Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chumbuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi hii leo angalau nami niwe miongoni mwa ambao wataweza kuchangia Wizara yetu hii ya Elimu, katika bajeti yake ya mwaka 2025/2026.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Profesa Mkenda, Naibu wake, na watendaji wake wakuu wote ambao wamekuwa ni msaada mkubwa kwao katika kuhakikisha wanayatekeleza yale ambayo watu wengi tumeyaishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nitakuwa na jambo moja au mawili, lakini sana nitakuwa na jambo moja. Nitajielekeza katika elimu ya vyuo vya amali ambayo ni sera mpya ambayo imeanzishwa kwa ubunifu wao hawa viongozi wetu, lakini nataka niipe nyama kidogo. Maagizo yao nayakubali hundred percent, lakini na maelekezo yao jinsi ambavyo wamekusudia kuifanya iwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwanzo, nachukua nafasi hii pia kuipongeza Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inaongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, zaidi katika kuhakikisha vile ambavyo vinapatikana kwa ajili ya kuinua elimu ndani ya Tanzania hii, lakini na sisi upande wa pili, basi vinatufikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwapongeze Wizara hii ya Elimu katika Mradi wao wa HEET. Mimi natokea Zanzibar Jimbo langu la Chumbuni lakini ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ndiyo maana nimesimama kuelezea Sera hii ya Elimu ya Juu ambayo na sisi inatuhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naipongeza Wizara hii ya Elimu kwa kuweza kugawa miradi ile ya HEET ambayo imekuja kwa nafasi kubwa sana Zanzibar na italeta ufanisi mkubwa ikimalizika. Kama haitoshi, pia kuja kwa hii HEET imetoa upanuzi wa kiuchumi na zaidi katika elimu, kiasi ambacho mpaka wenzetu wa UDSM sasa hivi nao wameamua kuja Zanzibar na kufungua tawi lao katika maeneo ya Buyu na tumewapa eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanaendelea na ujenzi na Inshallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watafanikiwa lile ambalo wanataka kulifanya, lakini na sisi kama Wazanzibar tutafaidika na uwepo wa Campus ile ndani ya Visiwa vyetu vile vya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Mheshimiwa Profesa Mkenda na QS Kipanga, lakini na timu yenu yote kwa kuweza kuyafanikisha haya. Tumekuwa tukipiga kelele sana, mimi mwenyewe nimekuwa nikimwuliza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa anakuwepo sana katika maswali, na nikitaka Mwongozo kwa hii miradi ya HEET, lakini namshukuru sana imeweza kuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 tumepata idhini ya dola milioni 21, kiasi ambacho siyo mchezo. Tunasema tunawashukuru sana, tunaipongeza sana Serikali hii inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije sehemu yangu ya pili ambayo nimekusudia. Sehemu yangu ya pili ni kuhusu hii Elimu ya Amali. Elimu ya Amali maana yake ni kuwafundisha wanafunzi ambao tunao kuhakikisha wanajifunza, wanapata skills za kujitegemea; which is sawa. Ni jambo zuri, lakini nataka niishauri Serikali sehemu moja au mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kuwa tuna maelezo mazuri katika makaratasi haya ya kuifundisha hii elimu yetu ya amali, lakini mpaka sasa hivi sina hakika kama tuna walimu wazuri ambao wanaweza kufundisha elimu ya amali kwa vitendo. Kwa sababu, elimu yetu hii ya amali maana yake ni elimu ya ufundi, yaani kwa Kiswahili cha haraka haraka, mambo mengi sana yanayopatikana ni ufundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivo, kwanza tunahitajika tuwe na walimu wenye knowledge ile ya kufundisha kwa vitendo, isipokuwa sasa hivi vyuo vya amali vipo vingi. Tunasema tunajenga vyuo 64 au 68 siyo haba, jambo siyo dogo, ni zuri, lakini je, tuna walimu hao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na walimu hao, jambo la pili tunatakiwa tuwe na maabara za kuwafanya watu waweze kusoma kwa vitendo. Elimu ya mafunzo ya amali eneo kubwa inasomeka kwa vitendo kuliko kwa nadharia. Walimu wengi ambao wapo katika hivi vyuo vya elimu ya amali, wengi wanakuwa na mafunzo yale ya nadharia, lakini siyo ya vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vinapatikana baada ya kuwa na walimu wenye knowledge ile na Serikali tukaamua kuweza kujitolea, kuhakikisha kabisa tuna mpango kazi wa kuhakikisha vyombo vinapatikana, maabara zinawekezwa, lakini na walimu wanapatiwa mafunzo ya kuhakikisha wanao uwezo wa kusomesha kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa nini ninasisitiza hii? Mwezi uliopita Serikali yetu ilipata; mnafahamu sasa hivi tuna ushirikiano na nchi hizi za UAE wakataka watu ambao wanaweza kuendesha magari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kama mmeangalia wiki iliyopita tu, Qatar walitaka watu 75. Kufika kule yale magari yote digital na waliochukuliwa hapa wamefanyiwa mtihani (vetting), wote wamesoma NIT, lakini karibu watu wote waliosoma wamesoma NIT wanafundishwa zile gia za hapa. Siku hizi kuna gari digital.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamefika kule, na mnajua Waarabu wenzetu wananunua gari ya mwaka huu. Wamefika kule wanakuta kuna magari ya digital. Walikuwa 75, walio-pass watano, 70 wamerudi. Hao watano siyo kwamba wameingia moja kwa moja kuendesha, wameingia kusomeshwa sasa zile gari za digital. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tusije tukawa na hii sera ambayo tunawasifu hapa muda wote, kila anayesimama, kwa ajili ya mafunzo ya amali, kwa sababu, mafunzo ya amali kwanza watu tukiwafundisha kuanzia sekondari na vyuo na ikiwa kuna vitu hivi, maana yake tayari tunawapa vijana ujuzi wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake nini sasa? Tukiwapa ujuzi wa kujitegemea maana yake hata ile mindset ambayo watu wengi wanajua, mimi nikisoma nikiwa na degree mbili lazima niajiriwe. Pia tangu yuko shule ameweza kupata ujuzi wa kutengeneza sabuni, mizinga ya nyuki na nini, au useremala, basi akimaliza hasubiri mpaka apate ajira rasmi ya Serikali au ya yale maeneo maalum. Atakwenda direct katika ile elimu ambayo ameipata shuleni wakati anasoma haya mafunzo ya amali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili pia nilikuwa nataka nilisisitize sana. Walimu kupewa uwezo, lakini na shule za amali ziwe na vitendea kazi ambavyo vitaweza kuifanya ile amali yenyewe iweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, napenda nichukue nafasi hii pia kukupongeza wewe Naibu Spika, jinsi ambavyo unatuongoza na hili suala letu la elimu nafikiri tunapata muda mzuri wa kuchangia bila wewe kutusumbua wala kengele. Nawashukuru sana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)