Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Kwanza, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika kuiongoza na kuisimamia hii Wizara ya Elimu. Nawapa hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa maono makubwa ambayo yamepelekea kuufumua mfumo wa elimu hapa nchini na kuja na mitaala mipya ambayo tunaamini inaenda kukidhi mahitaji ya Taifa letu. Tunampa hongera sana kwa hayo maono mapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu yetu, kwanza Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa jina peke yake, maana yake inazo kazi mahsusi kama tatu. Kazi ya elimu, kazi ya sayansi na teknolojia zake. Sasa elimu yetu hii lazima itupatie maarifa na ujuzi utakaosaidia kubadilisha tabia zetu, kubadilisha mitazamo yetu ili iweze kuendana na mahitaji ya Taifa, mahitaji ya jamii na tuweze kuliendeleza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu yetu lazima iwaandae vijana wetu kujenga Taifa linalojitegemea. Hatuwezi kujenga Taifa linalojitegemea kama hatutakuwa na elimu madhubuti yenye kuwapatia maarifa na ujuzi utakaotuwezesha kwenda huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi hii inafanywa vizuri na tumeanza kuifanya vizuri lakini elimu yetu ndiyo inatakiwa kufanya kazi kubwa yaku-support sekta nyingine zote ili ziweze kuendelea na kutoa mchango mkubwa wa uchumi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, viwanda vyetu tunavyotaka kujenga, iwe ni kilimo, iwe ni uvuvi, tunahitaji maarifa na ujuzi utakaosaidia kusukuma na kuchagiza kuhakikisha kwamba tunapata hayo maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kazi hii imeanza na inafanyika vizuri, nami nawapongeza, lakini tunalo eneo la Sayansi na Hesabu ambalo limekuwa ni changamoto kubwa. Mheshimiwa Waziri sasa hivi akienda katika maeneo mengi, akienda katika shule zetu kuanzia za msingi, sekondari na kuendelea, watoto wetu wanaogopa masomo ya Sayansi na Hesabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii maana yake hatuwezi kujenga nchi imara bila kuwa na sayansi na teknolojia. Kwa hiyo, lazima tuwaandae watoto wetu kupenda masomo ya sayansi, kama tunasema sayansi hatuihitaji, maana yake hatutaki kuishi hapa duniani. Bila sayansi hatuwezi kwenda popote. Kwa hiyo, ni lazima tuwaandae vijana wetu kupenda masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni nini tufanye? Ukichukua kwa mfano kwenye hesabu, tatizo la hesabu ni nyepesi na vijana wanaweza kuzielewa, lakini kabla hawajaenda hata shuleni wameambiwa Hesabu ni ngumu, wameambiwa Sayansi ni ngumu. Ukitaka kuona hilo ni tatizo la saikolojia, wewe mpe mtoto hesabu ndogo tu, mwambie mbili kuongeza kisanduku sawa sawa na sita kwenye kisanduku ni ngapi? Anasema hizo nyepesi sana, hizo nilisoma nyepesi sana. Sasa badilisha weka pale mbili kuongeza X sawasawa na sita, (2+X = 6) anasema hizo ngumu za ‘X’ sizijui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unajua kwamba hapa watoto tatizo ni la kisaikolojia zaidi. Kwa hiyo, kumbe Hesabu ni ile ile, formula ni ile ile, lakini anaogopa akishaona ‘X’ akishaona ‘Y’ tayari hesabu imekuwa ngumu. Kwa hiyo, nadhani tujenge misingi ya vijana wetu kuweza kupenda hesabu na kupenda masomo ya Sayansi, hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji wataalamu mbalimbali. niliona mwaka huo wakati Mheshimiwa Waziri anahitaji walimu wa masomo ya sayansi, na walimu wa physics. Somo la fizikia walimu hawakupatikana wa kutosha. Sina takwimu sahihi, lakini niliambiwa hawajapatikana wa kutosha. Sasa hivi katika maeneo mengi tunatafuta walimu wa Fizikia hawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunayo fursa hii, tuwaandae watoto kwenye masomo ya sayansi, tuandae watoto kwenye masomo ya Fizikia, tuandae watoto kwenye masomo ya Hesabu ili tuweze kujenga Taifa letu zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo nataka kusema, Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana, naishukuru sana Wizara, na ninamshukuru Mheshimiwa Rais, wametupatia zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kujenga Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo kinaenda vizuri, kinajengwa vizuri, tunashukuru sana, lakini naomba kile Chuo cha VETA wakati kinajengwa, tunatamani kinapokamilika watoto wa Jimbo la Vwawa wa Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe kwa sababu ni Chuo cha Mkoa, basi na vifaa viwe vimefika ili waweze kupata ujuzi na maarifa mbalimbali yanayohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo letu, sisi tunazo shule za sekondari. Kwa mfano, Wilaya ya Mbozi ni zaidi ya shule 75 za sekondari. Tunazo shule za msingi za zaidi ya 108 kwenye Wilaya ya Mbozi, lakini ukiangalia wale watoto wote wanaomaliza kidato cha nne na Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo kubwa na ni kazi ya Wizara yake kwamba, sasa hivi katika nchi nzima ukiangalia watoto wanaomaliza kidato cha nne, ni karibu shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa vyuo vyetu vya kati, vya juu na vyovyote vile kuchukua hao watoto pamoja na shule za kidato cha tano na sita haufiki zaidi ya 400,000.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hasunga, malizia.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba mweke mkakati hapo. Naomba kwa nusu dakika, tunaomba pale Ikunga wametenga eneo ekari tatu, wanaomba Chuo cha Elimu ya Juu au Chuo cha Elimu ya Kati, eneo lipo pale Nyimbili. Pia kuna eneo Kambi ya Vijana ya Sasanda, pana eneo. Pale Hasamba kuna maeneo tumeyatenga kwa ajili ya elimu. Mkoa wetu tunahitaji vyuo vya elimu ya juu ili viweze kuchangia katika maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)