Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Issaay, nilikuita lakini nilipoona haupo nikajua labda hukukaa kwenye kiti chako, basi endelea. (Kicheko)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, mic ilikuwa ina shida kidogo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nichukue nafasi hii kuungana na Watanzania wote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema nyingi katika nchi yetu, pia kwa baraka zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii tena kwa ufupi kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye hii Wizara na sekta ya elimu nchini. Amefanya kazi kubwa na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake; Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitazungumza maeneo machache. Eneo la kwanza ni la uboreshaji wa Vyuo vya Ufundi Stadi Nchini na ikiwepo Chuo cha Tango FDC kule Mbulu. Kwanza, naishukuru Serikali kwa sababu tayari walishakarabati zaidi ya nusu ya majengo. Chuo kile kilikuwa cha enzi ya ukoloni, sasa hivi maeneo mengi katika majengo yamekarabatiwa na mengine yanayohitajika yamejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitatu sasa bado viporo vya majengo havijakamilishwa, na niseme, katika bajeti hii kwa fedha zile zilizotengwa, tuone namna ya kukamilisha yale majengo. Pia, kwa kuwa sisi hatukupata fursa ya ujenzi wa Chuo cha VETA, tumeambiwa hivi Vyuo vya FDC vitakuwa VETA B. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, naishauri Serikali Tango FDC ni chuo cha zamani hapa nchini na bahati nzuri kina rasilimali ya ardhi. Mheshimiwa Waziri anisikilize, nilienda na Naibu Waziri tukafanya ziara. Nilipomshawishi tubadilishe, Marehemu Olenasha aliniambia tunakuja na “Tanzania ya Viwanda”, hatuwezi kubadilisha chuo hiki kuwa branch ya Chuo Kukuu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimwelewa wakati ule kwamba tunapokarabati, baadaye tutakuja kufanya maboresho. Pia tutaanzisha fani za kiufundi, kwa maana pengine kwenye sekta ya kilimo kwa sasa ina ekari karibu 400 ukitoa ya makazi ni ekari 200 za akiba zipo. Lakini katika mawazo yale ya awali ilikuwa tuwe na ranchi za ufugaji na pia tuwe na eneo lingine linalotumika kwa matumizi mbalimbali ya ufundi ikiwepo kwa maana ya ranchi za kilimo, pia demarcation ya kilimo kwa maana ya mashamba darasa pia na ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa hatujatumia hiyo rasilimali. Mheshimiwa Waziri, nadhani kama inawezekana, tunapoanzisha vyuo hivi vya VETA tukaacha zile FDC, bado hatujapata tija kamili katika eneo hilo kwa maana ya FDC kuleta tija nchini na malengo yaliyokusudiwa toka awali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakuomba, kama inawezekana, hawana trekta. Wana ekari 200, kilimo chenyewe hakina tija, ni kilimo kinachofanyika chini ya kiwango. Unaweza ukakuta pengine kwa ekari hawazalishi hata zile gunia 20 hadi 40.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna haja ya timu ya Mheshimiwa Waziri kufanya tathmini ya marejeo ya FDC nchi nzima ili kuona tija inayofanyika na mazoezi ya vitendo yanayofanyika kwenye vyuo hivyo nchini ili kuleta tija zaidi na namna ambavyo vijana hawa baadaye wataweza kutumia ujuzi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye eneo la elimu ya amali, naishukuru Serikali. Sasa hivi tunajenga shule ya amali kule Bunyoda, katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Jambo ambalo nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, ni kwamba, ujenzi huu wa shule ya amali tuangalie utaratibu unaowezekana wa kwamba tunajenga shule za amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie, je, wakati huu tunapojenga shule za amali kwa ajili ya ujuzi stadi pengine wa kutengeneza simu, kutengeneza vifaa mbalimbali na ujuzi wa mabomba na vitu kadhaa kama hivyo, hatuwezi kuwa tumekaa meza moja, yaani Wizara ya Elimu pamoja na Viwanda kwa maana ya SIDO, na pia Wizara nyingine mtambuka ili waje mezani kutambua namna ambavyo siyo kutengeneza tu vifaa kama ujuzi, na ubunifu unakuwepo wa kuwa na viwanda vidogo kupitia SIDO?
