuo, akishamaliza mzazi unakuja tena kupata mzigo mkubwa wa kumpatia ajira kwa sababu hizo ajira zenyewe hazipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, leo kibaya zaidi unakuta kwamba nafasi za ajira zinatoka, lakini wale wahitaji ni zaidi ya 5,000 au 10,000 lakini nafasi zenyewe ni nafasi 500 au1000. Kwa hiyo, hapo napo sasa imekuja kupatikana changamoto nyingine kubwa ambayo tunadhani na yenyewe itaendelea kutusumbua kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu sisi Wabunge kazi yetu ni kushauri, basi nashauri katika baadhi ya maeneo katika hiki kipindi tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia vijana wetu hasa wale wanaomaliza vyuo, na baada ya hapo sasa wanakaa nyumbani wakiwa wanahangaika kila siku na bahasha kwa ajili ya kutafuta kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa elimu, kwa bahati nzuri kwa Tanzania kama nchi sisi ndiyo waasisi wakubwa wa lugha ya Kiswahili, na lugha ya Kiswahili ni kati ya lugha ambayo sasa inakua kwa kasi na nchi nyingi zinaitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, leo katika utafiti tu mdogo wa haraka haraka hata kwa wenzetu wa nchi jirani, wao ndio wanaweza kutumia fursa hiyo ya kutoa walimu wengi kwenda kwenye nchi za wenzetu kwa ajili ya kufundisha Kiswahili. Leo unaposema unataka labda nchi nyingine ziweze kujifunza Kiswahili, wanahitaji tu vitu vichache sana. Watu wengi wanahitaji ajue kusoma na kuandika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia suala la kusoma na kuandika ni suala ambalo halihitaji Mwalimu aliyesomea Kiswahili per-se na kwa sababu halihitaji Mwalimu aliyesomea Kiswahili per-se kumbe sasa walimu wetu wote wale ambao ni ma-graduate katika masomo mbalimbali yawe ya Kiingereza, Historia na masomo yote hayo, bado anaweza kufundisha somo la Kiswahili ilimradi yeye alisomea Ualimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, leo tukiamua, ninaamini kwamba tunaweza tukapeleka watu wengi zaidi duniani, na vijana wengi zaidi tena kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda kwenye nchi yoyote ile, nenda hata Ufaransa; kwa bahati nzuri sisi kama Tanzania tunazo Balozi mbalimbali katika nchi mbalimbali. Sasa leo tukiamua tu kwamba kila nchi ambayo tuna Ubalozi nayo, ambao wanahitaji kujifunza Kiswahili, tunaweza tukawaambia zile Balozi zetu watenge tu pale vyumba vichache, halafu tukawa na walimu pale na hao walimu tukajaribu kutangaza, watu wakafahamu kwamba tunafundisha Kiswahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaamini kwamba kwanza watu wengi watapenda kujifunza Kiswahili kwa sababu watakuwa wanajifunza tu katika muda labda wa saa mbili kwa siku na kwa sababu ni Kiswahili cha kusoma na kuandika ambacho ndicho watu wengi wanakipenda, basi kwa hiyo, itatupatia nafasi kubwa sana ya sisi kupata wanafunzi wengi katika hivyo vyuo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, kwanza tutapata mapato kama nchi. Pili, ni kwa sababu sasa vijana wetu wengi wako huko duniani na wanafundisha Kiswahili, tafsiri yake ni kwamba watakuwa wamejipatia ajira. Kwa hiyo, tunadhani kwamba hilo nalo ni mojawapo ya eneo ambalo tukilitumia vizuri tunaweza vijana wetu wengi ambao wanakaa bila kazi wakaweza kupata ajira na maisha yao yakaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, eneo lingine tunadhani sasa ni wakati muafaka ambapo tungeshusha nguvu zaidi kwenye hivi vyuo vya kawaida ambavyo ndivyo vina watumishi wengi. Yaani leo ukiwa na watoto wawili, mmoja amemaliza chuo kikuu amesoma sociology, mwingine amemaliza tu kidato cha nne akaenda VETA, yule wa VETA bado kwako au yeye mwenyewe anaweza kuendesha maisha zaidi kuliko yule wa chuo kikuu, kwa sababu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, yule wa chuo kikuu maana yake ni kwamba mpaka apate ajira ile aliyoisomea ndipo maisha yaweze kuendelea, lakini kile tu kitendo cha kujiona amesoma amefika chuo kikuu maana yake kila mara anaanza kufikiria namna ya kupata ajira. Kwa hiyo, tunadhani leo tukiendelea kuimarisha vyuo kama hivi vya VETA pamoja na hivi vyuo vidogo vidogo vya ufundi vinaweza vikasababisha watu wetu wengi zaidi wakapata ajira. Vyuo vya kilimo, Vyuo vya mifugo vitasaidia kuliko hali hii tuliyonayo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda tu kwa wenzetu hapo Kenya wana vile vyuo vya ujasiriamali, huu ufundi mwingi mwingi wanafanya na kwa kweli unakuta wanakutengenezea vitu vingi na vizuri, lakini wanaita Juakali. Sasa Juakali kama hizo ukiangalia kwa majirani zetu, vimewapatia ajira kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumbe hata kwenye nchi yetu kama hii Tanzania tukiendelea kuzisaidia akina SIDO zetu, tukasaidia na hivyo vyuo vingine, kwa hiyo tafsiri yake ni kwamba vijana wengi zaidi wataweza kujiajiri na maisha yao yakaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali tuliyonayo sasa hivi ni kwamba tuna kundi kubwa la vijana wana elimu nzuri wame-graduate lakini kila siku wanatembea na bahasha wanatafuta kazi. Kutokana na hali hiyo, maana yake ni kwamba vijana wetu wanaendelea kusota badala ya kuwasaidia katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)