Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi ili nami nitoe maoni yangu katika Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya kielimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshuhudia ongezeko kubwa sana la mikopo katika elimu ya juu na elimu ya kati. Pia kuondoa ada kwa masomo ya advance, kitu ambacho kimewezesha watoto wengi kuendelea kusoma masomo ya advance.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri na wenzake wote Wizarani kwa kupeleka VETA pale Nyamongo. Nimeambiwa mpaka mwezi wa Saba inaweza ikawa imekamilika vizuri zaidi kwa majengo ya awali, ili wale vijana ambao wanafanya kazi ya uchimbaji, na wanaolima karibu na Mto Mara pale wapate course na waweze kufanya kazi za kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tunaomba Mheshimiwa Waziri waweke nguvu katika kile Chuo cha Kilimo Butiama ambacho kina heshima kubwa ya jina la Baba wa Taifa pale ili kiwe Chuo kamili kama ilivyo Chuo cha Sokoine na watoto wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine wapate hiyo taaluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa Rais aliahidi pale Hospitali ya Kwangwa iunganishwe na utalaamu wa kidaktari na manesi ili wanapoenda pale kufanya kazi ya mafundisho pia wafanye kazi ya kuhudumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la mitaala hii, tumekuwa na mjadala mkubwa sana katika nchi yetu. Ukiangalia Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa, kwamba ni kweli kumekuwa na wanafunzi ambao wameenda vyuo vikuu, wamehitimu lakini wamekosa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapambana hapa kusugua ubongo, kutafuta namna ambavyo tutafanya kupunguza gap kubwa ya ajira iliyopo Tanzania, watakaopata kazi ya ajira katika sekta mahsusi, sekta binafsi au wakajiajiri lakini wapate utalaamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja imejitokeza hapa asubuhi nataka niisemee kidogo, mimi ni Mwalimu wa Hesabu na Chemistry, kwamba quadratic equation haina maana. Ukiingia kwenye google sasa hivi hapo ulipo Mheshimiwa Mbunge wewe andika tu hapo, “use of quadratic equation in life,” utakuja kuona ni vitu vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kwa watu ambao wameenda jeshini kitaaluma, military bases zile, ukitaka kufanya projection, unaipiga ndege imeruka hapo, uipige pale; ni lazima ufanye projection ya sayansi, na hiyo equation ni quadratic equation.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, watu ambao wamefika NASA kule Marekani, unazungumza kurusha parachute satellite, unazungumzia quadratic equation applications, zipo pale. Kwa hiyo, kuna vitu vingi, lazima hii tuisemee kwamba siyo kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, ila wale ambao wanaweza kuisoma quadratic equation wakafaulu, waache waendelee; wale ambao wanataka kusoma Kiswahili na Historia waache waendelee; wale ambao wanasoma ili wapate ajira tu, waendelee. Hapa kuna taaluma, kuna fani na kuna watu waliobobea, hao tuwaache waende kwenye sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, huwezi kuniambia kwamba hakuna matumizi ya periodic table; no periodic table no chemistry. Huwezi kuzungumza atomic nuclear hapa, atomic energy, nuclear energy zile elements zimekuwa raised accordingly to the increment of atomic number na atomic mass. Huwezi kuzungumza electrolysis hapa, huwezi kuzungumzia habari ya umeme positive and negative charges move, hii ni periodic inafanya kazi tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii hizi taaluma za watu tuwaachie wengine waendelee. Tunapata shida kuwashawishi watoto wasome sayansi, watakimbia masomo. Nenda kwenye shule ukafanye sampling yoyote ile, wengi wanaenda kwenye arts.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri, sasa hivi pia imeibuka hoja kwenye taaluma hizi, tusichanganye habari. Kuna watu wanachangia sasa hivi hoja, wanazungumza upungufu wa ajira versus taaluma, hapana. Vijana mtawaandaa duniani watapwaya sana. Ukienda kwenye vyuo vingine, hutaenda, na ukiacha sayansi kwenye ngazi ya chini, huko mbele ni shida kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, waache vijana wajaribu, wale wanaoweza kusoma physics, wanasoma biology, wasome chemistry. Mwili wa binadamu huu 96% una carbon, una oxygen, una nitrogen, una hydrogen humu ndani. Unawasha taa nyumbani ni chemistry ile, bulb ni chemistry ipo pale, helium ni chemistry, unazungumzia gesi ni chemistry. