Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kunipa fursa hii ya kupumua na kuweza kuendeleza majukumu yangu ya Kibunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naishukuru familia yangu kwa kuendelea kunivumilia nikitoa huduma hii kwa wananchi wangu. Halikadhalika, nawashukuru wananchi wangu kwa kuniunga mkono wakifahamu kabisa kuwa, napambana kwa ajili yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia mambo mawili. Kwa kuanzia, kama walivyofanya wenzangu, naanza kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada zake kubwa sana katika eneo la elimu. Kipekee pia, nampongeza Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Prof. Mkenda, kwa kweli amefanya kazi kubwa ya ku-transform elimu kutoka tulikokuwa mpaka sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna mtu anaweza kupinga kwenye hili kwamba, sasa hivi tuko katika mazingira ya mapinduzi makubwa kabisa ya elimu, lakini pamoja na pongezi hizi zote na kazi kubwa iliyofanyika, bado tunayo ya kusemea, kwa maana ya mambo ambayo tunatamani yafanyike, ili mapinduzi haya yaende kwa umakini kabisa, na yawe very successful.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira yetu yanatofautiana, kwa maana ya mazingira ya jimbo, mazingira ya mikoa, halikadhalika mazingira ya wilaya na hata mazingira ya kata. Kuna maeneo ambayo yanahitaji sana huduma hii ya elimu, na kuna maeneo ambayo tunasema kwamba, yana afueni. Kwa mfano, tukichukulia maeneo ya vijijini, ni maeneo ambayo yanahitaji sana huduma ya elimu. Tunahitaji sana kutoa kipaumbele katika maeneo haya, kwa sababu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mazingira yaliyokuwepo bado yamesababisha wananchi wa vijijini kupata elimu isiyotosheleza, kwa maana watu wengi wanakosa kuwa na elimu stahiki. Pia, wale wachache wanaopata, bado wanashindwa kuitumia elimu hiyo katika kufanya maendeleo ya hali halisi ya pale walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Sera za Elimu ni lazima uzingatie haki za binadamu kwa maana elimu ni haki ya msingi kabisa na Kikatiba na ni haki ya binadamu. Hivyo, kila mtu anastahili kupata elimu kwa kiwango cha juu kabisa, na hii ndiyo itasababisha kwamba, haki imetendeka kwa wananchi wote katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumefanyika jitihada kubwa ya kupeleka miundombinu kadha wa kadha, lakini kama nilivyosema katika maeneo ya vijijini, kwa mfano ukichukulia katika eneo langu, kwenye jimbo langu, bado nina uhitaji mkubwa wa elimu, hususan elimu ya sekondari na elimu ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba kwa sasa hivi ukizungumzia kwenye kata, takribani kata zote za Jimbo la Lulindi kuna shule za sekondari. Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hilo, lakini ninachoongelea hapa ni kwamba, kuna baadhi ya kata zina vijiji zaidi ya 11, kwa maana, bila shaka kata hizi zinahitaji kuwa na shule mbili za sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukichukulia Kata ya Mkululu ni kata ambayo inastahili kuwa na angalau shule mbili za sekondari. Halikadhalika, ukienda kwenye Kata ya Mchauru kuna hali hiyo, na ukienda Kata ya Mbuyuni, maeneo haya ni maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa. Kwa sababu gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji viko mbalimbali sana. Kutoka eneo moja kwenda kutafuta elimu inachukua umbali mrefu kweli kweli, ili ufike. Kwa mfano, ukitoka kule Namtona uende ukaitafute Nakachereni iliko, ni takribani zaidi ya kilometa saba; lakini ukitoka Namtona kwenda kuitafuta Sekondari ya Lupaso iliko, ni takribani kilometa 21.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia mazingira hayo, watu wengi sana, kwa maana ya vijana na watoto, wanakatishwa tamaa kwenda kusoma huko. Kwa hiyo, angalau tukiweka shule maeneo ya karibu wataweza pia kusogea hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuunganisha hilo pia, ningetamani tuwe na upendeleo mahususi kabisa katika shule hizi za vijijini. Kuwe na mabweni katika shule zote za sekondari kwa sababu, umbali ulioko unawafanya watoto kushindwa kabisa kwenda kutafuta elimu, ni mbali. Kwa hiyo, kukiwa na mabweni itawashawishi watoto wengi kupata elimu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna uduni wa elimu inayotolewa pale, ambao unatokana na hali halisi, mojawapo ikiwa ni uchache wa walimu waliopo. Kwenye jimbo langu kumekuwa na changamoto kubwa sana ya walimu, ambayo nimekuwa nikiizungumzia hapa Bungeni mara kwa mara, lakini haijapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu unakuta mwalimu yuko mmoja tu na hiyo ni shule ya sekondari au unaweza ukakuta walimu wako wawili tu na wanatakiwa wafundishe kuanzia form one hadi form four, lakini hata kwenye shule za msingi hali iko hivyo hivyo, kuna changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, jambo hili alichukulie kwa umuhimu mkubwa kabisa katika Jimbo langu la Lulindi. Kuna changamoto kubwa nilishazungumza hapa mara kwa mara, natamani atakapokuja ku-windup anieleze una mkakati gani maalumu kabisa kwa niaba ya Jimbo la Lulindi? Ni kwa jinsi gani tunaweza tukaondokana na hii adha ya uchache wa walimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika, nashauri suala la ujenzi wa nyumba za walimu lingeweza kusaidia sana kwa kiasi kikubwa walimu ambao wanakuja wasiondoke, kwa maana ya kutaka kuhama kukimbia mazingira mabaya; wangeweza kushawishika kuishi. Kwa hiyo, nashauri sana, hizi shule za vijijini angalau basi kuwe na nyumba za walimu kwa kuanzia, ili walimu wanavyokuja waweze kuwa wana sehemu za kuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, natamani sana kuwe na bonus maalumu ya ufundishaji vijijini. Mwalimu wa kijijini asilipwe sawa na mwalimu wa mjini. Mwalimu wa kijijini alipwe mshahara mkubwa, ili kumshawishi yule mtu anayetaka kukimbia aendelee kubaki kule kwa sababu ya mshahara. Eneo hilo ninafikiri lingeweza kutusaidia pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine natamani kushauri kwamba, kuwe na upendeleo maalumu kabisa kwa wale wanaoomba kutoka katika maeneo ya vijijini. Kukiwa na watu wanaomba kutoka vijijini, basi wapewe upendeleo wa kwanza kabisa kuajiriwa kuliko hawa wa mjini kwa sababu, mazingira yao yako tofauti na mazingira yao, ingeweza kusaidia sana wao kuendelea kukaa kule vijijini badala ya kukimbilia mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)