Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia machache juu ya hoja ya Bajeti ya Wizara ya Elimu iliyopo Mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameonesha utashi wa kisiasa kuhusu utoaji wa elimu katika nchi yetu. Hakuna kipingamizi au maneno yoyote tunayoweza kusema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli shule nyingi sana zimejengwa katika nchi yetu kipindi hiki. Zaidi shule za watoto wa kike zimejengwa kila mkoa. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Rais wetu kwa kuliona hili, na kwa kweli apate maua yake. Unapomsifu mtu, tunasifu na uwezo wake, tunamsifu pia kuwa ni mwanamama kwamba kwa kweli amejitahidi sana kuhakikisha nchi yetu, watoto wetu wote wanaweza kupata nafasi ya kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitauelekeza katika mdondoko wa wanafunzi (dropout). Nimesoma katika Randama ya Wizara ya Elimu ya Bajeti ukurasa wa 18, wamejitahidi kutuonesha takwimu kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Randama hiyo mnasema mwaka 2020/2025 wavulana 5,613 na wasichana 10,239 ambayo inaleta karibu wanafunzi 15,800 wameweza kurejea katika mfumo rasmi wa elimu, lakini ukienda TAMISEMI sasa, wao wanasema 2023/2024 wana wanafunzi wavulana 76,125 na wasichana 72,218 ambayo inakuja takribani 16,000 hawa wamedondoka, ndiyo mdondoko huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakuja NECTA; wao wanasema 2022/2023 wana wanafunzi 503,094 ambao hawakumaliza mitihani yao. Sasa nataka niiulize Serikali, kwamba je, kwa takwimu hizi ambazo zinatoka kwao, zinatoka TAMISEMI na NACTE, ni kipi kipo sahihi? Napenda niishauri Wizara ya Elimu, kwamba wafanye utafiti sasa ili wahakikishe kwamba tunajua ukubwa wa tatizo hili. Jambo hili wasilipuuzie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, ni kwamba, Mheshimiwa Rais wetu amejitahidi kujenga shule, kwa hiyo, nchi ina-invest kwenye elimu, halafu kuna watoto ambao wanapotea huku hatujui hata mahali walipo. Hawafanyi mitihani, hawamalizi shule wasichana kwa wavulana; na wao huku kwenye randama wamesema wavulana ndio wengi. Kwa hiyo, ni lazima tufanye utafiti, waje na jibu ili wapate takwimu, waweze kupanga mkakati ulio rasmi wa kuweza kukabiliana na janga hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimetazama katika mpango wao wa bajeti, hakuna mahali ambapo wamegusia, yaani tuseme kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri hana kitu chochote alichotuwekea kwamba, je, mwaka huu kama walisema mwisho ni shilingi milioni 15, je, sasa hivi hii bajeti ambayo ni ya mwaka 2025 wameweka wanafunzi wangapi ambao watarejea? Kwa hiyo, tungetaka kujua kwamba watarejea wangapi ili tuone kwamba tunaweza kupunguza hili tatizo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua hii takwimu ya TAMISEMI ni wanafunzi zaidi ya laki moja na arobaini na kitu. Ukitoa hiyo kumi na sita tuna wanafunzi 120,000 ambao hawamalizi shule, wanatoweka mitaani na hatujui mahali waliko ilhali tuna-invest na tunaweka watoto wetu. Je, baada ya miaka 10 ni kitu gani tutakachokuwa nacho?

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri kwamba, wahakikishe kuwa wanafanya utafiti, wanahakikisha kuwa tunaweza kumaliza hili tatizo la wanafunzi wetu kutomaliza shule. Ukizingatia kwamba, tunapo-discuss bajeti hapa ni kwamba, tunaangalia mipango yetu ya nchi, na mipango hii tunaitafsiri katika fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kwamba, bajeti haipaswi kumwacha mtu nyuma. Kwa hiyo, tuhakikishe kwamba watu wote wanakuwa included, bajeti inawaunganisha kwa pamoja, mipango yetu inawafanya na wao wafaidi bajeti yetu ambayo tunapitisha leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda niliongelee ni kuhusu walimu. Ni kweli kuwa tuna uhaba mkubwa wa walimu, lakini sitaongelea uhaba. Nitakachoongea ni kuwa, ni kwa namna gani Serikali inaweza ikaandaa wanataaluma ya ualimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwalimu professionally, nilisoma kwenye chuo cha ualimu, nimepitia hatua zote. Najua mwalimu anavyoandaliwa. Unakwenda block teaching una mwalimu wako nyuma, unajifunza methodology, unajifunza vitu mbalimbali, unapikwa na baadaye unafanya mtihani, wanakupa certificate kwamba, sasa nenda unaweza kufundisha watoto wa umma. Ndivyo tulivyosoma na ndivyo tulivyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulifundishwa mpaka BBD, inaitwa blackboard what, lazima ufunzwe hata namna ya kuandika ubaoni, unafundwa kila kitu. Sasa wanawaandaa walimu halafu wanawa-dump. Tunao watoto mtaani wa mwaka 2018 mpaka leo. Sasa wamemsomesha mtu, wamempa certificate anakwenda kuwa bodaboda, anakuwa kwenye vibanda vya fedha, anakuwa mama lishe kwa sababu lazima ajikimu. Halafu wanatangaza ajira, wanataka kumpa mtihani, upi? Ana certificate yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi cheti changu cha ualimu ndicho kilichonipa ajira, kwa sababu nilipita chuoni wakaniambia kwamba sasa Conchesta unaweza kwenda kufundisha watoto wa umma. Sasa wamewapika, wamewaandaa, wanatupa taaluma ya ualimu mitaani, halafu wanawadhalilisha na kuwanyanyapaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wao mtu akiwapa mtihani wataufanya sasa hivi? Hata wa darasa la saba watashindwa. Eeeh! Kwa hiyo, wasiwanyanyapae, waje na certificates zao, waliandaliwa kule. Hivi vyuo wanavidharau, waweke mitaala ya bodaboda kule basi, waweke mitaala ya mama lishe. Wajue kwamba, walimu hawa wakishasoma watatoka huko watakwenda kuendesha pikipiki. Watakuja sasa utawaambiwa kwamba, umekuja tuambie gia ya pikipiki inawekwa namba ngapi ili kusudi tukupe ualimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali waache kupoteza taaluma ya wasomi hawa, walimu, wanawa-dump halafu wanasema kuna uhaba wa walimu. Wawatoe waje na vyeti vyao, wanalalamika. Unakwenda kumuuliza maswali gani? Mimi hata siyajui, labda wengine wanajua wanawauliza maswali gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wewe umesomeshwa na mwalimu wako halafu baadaye Mheshimiwa Prof. Mkenda unamwambia x + y au unamwambia nini? Yeye amesoma taaluma yake na amekabidhiwa cheti, halafu unamweka miaka sita, jamani, ni mtu gani huyo ambaye anaweza kukaa miaka sita bado anakumbuka alivyoambiwa uwe msafi darasani?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili kwa kweli silipendi sana. Kwa mawazo yangu mimi mwenyewe, napenda watoto waje, hakuna interview. Waje na certificates zao. Kama ni certificate, walifoji? Kama walimu wamewapika, wamepikwa wamekuwa walimu kama sisi, anakuja na certificate, ndiyo nyenzo ambayo inaweza kumfanya kuwa mwalimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)