Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaomba nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwenye Wizara kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye elimu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Geita hasa Geita Mjini ni mashahidi. Tumeshuhudia ongezeko la shule nyingi za msingi, sekondari, pia Ujenzi wa Shule Maalum ya Wasichana Geita Girls ambayo imekamilika na sasa inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kabla sijaendelea, namhakikishia Mheshimiwa Waziri kwamba hoja inayozungumzwa ya walimu ni tatizo kubwa sana, ingawa nadhani inawahusu sana TAMISEMI, lakini nina hoja mahsusi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule yangu moja ya Shanta Mine na shule nyingine ya Geita Sekondari kuna walimu wanajitolea pale wa Hesabu na masomo ya Sayansi na zilipotangazwa nafasi za ajira hawa walimu wakaenda kufanya interview, katika shule hizo. Katika shule hizo, nakuruhusu u-google ataona matokeo ya hizo shule ni division one, division two watoto wanafaulu masomo ya Sayansi na Hesabu, lakini hawa walimu walioenda kufanya interview wakafeli, interview ambayo wameletewa kutoka Wizarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamefundisha watoto wanafaulu lakini wanafeli interview inayokuja kufanywa ili waweze kuajiriwa, sasa napata shida sana, amesema hapa mchangiaji wa kwanza na wa pili nini kinatokea hapa? Kwamba mwalimu ambaye anafundisha watoto wanafaulu, akija yeye kufanyiwa interview anafeli.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona wengi wanalalamika wanaona kama kuna upendeleo, kwa hiyo, nafikiri kuna haja ya kuangalia vizuri, lakini hilo pia litusaidie kwenda kwenye vyuo vyetu kuangalia pengine mahitaji ya walimu ya sasa na wanaoandaa mitihani ya interview hayafanani na walimu waliofundishwa zamani na hii ndiyo changamoto ambayo tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kwa Mheshimiwa Waziri, ni mwaka 2024 wakati wa maonesho ya madini pale Geita, nashukuru sana alikuwepo Mheshimiwa Waziri pamoja na Mawaziri wengine karibu kumi. Maonesho yetu yalihudhuriwa na Mheshimiwa Rais na Wananchi wa Geita wanakumbukumbu na maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maombi ya wananchi wa Geita, tunaipongeza Serikali kwa ujenzi wa Chuo cha VETA. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia Chuo angalau kikakamilika na kimeanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimweleza kwamba mwaka 2024 kilikuwa na upungufu mwingi, akaahidi atakuja. Nadhani muda upo, utakuja, lakini yapo maombi maalumu tuliyaleta wakati wa maonesho yale, tunataka Chuo chetu za VETA cha Geita Mjini kifundishe zaidi teknolojia ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunasema hivyo? Kwa sababu vijana wengi wanaozunguka maeneo yale wanatamani kufanya kazi kwenye maeneo ya madini. Wanatamani kufanya kazi ambazo zina uhusiano na shughuli za mitambo ya madini, shughuli za uchenjuaji wa madini, shughuli za uchimbaji wa madini, shughuli za utambuzi wa madini, na shughuli za ku-process madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa natamani kuona kwenye bajeti hii, Mheshimiwa Waziri akiwa amechukua yale maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo wananchi wa Geita wanatamani kuyaona kwenye bajeti hii yakiwa yameingizwa kwenye bajeti yake, ikiwa ni pamoja na kukipa Chuo kile miundombinu na vifaa vya kutosha ili kiweze kutoa product ambazo zimekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema wakati ule kwamba ni kweli kilikamilika, lakini kilikamilika kwa zimamoto. Ukifika pale utaona ni chuo ambacho hakina vifaa vingi. Tunashukuru kimeanza, safari imeanza na ninaamini kitakamilika, lakini naomba Mheshimiwa Waziri afike akitengee fedha, kitakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye eneo hilo, changamoto ya ajira ni kubwa nchini. Hakuna Wizara nyingine naitazama ambayo itasaidia Serikali kumaliza changamoto hii. Ninalo wazo, badala ya kufikiri kupeleka graduates wakakae VETA mwaka mmoja, miezi sita, miezi mingapi tufikirie kuwa na incubators. Tuwe na incubators nyingi maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, incubators zinaweza zikatengenezwa. Kwanza ziwekewe resources, pawe na mentorship ambayo ita-focus kwenye kukabiliana na tatizo tulilonalo sasa. Kwenye incubators unaweza ukatengeneza entrepreneurs, ukafanya innovations, ukafanya technology mbalimbali, lakini zikawa zime-focus jambo fulani mahsusi na kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, incubators nyingi ambazo ziko huko duniani, zinasaidia sana kwenye kupunguza tatizo la ajira, hata kwenye management ya talents mbalimbali, unakuta kuna mtu ana talent ambayo badala ya kwenda chuo, anaweza kupelekwa kwenye incubator sehemu fulani na kwa muda mfupi akaweza kujitokeza na hivyo kuweza kumwajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maoni yangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba katika eneo hilo badala ya kufikiria graduates wote Tanzania waanze kwenda VETA ama wapi, tufikirie namna ambavyo tutatengeneza incubators ambazo zitasaidia kupunguza tatizo la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo nataka kuzungumza kwa Mheshimiwa Waziri, ni kwamba Wizara ya Elimu ilifuta Walimu wa Grade A. Ikasema, itakuwa na walimu waliomaliza Form Six, tena ikasema angalau division one, two, three, ni jambo jema kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huku chini kuna vyuo ambavyo mtu ana ‘D’ nne anaanza kusoma certificate, anasoma diploma anakwenda kwenye NACTVET, anakwenda anapata diploma baadaye ana-graduate BBA, halafu huyo mtu anakwenda kusoma Post Graduate Diploma ya Education, tunawaona wanaajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kupata ufafanuzi, tumefuta Grade ‘A’ ya walimu ambao wamefaulu Form Four ana masomo mazuri, ana division three, ana ngapi? Huku juu tunaelekea kupokea walimu waliopata ‘D’ nne ambao tu ana degree ya BBA ya kuungaunga halafu akaenda kupata Post Graduate Diploma ya Education ili kwenda ku-cover gap.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwachukue walimu hawa hawa kama tuna tatizo la masomo ya biashara, tukawapeleka incubator, tukawapeleka short course, waliosoma Kiingereza na masomo mengine, tukawapeleka kufundisha masomo ya biashara badala ya kuchukua mtu ambaye ukimtazama kama anavyosema Mheshimiwa Waitara hata anachokwenda kufundisha hakifahamu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani utaratibu huu unaweza kutusaidia tukatoa product ambazo zimepata elimu ambayo kwanza ina viwango, lakini anayefundisha anajua anachokifundisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)