Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nami moja kwa moja naipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa ambayo imefanyika. Pia, napongeza kwa Sera ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 ambalo tunaendelea nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imeendelea kuwa na sera mbalimbali za elimu tangu tulipopata uhuru na lengo la kubadilisha sera zile kila wakati ilikuwa ni kuendana na wakati na mabadiliko ya wakati huo, lakini pia kupata tija kutoka kwenye elimu kutokana na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1962 tulikuwa na Sera ya Elimu ambayo lengo lake kubwa ilikuwa ni kuangalia baada ya kupata uhuru, kuna nafasi nyingi ambazo zilikuwa zimeachwa wazi. Kwa hiyo, ilitakiwa kuandaa Watanzania haraka ili kuweza ku-feed nafasi hizo. Hilo lilifanyika kwa kuanzisha program mbalimbali ikiwepo kuanzisha madarasa kufika mpaka nane, lakini baadaye kuongeza masaa ya kujifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda kwa 1967 tukaona kwamba elimu tuliyokuwanayo bado ilikuwa ina misingi ya kikoloni. Kama tunavyojua, elimu ya kikoloni ilikuwa ni kwa ajili ya kupata maslahi ya kikoloni. Wao walianzisha elimu kutokana na wao walivyokuwa wanataka kwa kuzingatia maslahi yao, na sisi tukataka tuzingatie maslahi ya Taifa letu. Tukaanzisha elimu iliyoendana na Sera yetu ya Ujamaa na Kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, zimekuja sera nyingi na program nyingi za elimu na mwisho tumekuja na hii sera ambayo tukonayo sasa hivi ya 2014 ambayo hii nayo ilionekana ina upungufu kutokana na kutokuwa na walimu wa kutosha, mazingira ya ufundishaji na kujifunzia kutokuwa bora, na pia kutokuwa na udhibiti wa ubora katika elimu yetu na kuwa na elimu ambayo haiendani na soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetengeneza sera nyingine ambayo kwanza tunaipongeza Serikali kwa sababu katika mazingira ya kujifunza na ujifunzaji kuna mambo makubwa yamefanyika kuhakikisha kwamba tunapata shule za kutosha na pia tunapata miundombinu mingine ya shule za kutosha, kuhakikisha kwamba tunaleta motivation kwa watumishi kwa kuajiri walimu wa kutosha na kuboresha maslahi ya walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba wana malalamiko makubwa ya mishahara, kupandishwa madaraja na stahiki za wafanya kazi. Haya yote Serikali imeyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nilitaka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Elimu maana yake ni mchakato unaohusisha mtu kupata ujuzi na maarifa, maadili na mtazamo. Sasa kwenye Taifa letu tume-concentrate sana kwenye ujuzi na maarifa, hatuangalii maadili na mtazamo (attitude za watu) na hii ndiyo inayotupa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa Mbunge aliyetoka, hii inatupa shida, mtu kufikiri kwamba akipata elimu lazima aajiriwe au akipata elimu lazima apate kazi. Sasa hii iko kwenye package ya Mheshimiwa Waziri na kwenye hii Sera ya 2014 Toleo la 2023 wewe kama Wizara ndiyo msimamizi wa uendeshaji wa elimu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunatamani tuone Wizara inasema nini katika suala linalohusu maadili na linalohusu mtazamo. Tunawajengeaje watoto wetu mtazamo chanya kwamba elimu ni nini? Tunawajengeaje watoto wetu maadili chanya hata wakipata kazi waweze kuwa na tija kama ambavyo sera yenyewe inasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto kwenye mifumo yetu ya elimu. Kwanza katika usimamizi, lazima tukubaliane kwamba elimu kama mchakato wa kupata ujuzi, maarifa, maadili na mtazamo unahusisha mfumo wa shule ulio rasmi ambao Waziri anausimamia lakini na mfumo usio rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea watoto hawa wapate maadili kutoka kwenye vyombo na taasisi nyingine pia, lakini leo hii, mfumo wa elimu umechukua muda mrefu kwa mtoto wetu. Watoto hawana muda, na vipindi vingine hatuwaachii, hatuna zile taratibu nzuri za kuwaachia ili kuruhusu taasisi nyingine zipate muda wa kupandikiza kitu kwa hawa watoto wetu ikiwemo taasisi za kidini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii watoto wakiwa likizo wanakwenda tuition, wakiwa shuleni Jumamosi na Jumapili wanakwenda tuition. Makanisa hayapati muda wa kuwafundisha hawa watoto imani zilizo sahihi; misikiti haipati muda wa kuwafundisha hawa wototo imani zilizo sahihi, as a result tunapata wasomi ambao wanafikiria ili akae kwenye cheo, lazima aroge; ili akae sijui kwenye nafasi ya biashara, lazima afanye mambo ya kikatili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima sasa Wizara ya Elimu ituletee ratiba na ituambie; Mheshimiwa Nahodha alisema kwamba mtoto naye akifundishwa sana inaonekana pia hawezi kuelewa, hivyo unamletea problem ya afya ya akili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati lazima tukubaliane, watoto wanatakiwa sasa wakajifunze masomo ya darasani na wakati huu tuwaachie wafanye masomo mengine ili kuwajengea mtazamo na maadili. Mheshimiwa Waziri wa Elimu ni lazima tukubaliane, kuna informal education tuliyokuwa tunapata iliyokuwa nzuri. Tulipata kwenye unyago wakati huo, leo hii katika mfumo wa elimu ambao tunakaa nao muda wote...