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo viwanda vidogo vitachochea kwa jinsi ambavyo malighafi zinakuwepo katika baadhi ya maeneo nchini ili walau vijana wanapojifunza na baadaye isiwe sisi ndio tunatengeneza simu kutoka nje, tunaunganisha umeme kwa kutegemea waya kutoka nje. Pia, kuna masuala kama mbegu na vitu gani ambapo kuna fursa kwenye maeneo hayo nchini, ili kwa pamoja Vyuo vya FDC (VETA), Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Elimu, na Wizara nyingine Mtambuka ili waje na mpango ambao unakuwa mwambata wa fani hizi mbili kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kupoteza muda, niendelee pia kuona mchango mkubwa ambao Waziri ameutoa katika Wizara hii kwa maboresho haya ya shule ya amali. Tunaona shule zinajengwa, lakini tunakuta kwenye yale maeneo ambayo pengine shule tayari zimeshaanza kupokea watoto, hatujaandaa kama ni karakana ama shule hii tumeiandaa kwa mtaala upi? Kama ni mtaala wa sayansi, ama ni mtaala wa kilimo, ama mtaala wa aina gani? Kama ni karakana na vitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani katika bajeti zetu zinazokuja kuanzia mwaka huu, tuanze kufikiri shule zile zinapata vifaa vya kujifunzia, kwa maana ya fani iliyokusudiwa pale ili tuweze kuleta tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kwamba, katika eneo hili la vyuo vikuu, vijana wengi bado hawajapata mikopo na wanakuwa na mdondoko kwa maana ya kuahirisha masomo. Nadhani kuna haja ya Serikali kutazama upya, vijana wangapi nchini kwa mwaka wameshindwa kuendelea na masomo baada ya changamoto hii ya ada, ili kuona ni namna gani hao wote ambao wamekosa namna ya kuendelea na masomo kwa ajili ya ukosefu wa ada, tunawatafutia dirisha lingine la kutambua matatizo yao na namna ya wao kurudi kwenda kusoma, kwa sababu haki ya kuwasomesha na wajibu wa kuwahudumia kwa ada tunao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, nendeni kwenye takwimu zetu mtaona idadi kubwa ya vijana wengi wameshindwa kuendelea na masomo kwa ajili ya ada, na kwa maana ya gharama ya vyuo vikuu. Ni kweli kuwa vijana wengi na hasa wale wananchi walioko kijijini, ama kwa taarifa zao kutokukaa vizuri ama kwa uwezo wetu mdogo wa Serikali, lakini kwa ujumla wao wameshindwa kuendelea na masomo. Hii sehemu itasaidia sana kutoa imani na pia kuleta ubunifu zaidi, lakini pia vijana hao kumaliza safari yao ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee tena kuangalia eneo hili la elimu maalum. Nawashukuru sana, Shule ya Msingi Endagikoti katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na maeneo mengine, mmefanikiwa kujenga mabweni ya watoto wa elimu maalum, lakini hatukuweza kuwapata walimu, hatukuweza kupata vifaa vya ufundishaji, na pia hatukuweza kupata pengine vifaa vingine pamoja na kuajiri watumishi wengine katika maeneo haya ya elimu maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wanafunzi wako bweni, lakini walimu wanalipwa pengine kwa kuchangia changia na wengine huwa hawapo, hivyo kukosa tija kwenye eneo hili la hao wanafunzi wa elimu maalum. Naomba kama inawezekana, kwa kuwa ninyi ni sera na wale upande wa elimu pengine ni TAMISEMI, lakini kwa namna ambavyo tayari tumejenga, Serikali ni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga mabweni, tuna wanafunzi zaidi ya 40, lakini unakuta walimu wa fani hiyo hawapo, lakini pia unakuta vifaa hatujaweza kutafuta na tukapeleka pamoja na vifaa vingine mbalimbali, lakini pia na watumishi wasio walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninafikiri kuna haja ya kutazama, je, tumejenga bweni?
(Hapa kengele ilila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Issaay, malizia.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, tumejenga bweni, je, tija inapatikana na hao vijana wanapata hiyo elimu? Kwa jinsi ambavyo tunaona, kazi kubwa imefanyika ni maboresho yanahitajika. Nawapa hongera Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashauri Wizara itazame vyuo vya FDC kama vina tija na kwa namna gani tunavyoweza kuleta maboresho zaidi katika fani mbalimbali ya kuweza kuwapatia vijana wetu ujuzi wa kujiajiri huko baadaye na kwa namna ambavyo tutafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)