Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Michael Mkundi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukerewe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Taifa letu lipo kwenye mkakati mkubwa wa kufanya mapinduzi makubwa ya kitaaluma na kielimu, ili tuweze kupata maendeleo ya kiuchumi, na hatuwezi kufikia maendeleo hayo bila kurudi kuimarisha sekta ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2022 kwa mujibu wa sensa, Tanzania ina watu zaidi ya milioni 60, lakini karibu zaidi ya 40% ya kundi hilo ni kundi la umri wa kati ambalo ni kundi la wazalishaji. Kama kundi hili tutalitumia vizuri linaweza kutusaidia kufanya mapinduzi makubwa sana ya kiuchumi. Sasa, ili tufikie huko ni lazima kundi hili litumike, lakini haliwezi kutumika bila kuandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimeona nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uwekezaji mkubwa sana uliofanyika kwenye sekta ya elimu. Nitakuwa sijatenda haki kama sitampongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Mkenda, Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Elimu kwa namna ambavyo wamemsaidia Mheshimiwa Rais kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sekta ya elimu kwenye nchi yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa sana suala la Elimu ya Amali, lakini sambamba na hilo, nilitamani niongelee eneo la VETA. Katika maeneo mengi kwenye mataifa mengi yaliyopata maendeleo na kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi, mengi yametumia hizi vocational training kwa ajili ya kutengeneza wazalishaji mali kwenye viwanda na hatimaye kufikia maendeleo hayo ya kichumi. Kwa sababu tunapoanzisha VETA hizi, hata sisi kwetu hapa lengo la hizi VETA kwanza ni kuandaa utaalam, kuchochea ujasiriamali, kuimarisha ajira na hatimaye sasa kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo furaha kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ameonesha namna ambavyo wanafanya mapitio ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Ni jambo jema sana kwa sababu kupitia mapitio haya kama itafanyika vizuri, jambo hili litatoa mwelekezo mzuri wa namna ambavyo hivi Vyuo vya VETA vinaweza kutusaidia, kwa sababu kama Taifa, tumefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye ujenzi wa VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo ninaamini tukifanya kama ambavyo tunatarajia, itatusaidia sana ku-absorb namba kubwa ya vijana kuingia kwenye taasisi hizi, wakapata uelewa na utaalam ambao utasaidia kufikia lengo letu la mapinduzi ya kichumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka nishauri mambo mawili kwenye eneo hili. Ni lazima kama lengo letu ni kufanya mapinduzi ya kiuchumi, ni lazima tuendane na teknolojia na mabadiliko yanayoendelea kwenye teknolojia, na kwa sababu hiyo, kama walivyosema wachangiaji kadhaa, uwepo wa vifaa vya kisasa vinavyoendana na mabadiliko ya kiteknolojia na sayansi kwenye vyuo hivi, ni jambo la msingi sana. Vile ambavyo tayari vimeshaanza, ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba, vinapatiwa vifaa. (Makofi)

Naibu Spika, vile ambavyo vinaendelea kujengwa, basi utaratibu wa kupata vifaa ni jambo la msingi sana, ili pale ambapo vinakuwa vimekamilika, basi vifaa hivyo vinapatikana. Nikitoa mfano, kwenye Jimbo langu la Ukerewe, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Wizara imetusaidia kujenga Chuo cha Ufundi cha VETA pale Ukerewe, lakini chuo hiki bado hakina vifaa. Walimu wanalazimika kuazima vifaa kwenye vyuo vya jirani ndiyo wafundishe watoto kwenye chuo kile. Kwa hiyo, ni muhimu sana vikapatikana vifaa (machine tools) zikawepo, ili watoto wanapoenda pale waweze kufundishwa na kupata kile ambacho tunakitarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilipenda kushauri vilevile kama ambavyo baadhi wamesema, ni maandalizi ya wakufunzi kwenye vyuo hivyo. Ni muhimu sana tukapata wataalam, ili tunapokuwa tunapata watoto kuweza kupata elimu hii ya ufundi, basi wataalam wakufunzi wawepo kwa ajili ya kuwasaidia kuwa-equip watoto hawa na taaluma ile tunayoitarajia, mwisho wa siku tupate products ambazo zinaweza kutusaidia kwenye eneo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa mfano, vilevile nashukuru kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kwamba wanaandaa wanafunzi 391 wanaopewa mafunzo kwa ajili ya kuja kufundisha, lakini kwangu naona kama hii namba ni ndogo kwa sababu Chuo cha VETA cha Ukerewe kina upungufu kwa mfano wa wakufunzi karibu tisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukiangalia na vyuo vingine nchi nzima bado mahitaji ni makubwa. Kwa hiyo, ni muhimu sana maandalizi ya wakufunzi hawa na hasa wenye uwezo na ujuzi wa kuwasaidia vijana wetu ikahitaji uwekezaji mkubwa, ili tupate wakufunzi wa kutosha watakaotusaidia kwa ajili ya kuandaaa vijana ambao kweli wanaweza kuwa competent, wakatusaidia kufanya mapinduzi hayo ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitamani kuchangia ni juu ya namna ambavyo tunaweza tukapata watoto wazuri wenye uelewa na uwezo wa kitaaluma. Moja kati ya changamoto tulizonazo kwenye Taifa letu, tunachukulia kirahisi sana suala la lishe kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa siku za karibuni kumekuwa na msisitizo kuhakikisha kwamba watoto wanapata chakula wanapokuwa shuleni. Bado kuna uelewa mdogo sana wa jamii yetu juu ya umuhimu wa kuhakikisha kwamba watoto wanapata lishe wakiwa shuleni. Matokeo yake pamoja na kwamba ni kweli Serikali haiwezi kutoa chakula kwa watoto wote, jamii imekuwa inashirikishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jamii inaona kama jambo hili siyo la lazima na muhimu, lakini ni jambo ambalo linaathiri sana watoto wetu kukua kiakili, kuwa na uwezo wa ku-absorb kile ambacho wanapewa kama wanafunzi na hatimaye kuwa watoto ambao wanatoka wakiwa na uwezo wa kulisaidia Taifa, kwa sababu akili inakuwa haiwezi kuwa na nguvu ya uelewa kama ambavyo ingekuwa iwapo wangepata chakula shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali kupitia Wizara ikishirikiana na TAMISEMI itoe mwongozo, elimu au namna yoyote ambayo itafanya jamii ihamasike, ielewe nini umuhimu wa watoto wetu kupata chakula shuleni na hatimaye watoto wale wanapokuwa wanapata chakula, wanakuwa na uwezo wa kuelewa na kupata yale ambayo wanafundishwa na hatimaye Taifa linakuwa na products ambazo zinakuwa na uwezo kweli na nguvu na zinaweza zikasaidia Taifa letu kuleta maendeleo ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshmiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)