MHE. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: ...watoto wetu wanapata wapi mafunzo yale ya kujitambua kama mama? Kujitambua kama baba na kujua wajibu wao?

MHE. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana msemaji anayezungumza sasa hivi, na hasa anaposema kwamba, tuangalie elimu inayotoka kwenye maeneo mengine. Kama dini zifundishwe, lakini nimtahadharishe kwamba, siyo dini zote zinatoa maarifa yanayofaa kwa watoto. Kwa mfano, kuna mtu anasema kabisa, anakwenda pale Kanisani au sehemu ya dini anasema yeye ni Mungu. Sasa dini hizi pia, tuangalie ni dini gani zinafaa kwa watoto wetu? Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca, taarifa hiyo.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipokea taarifa yake. Kama ilivyo kwamba, tunaposema imani, tunajua zipo imani potofu na siyo imani za kidini tu, hata hizo imani nyingine za kienyeji, zipo nyingine ambazo pia ni potofu. Kwa hiyo, naamini kabisa kwa namna Profesa alivyo makini, tunafahamu ni imani ipi tunayoiongelea kwa watoto wetu ili wajitambue, wajue na wawe na maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, hawa watoto tunataka wa-acquire ujuzi na maarifa. Sehemu kubwa ambayo inatumika, kiungo kinachotumika kwao katika kupata ujuzi na maarifa ni kichwa, na afya ya akili. Kwenye shule zetu watoto hawa wanapataje skills au wanafundishwaje kuwa na afya ya akili?

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunajua kabisa kwamba, kuwa na afya ya akili, kwanza mtu yeyote mwenye afya ya akili, ndiye mwenye uwezo wa kuzalisha vizuri, kupambana na changamoto, kusaidia jamii yake na kujitambua. Sasa, haya ni mambo ya muhimu kwa watoto wetu kuanzia ngazi ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona kabisa katika masuala ya ukatili wa kijinsia mambo mengi yamegundulika shuleni. Watoto wetu wanakwenda shuleni wana stress nyingi sana kutoka kwenye familia. Kule shuleni wakifika kuna chombo gani kinakaa kuwaangalia wale watoto?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna watoto wengine wanazaliwa na ulemavu. Kutokana na taasisi zetu zilizopo, wengine wanashindwa kuwatambua toka huku chini. Anapofika shule, tuna kitu gani pale shuleni ambacho anaweza akaenda akatambuliwa? Mimi ninafikiri ni wakati sasa umefika...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba robo dakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri wakati umefika, tuanzishe clubs za mental health shuleni, ili watoto wetu wapate kuwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu hii inatakiwa itolewe kwa usawa. Tumejenga shule za bweni za watoto wa kike, tunataka tujenge shule za bweni za watoto wa kiume. Wakati ule wa Sera ya Elimu tulikuwa tunajenga shule mbili mbili; ya kike na ya kiume.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulikuwa tuna Iringa Girls na tulikuwa na...