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani haya mambo niseme kwamba siyo wote ni wanasiasa na sisi tuna taaluma zetu hapa tumetulia. Kwa hiyo, ukigusa kidogo, lazima tutatofautiana katika maeneo hayo ili turudishe watu kwenye msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kuna hoja imejitokeza sasa hivi, nimeenda kwenye shule zangu kule, ni kweli wameanza utekelezaji wa mitaala mpya, lakini ataka kumwambia Profesa, kuna changamoto ya walimu waliobobea katika huu mtaala mpya, uelewa ni mdogo sana, na kuna upungufu mkubwa sana wa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia mwaka 2024 kwamba kama ungeweza kufanya tathmini upya, kama unaweza kufanya wakati mmoja kuanza mtaala mpya, tuendelee; kama unadhani hatuwezi, mngefanya sampling baadhi ya shule muimarishe walimu wapatikane. Hapa amesema amefundisha walimu wa shule ya msingi na awali aah, fundisheni mpaka sekondari zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hata walimu wa masomo ya Kiingereza kwenye shule hawapo. Wanafunzi wana-struggle. Ametoka shule ya msingi, amesoma masomo yote Kiswahili halafu anaenda sekondari hana mwalimu wa English, halafu unataka aelewe masomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye shule yangu, Jimbo zima mwaka 2024, watoto wa form two waliopata division zero 1,539 kwa mwaka mmoja. Ukienda division four ni wanafunzi 3,710 hiyo ni mwaka mmoja. Nenda miaka mitatu nyuma, kuna shida ya lugha ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twendeni tukaandae walimu wanaojua Kiingereza na Kiswahili vizuri. Bora akosekane mwalimu wa hesabu, kwa muda atafundishwa hata mtaani, lakini lugha inafanya watoto wakose masomo na wanakimbia masomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo mmesema habari ya mimba, ongeza tena, kuna mimba, kuna kuolewa, kazi za majumbani na kushindwa kujua lugha. Mwalimu mwenyewe anayefundisha Kiingereza shuleni hajui Kiingereza. Mwanafunzi anashangaa mwanzo wa kipindi mpaka mwisho wa kipindi halafu unampa mtihani afaulu, hapo mtihani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri ni muhimu sana Serikali ijipange kuandaa Walimu wazuri wa Kiingereza na ikiwezekana watoto kabla ya kuingia form one wafanye orientation course, kama vyuo vikuu wanafundisha CR siyo! Tumefundishwa zile. Kwa hiyo, hawa watoto wasaidiwe lugha ya mawasiliano na namna ya kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ningetaka nione kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri, walitenga shilingi bilioni 17 ziende kwenye Taasisi ya Elimu ili kuchapisha, kusambaza na kuandika vitabu. Fedha imekaa TAMISEMI miezi mitano, imerudishwa Hazina. Kule Shule yangu ya Kubiterere, Nyagisya, Kimusi, na Nyabichune kuna kitabu kimoja cha chemistry tu cha mtaala mpya, halafu fedha imekaa miezi mitano!

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu tuelezeni ni nini kilitokea? Shilingi bilioni 17 haikufanya kazi ikarudi Hazina, watoto hawana vitabu, walimu hawana vitabu vya kufundishia. Halafu hawa watu wa TAMISEMI waliwachukulia hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini fedha isitoke Wizara ya Elimu moja kwa moja wapeleke Taasisi ya Elimu waka-print, wakaandike, na wakasambaze? Kwanza shule unakuta ina upungufu wa walimu. Tarime Vijijini tuna upungufu wa walimu wa Sayansi 145, sasa hakuna mwalimu wa Sayansi, hakuna kitabu cha Sayansi, mwalimu hana, hata shule ya jirani huwezi kuazima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani huu mtalaa hebu tujipange vizuri. Mambo ambayo tunaweza kuyatekeleza ndani ya uwezo wetu tuyafanyie kazi. Baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara, sasa ungetupatia kabisa na Newton’s Law of Motion. (Kicheko)

MHE. MWITA M. WAITARA: Eehee!

NAIBU SPIKA: Aaah, kaa chini! (Kicheko)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni baharia, umesoma sayansi kidogo. (Makofi/Kicheko)