Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai, tuko hapa tunachangia Wizara yetu ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mapinduzi makubwa mno katika elimu nchini. Sisi sote tunatambua ni namna gani alivyoleta mapinduzi juu ya suala hili la elimu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namshukuru na kumpongeza sana Waziri wa Elimu, kwa kweli anastahili pongezi na anastahili sifa. Amefanya kazi kubwa sana katika Wizara hii na ameleta mapinduzi makubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Adolf Mkenda kwa kweli anastahili pongezi kubwa. Pia namshukuru na kumpongeza Naibu Waziri QS Kipanga, naye pia amekuwa madhubuti katika kumsaidia Waziri wetu wa Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru na kumpongeza tena Katibu Mkuu wa Wizara hii Profesa Carolyne Nombo, amefanya kazi kubwa sana, tangu ameingia katika Wizara hii tunaona Wizara imetulia mno. Vilevile nawapongeza wataalam wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba tunaishukuru Serikali katika Jimbo letu la Tunduru, tumepata shule mpya nne kwa awamu hii ya mama yetu mpendwa, ambapo kwa muda mfupi tumepata shule kubwa nne ambazo mpaka sasa zinafanya kazi vizuri. Tunashukuru na kuipongeza Serikali kwa namna ilivyotuletea zile shule kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nayo maombi machache katika shule ile. Natambua kuwa Wizara ya Elimu inasimamia elimu, lakini majengo yako chini ya Wizara ya TAMISEMI. Kwa hiyo, naomba, Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI, basi tuweke mkakati wa kuhakikisha kuwa zile shule zote za sekondari tulizozipata ziwe na mabweni kwa ajili ya wanafunzi ama hosteli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Kwa mfano, Shule ya Sekondari ya Kungu pale Nakayaya, watoto wengine wanaosoma pale wanatoka kilomita nane, wengine wanatoka kilomita tano, wengine kilomita nne. Wakati mwingine wale watoto ni wa kike, kwa hiyo, kutoka asubuhi kwenda shuleni na kurudi jioni inakuwa ni ngumu sana. Otherwise ni lazima wazazi wawatafutie vyumba ili waweze kupanga na hatimaye kuondoa usumbufu wa kwenda na kurudi shuleni. Sasa hii inaleta shida kubwa mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwamba shule zile zipatiwe hosteli ili wanafunzi waweze kulala pale pale shuleni na wapate utulivu ili waweze kupata elimu iliyo bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunazo shule za sekondari pale ambazo hazina uzio. Kuna Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Masonya haina uzio na ipo katikati ya mji, upande mmoja ni mji na upande wa pili ni mashamba; kuna mikorosho. Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba sisi kwetu tumezungukwa na hifadhi. Sasa wakati mwingine simba wanakuja pale shuleni, fisi pia wanakuja shuleni ilihali shule ile ni ya wasichana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna changamoto nyingi. Kuna changamoto za wanyama na pia kuna changamoto ya vijana wale wanaotamani sketi, kwa maana ya wale wanafunzi wa kike huwa wanasumbuliwa sana. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI tuzipatie uzio Shule ya Sekondari ya Masonya na Shule ya Sekondari ya Nakapanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nizungumzie suala la Tawi la Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Nimesimama hapa leo hii kwa mara ya pili ama ya tatu, kama sikosei, nazungumzia suala hili la Tawi la SUA pale Tunduru.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato huu tuliuanza tangu mwaka 2018, leo hii tunazungumza miaka saba sasa imepita, lakini bado hatujakamilisha kupata chuo na wanafunzi waendelee kupata mafunzo yao pale ya kilimo kwa muda wote. Isipokuwa mpaka sasa wanafanya practice kwa siku 14 kwa kila mwaka. Yaani kila mwaka wanakuja wanafunzi kutoka Sokoine na maeneo mengine wanafundishwa pale kwa siku 14 tu, baada ya siku 14 wanaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kuwa pale kulikuwa na majengo ambayo yametolewa na halmashauri, majengo hayo ni yale ambayo yalikuwa yameachwa na wakandarasi wa barabara. Pia, tulitoa mashamba ekari 500; na wale wenye mashamba waliridhia kukiachia chuo; na baada ya hapo wakaambiwa wasiyaendeleze. Kwa bahati mbaya sana hakukuwa na mthamini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadaye katika hali ya kutafuta mthamini na watu wamekaa kwa muda mrefu baada ya kuona mashamba yale hayaendelezwi, chuo hakiendelei wakaamua kuyatwaa tena yale mashamba na kufanya shughuli zao za kilimo. Baadaye, baada ya kuomba sana, ndipo SUA wakatupatia 18,800,086,690 kwa ajili ya kufanikisha kupata hati ya eneo lile la Tawi la SUA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ataona, kwamba kwa miaka saba yote, na mchakato ule tulivyouanza mpaka hivi sasa kitu pekee tulichokifanikisha ni kuwa na mchakato wa kupata hati peke yake, ili kuweza kuweka majengo pale, kwa maana ya kwamba Serikali haiwezi kuwekeza eneo ambalo halina hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najiuliza, kwamba kama hati peke yake tumechukua miaka saba vipi, majengo yenyewe yatakamilika kwa miaka mingapi? Hilo ni swali ambalo najiuliza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba baada ya kupatikana fedha ile ya hati, mthamini amekwenda, amefanya uthamini wake na watu ambao wanahitaji kulipwa pale mpaka sasa kutoka kwenye ekari 500 zimebaki ekari 300 tu peke yake, lakini zile ekari 300 zinao watu ambao wanadai fidia, na fidia yake siyo chini ya shilingi milioni mia tatu na kitu hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala hili kwake ni dogo sana. Shilingi milioni mia tatu na kitu, kwamba halmashauri imeshindwa kulipa! Namwomba atuisaidie Halmashauri ya Tunduru kuweza kulipa fidia ya watu wale ili eneo lile lipatikane na hatimaye hati ikamilike na baada ya hapo tuweze kukamilisha chuo kile cha kilimo na tuweze kupata tija ya elimu ya kilimo kwenye Wilaya yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna Mheshimiwa Waziri anavyoweza kufanya kazi na jinsi alivyoleta mapinduzi makubwa kwenye Wizara hii, jambo hili ni dogo sana, haliwezi kumshinda. Shilingi milioni 300 ni ndogo sana katika Wizara hii. Naomba sana sana sana atusaidie katika jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba nimalizie na suala la VETA. Kwenye wilaya yetu sisi hatuna chuo kabisa na Tawi hili la SUA ndilo ambalo lilikuwa linakuja sasa kutuamsha na kutufumbua. VETA pale majengo ya awali yalianza kwa speed kubwa sana, na Wanatunduru walifurahi kweli kweli kuona sasa watoto wao wakimaliza elimu hawatakwenda mbali kupata elimu yao ya ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpaka sasa, baada ya yale majengo ya awali kuanza, yamefika sehemu yamesimama, hakuna kinachoendelea. Tunatambua Serikali inafanya kazi kubwa sana, ina mambo mengi na miradi mikubwa inatekeleza, lakini tunaomba ichukulie mkazo kwa umuhimu wa peke yake ili tuweze kusukuma ile VETA ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)