Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Napenda kushauri mambo machache katika Wizara hii ya Ardhi. Mheshimiwa Waziri imeonekana kama ana mikakati kabambe kwenye maandishi yake, lakini sijajua alivyojipanga kwa sababu suala la migogoro ya ardhi lipo kila sehemu nchini na halijaanza leo na sitapenda sana kama Waziri anasubiri na Mkoa wa Rukwa yatokee kama yanayotokea Morogoro ndiyo achukue hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wamekuwa na utaratibu mmoja wa kusubiri matukio ndiyo wamnakuja na matamko na mikakati. Nafikiri ni vema kwenye maeneo ambayo haijatokea migogoro, wakaweka mikakati thabiti kuonyesha kwamba wako serious na suala hili. Tatizo wanasubiri matukio ndiyo wanakuja na kauli ambazo hazisaidii chochote, watu wanakuwa tayari wameangamia, wamepoteza maisha, hawana tena cha kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mgogoro wa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na mwekezaji EFATHA, limekuwa ni kero sana kwa Wabunge wanaotoka Mkoa wa Rukwa, tumezungumza mara nyingi sana. Mheshimiwa Waziri amezungukia maeneo mengi lakini Mkoa wa Rukwa bado hatujamwona. Hili suala limeleta shida sana kwani kuna watu wameumia sana pale, kuna watu wamefungwa, sijajua shida ni nini? Hili suala sijui halijafika mezani kwa Mheshimiwa Waziri au kama limefika ni kitu gani kinazuia asije Mkoa wa Rukwa kuangalia nini kifanyike? Nimeona jitihada za Waziri, lakini napenda kuziona pale atakapofika kuzungumza na wananchi wenyewe. Napenda kumshauri ili afanikishe masuala haya, asifanye kazi kama Wizara nyingine wanaopewa maandishi wanaridhika kwa maandishi yale bila kwenda sehemu husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna migogoro ambayo inaendelea mpaka sasa, Jimbo la Kalambo kuna mauaji yametokea hivi karibuni. Migogoro hii iliyopo kwa Wafipa ilikuwa haipo sana kwa sasa ipo kati ya Wafipa na Wasukuma lakini shida siyo makabila, elimu mnaitoa kiasi gani? Mmegundua shida ya migogoro hii ni nini? Yawezekana mmekosa suluhisho kwa sababu hamjaja na njia ya kusuluhisha migogoro hii ila mnakuja na matamko ambayo hayana tija. Ni vema mkajua tatizo la migogoro ni nini na mkaja na suluhisho la kudumu siyo la muda mfupi kwa ajili ya kampeni, mkaja na suluhisho ambalo litaondoa migogoro kwenye nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la kuwapa ramani viongozi wa Serikali alilozungumzia hapa Mheshimiwa Waziri. Mkoa wa Rukwa nimeangalia hapa pesa zilizorudishwa kwao, kwenye kitabu cha hotuba, ukurasa wa 83 anasema marejesho, ile asilimia 30, Manispaa nzima ya Sumbawanga kiasi ambacho kimerejeshwa pale sijajua kama kinaendana na Manispaa, kuna shida kubwa sana hapa. Yawezekana ni mawasiliano mabovu kati ya Wizara yenyewe ya Ardhi na Manispaa husika. Kama siyo rushwa basi kuna shida kubwa sana kwenye Wizara au kwenye Manispaa pale pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanaowaweka kwenye Manispaa na Halmashauri zetu wamekuwa wakijitukuza kama Miungu watu ambapo wananchi wanapokuwa na shida wanashindwa kuwahudumia kwa uharaka, wanaangalia ni nani anasema, anasema nini, ana kiasi gani. Sasa nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama eneo ninalotoka mimi Kata ya Chanji, ni ya muda mrefu sana kwenye Manispaa ya Sumbawanga, iko katikati ya mji lakini Mheshimiwa Waziri akitazama maeneo yaliyopimwa atashangaa lakini property tax inakusanywa! Halafu baadaye ndiyo watakuja na hili la bomoabomoa, Sumbawanga haijafika lakini wananchi wako kwenye tension kubwa sana kwamba sijui mimi nitaondoka au nitabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ni vizuri elimu ikatolewa kwanza kwa watu hawa na elimu tunayoizungumzia ni bora wakapewa Wenyeviti wa Serikali au Vitongoji na Vijiji, wale ndiyo wako karibu na wananchi kuliko hawa mnaowapeleka. Hawa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vitongoji au Vijiji wataweza kueleweka vizuri na wananchi wao kwa sababu wanajua maeneo na wanajua ramani vizuri za maeneo hayo. Kama tutachukulia mambo haya juu juu hatutaweza kukomesha tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana Waziri ana nia njema lakini watendaji wake wa chini ndiyo wanaomwangusha lakini yawezekana na wao ni kwa sababu elimu hawana au yawezekana hawa watu ambao wanaweza wakafikisha ujumbe ni wachache kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, kuna haya mambo yanawezekana yanakurudisha nyuma kwa sababu aidha, watu kwenye Halmashauri ni wachache au hata waliopo hawatimizi wajibu wao. Kwa hiyo, ni vizuri katika haya anayotaka kuyafanya akagundua kitu gani kinakwamisha pengine ni bajeti anayopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefikia mahali nchi hii haitambui kwamba migogoro hii inapelekea kukosa amani katika nchi yetu, kwa sababu unapotokea mgogoro kati ya shule na wananchi unategemea ni nini kinaendelea? Siyo kwamba wale Walimu wanatambua maeneo yale wao wamekwenda pale kufundisha, lakini nani anayatambua yale maeneo? Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa haelewi ramani halisi ya pale ikoje. Sasa inapotokea migogoro kama hii nani alaumiwe Serikali, Halmashauri ya Mji au Manispaa ambayo inahusika na lile eneo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kabla hatujachukua hatua na migogoro mingine haijajitokeza, elimu itolewe kwa watu wetu na elimu hiyo tusi-base tu kwa watu ambao wako Wizarani, tu-base kwa watu ambao wako na wananchi wetu ambao ni Wenyeviti wa Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la asilimia 20 kwa Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa, yawezekana maeneo mengine wanapewa, Manispaa ya Sumbawanga kuna shida katika suala hili. Inafikia mahali Watendaji wa Kata wanasema wanaopaswa kukusanya ni mgambo, sheria inasema nini juu ya suala hili, ni akina nani wanaokusanya hii property tax? Sheria inasema nini, inawezekana ni mkanganyiko. Sasa Wenyeviti wanapata shida, wanakusanya pesa hizi kwa amani kabisa, wanapokwenda kule hawapewi, sasa shida nini Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana naona kwamba Waziri ana nia njema katika maelezo yake, lakini yawezekana watendaji wake ndiyo wanaokwamisha mambo anayotaka kufanya. Pia hata bajeti anayopewa haifanani na migogoro ambayo ipo kwenye nchi yetu, haifanani kabisa. Ndiyo maana muda mwingine tunaona kama kiini macho au kama story za miaka yote. Yawezekana ana kusudio jema, tunataka tuone haya mambo kwa vitendo na pale Waziri anapoona amezidiwa asisite kusema. Kazi yetu hapa siyo kumshangilia, tutamshangilia pale atakapofanya vizuri, lakini kama atakuja na haya mabegi aliyotupatia leo na documents nyingi halafu akashindwa kutimiza kile alichopanga, haitatusaidia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kusema ni kwamba, suala la rushwa kwenye Wizara hii ni kubwa sana. Yawezekana hata Waziri katika maeneo aliyokwenda ameliona lakini maeneo mengine akashindwa kuona kwa sababu sijajua kama anapewa ushirikiano wa kutosha. Huu ushirikiano ni lazima kuwepo na semina elekezi ili Mwenyekiti wa Serikali ajue wajibu wake, ajue anapata nini na anapaswa kufanya nini kwenye suala la ardhi, lakini ajue wananchi wake wanapaswa kutimiza wajibu gani kwenye kumiliki majengo yao au wanapokuwa wanataka umiliki wa ardhi. Mheshimiwa Waziri wananchi kwa sasa wanatamani maeneo yao yapimwe lakini anapokwenda pale mpaka aje apate hiyo hati ya kumiliki ardhi ni shida, tatizo ni nini, kuna shida gani hapa na bado inakuwa ghali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri hata hizi nyumba tunazosema za National Housing bei wanazotoa hazifanani na mazingira halisi ya maeneo husika. Huwezi ukauza nyumba kwa shilingi milioni 30, kwa Manispaa ya Sumbawanga, unategemea Mfipa anayepata gunia tatu kwa mwaka ataweza kununua hiyo nyumba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hizo nyumba zijengwe kulingana na mazingira halisi ya eneo husika. Kama ni Manispaa ya Sumbawanga waaangalie watu wa Manispaa ya Sumbawanga uwezo wao wa kipato ni kiasi gani. Wasichukue mazingira ya Dar es Salaam wakayapeleka Manispaa ya Sumbawanga haitawezekana. La sivyo hizo nyumba watakwenda kujenga kwa ajili ya wafanyabiashara lakini kusudio la zile nyumba ilikuwa ni watu wa hali ya chini waweze kupata nyumba za kuishi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri katika hilo, awatazame watu wa Sumbawanga kwa jicho lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu wa kumaliza hii migogoro, Mheshimiwa Waziri ana nia njema na ameonesha njia, napenda kushauri tena kuwe na ushirikishwaji. Manispaa ya Sumbawanga siyo lazima twendaemahakamani, sisi tunaheshimu sana mila na desturi, anaweza akaa na watu wa pande zote mbili wakamweleza shida ni nini badala ya kusubiri migogoro mpaka ifike mahakamani na watu kuuawa. Kwa hiyo, ushirikishwaji ni suala jema sana na litasaidia kumaliza migogoro hii. Yawezekana sheria zipo, lakini zimepwaya au usimamizi ni mbovu. Kwa hiyo, hata kama zitakuja hapa zikawekwa kwa staili nyingine, inawezekana ikawa ngumu kwenye utekelezaji.