Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nianze kwa kumpongeza Waziri na timu yake yote, lakini niendelee kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye eneo la elimu jumuishi. Tukizungumzia suala la elimu jumuishi, ni elimu ambayo kwa ujumla wake inahitajika isimwache mtu nyuma. Mimi nimejaribu kupitia Taarifa ya Waziri, nimeona amezungumzia masuala yote hayo yanayogusa elimu jumuishi. Nikilisema hilo, maana yake ni kwamba tunakwenda kuwalenga watu wenye mahitaji maalumu. Watu hawa ni sehemu ya jamii yetu, hatuwezi tukashiriki elimu kwa mapana yake wakati wao tunawatenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sura hiyo nikijielekeza, kwa mfano, kwenye eneo la mikopo ya elimu ya juu, nimeona kwa kuanzia kulikuwa na shilingi bilioni 787.4 kwa mwaka 2024/2025 kutoka shilingi bilioni 570 ya mwaka 2021/2022 ambapo wanafunzi walitoka 177,925 mwaka 2021/2022 hadi 248,000 mwaka 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukisema suala hilo la mikopo ya elimu ya juu, ningetamani, nikirudi kwenye point yangu ya elimu jumuishi, tunapokutana na watu wenye mahitaji maalumu katika eneo hili la mikopo, nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri, tuje na upendeleo kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni anapokwenda kushiriki mkopo wa elimu ya juu na ukiangalia mahitaji ya mtu huyu, angeweza kupata hata ruzuku kwa sababu, ana mahitaji ya ziada. Kwa hiyo, tunapomweka kwenye kundi moja, na sisi tusiokuwa na mahitaji maalumu naona hapo Serikali inatakiwa tupaangalie kwa namna ya pekee, nashauri kama ni ruzuku au scholarship, kitu cha namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la elimu jumuishi, kwenye suala la vifaa saidizi, watu wenye mahitaji maalumu, kwa maana ya vifaa saidizi, wenzetu hawa nimejaribu kupitia hapa, wanakutana na changamoto kubwa. Mathalan kiti-mwendo ni kati ya shilingi za Kitanzania 600,000 hadi 1,200,000. Kuna kifaa cha masikio, ni kati ya shilingi 800,000/= hadi 3,500,000. Vifaa ni ghali mno, na kama kweli tunahitaji watu hawa washirikishwe katika suala zima la kupata elimu na mahitaji mengine ya namna hiyo, Serikali iangalie namna ambayo ama kutakuwa na msamaha wa kodi, hasa kwa maana ya vifaa hivi ambavyo vinakuwa ni ghali mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, kuna suala zima la eneo la utambuzi na upimaji wa total. Nikilisema hili, na Waziri anisaidie hapa, Wizara itusaidie katika eneo hilo. Leo utakutana na mtoto darasani anaweza akaonekana labda ni mkorofi, hataki kusikiliza au mambo ya namna hiyo, lakini kimsingi kumbe mtoto huyu ana tatizo la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo la upimaji na utambuzi wa watoto, suala hili natamani isiwe tu ni Wizara ya Elimu peke yake, inaweza ikashirikisha Wizara ya Afya na watu wengine wa namna hiyo, ili tutakapombaini mtoto katika hatua za mwanzo, itakuwa ni rahisi kupunguza madhara huko mbele ya safari.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mtu labda hata uelewa wake darasani ni mdogo, ukifikiri labda akili yake ni ndogo, no! Kumbe kuna tatizo la msingi. Kwa hiyo, vituo hivi vya upimaji, ninashauri viendelee kwenda mpaka katika ngazi za halmashauri zetu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, naomba kuhusu lugha ya alama. Tukizungumzia lugha ya alama, watu wanaweza wakaona hili ni jambo la namna gani? Lugha hizi kwa ujumla wake zikafundishwe kama yalivyo masomo mengine yoyote katika ngazi zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili, ni muhimu kweli kweli, mtu mwingine anafikiri kwamba, hizi lugha za alama ni kwa ajili tu ya watu wenye ulemavu. Iko katika sura hii, mtu mwenye ulemavu anaweza akahitaji kwenda kupata huduma za kifedha, labda benki, mtu mwenye ulemavu anaweza akahitaji kwenda kupata huduma TRA, mwenye ulemavu anaweza akaenda katika maeneo yote hayo na kuhitaji huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa isije ikawa labda tunamhitaji tu awepo mwalimu au mtu mwingine wa namna hiyo. Ikiwa sote tumebahatika kuzijua lugha za alama inakuwa ni msaada mkubwa mno kwa sababu, inafika mahali ni uhitaji. Nimezungumzia habari ya elimu jumuishi. Ni uhitaji kama ulivyo uhitaji mwingine wowote. Leo nimejaribu hata kutoa mfano mmoja mdogo, japo hilo linatakiwa liende mbali zaidi, kwa maana ya utaalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka hata Traffic Police anavyokusimamisha hivi, halafu anaelekeza hivi, ametumia alama. Sasa tunatakiwa twende mbali zaidi katika masuala mengine ambayo yatafanya hawa wenzetu nao waone wamejumuishwa katika shughuli zetu za kila siku. Naomba hiyo lugha ya alama, nimesema, tuiweke kwenye sura hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba kuna suala la akili mnemba (Artificial Intelligence). Wenzetu wenye ulemavu, kwa maana ya elimu jumuishi, tunasemaje katika eneo hilo na tunawashirikishaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tuone kwamba, dunia tunayokwenda sasa hivi hatuwezi tukakwepa suala la elimu hiyo ya Artificial Intelligence (akili mnemba) au whatever lugha yoyote ambayo inaweza ikazungumzwa hapo. Kwa hiyo, isiwabague watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo nilikuwa naomba nihitimishe. Ninafarijika, nimeona tunazungumzia changamoto za mdondoko wa vijana, lakini kwa maana ya changamoto hii tumeambiwa kuna ujenzi wa shilingi bilioni 28.7 wa shule saba za kanda ambapo shule hizo zitasaidia hasa watoto wa kiume. Ni katika mwendelezo wa Serikali kukabiliana na suala zima la mdondoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)