Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Joseph Zacharius Kamonga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Elimu. Nianze kwa kuishukuru sana Serikali na kuipongeza hususan Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya kwenye Sekta ya Elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda alitutembelea kule Ludewa kwenda kuangalia VETA ya Mkoa wa Njombe ambayo imeshakamilika na watoto wameanza. Kwa kweli niweze kuipongeza sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, namshukuru Mheshimiwa Prof. Mkenda, siku ile niliomwomba vifaa, fedha kwa ajili ya samani za ofisi, viti, meza na mambo mengine na nimechungulia huku ninaona kama ametenga fedha. Kwa hiyo, namshukuru sana na ninaishukuru sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa miaka hii mitano Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana kwenye elimu ya awali, elimu ya msingi, na elimu ya sekondari. Reforms nyingi sana zimefanyika na maboresho makubwa ya miundombinu yamefanyika kwenye elimu ya msingi, sekondari, na ile elimu ya awali, hasa eneo la sekondari. Kwa kweli kazi kubwa sana imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumza kwenye bajeti ya Waziri Mkuu na TAMISEMI na nikataja idadi ya shule ambazo Ludewa tumeweza kuzipata. Shule mpya za msingi mbili, shule za sekondari ambazo zimekamilika na kuanza nne, ikiwemo Shule ya Amali ya Mkoa wa Njombe, ambayo ni Njombe Technical School ambayo imejengwa pale Mlangali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tuna kila sababu ya kuishukuru sana Serikali na tuweze kumwahidi Mheshimiwa Rais kwamba, kule Ludewa yeye hatumdai isipokuwa anatudai sisi tuweze kumpigia kura nyingi ili miradi mingine iweze kuendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda sasa kujikita kwenye elimu ya vyuo vikuu. Kutokana na maboresho makubwa sana ambayo yamefanyika kwenye elimu ya awali, msingi, na sekondari, sasa tunatarajia hii fujo itahamia kwenye elimu ya juu. Kwa hiyo, naomba Serikali kwa kushirikiana na Tume ya Mipango, waanze sasa kuweka mikakati ya kufanya reforms kubwa sana kwenye elimu ya juu, hasa elimu ya diploma, cheti na vyuo vikuu. Maeneo haya nayo yaweze kuangaliwa, tuangalie sera tuboreshe tuweze kujilinganisha na wenzetu ngazi ya Kikanda na Ngazi ya Kimataifa, tuone kwamba je, tunaenda sawasawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo nashauri tuliangalie zaidi, kwanza ni miundombinu kwenye vyuo vikuu. Sasa, mtoto asije akaenda kwenye chuo kikuu akaona hamna mazingira yaliyobadilika kutoka kule alikotoka. Lazima vyuo vikuu viweze kuboreshewa sana miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Serikali imefanya kazi kubwa, lakini kutokana na reforms kubwa zaidi ambazo zimefanywa na Serikali na fedha nyingi zaidi zilizofanywa huku kwenye elimu ya awali, msingi, na sekondari, sasa tunatarajia huku juu sasa ndiyo fujo inakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, na kwenyewe tuanze kujipanga sasa kuviwezesha vyuo vikuu kuhakikisha kwamba vinaweka miundombinu yake vizuri ya kujifunzia na kufundishia. Vilevile, lazima tuangalie ile staffing, tuangalie wale professors, je, tuna Professors wa kutosha? Kama hakuna, basi tuwe na mikakati kwa kushirikiana na Tume ya Mipango kuhakikisha kwamba tunazalisha wanataaluma wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi kwenye vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuangalia hawa Professors wawe kwa kiwango cha kutosha, vilevile tuendelee kuangalia hata muda wa professors kustaafu. Nakumbuka kuna Mwalimu wetu mmoja hapo UDOM alikuwa anaitwa Kopoka, alistaafu akiwa bado ana uwezo mkubwa, ana nguvu, na alikuwa anaweza kuendelea kulisaidia Taifa letu, lakini unamlazimisha astaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tuangalie vizuri hili eneo kwa sababu kuna bidhaa nyingine inavyozidi kukaa ndiyo inazidi kuwa bora. Nafikiri hata divai ya Dodoma ikikaa muda mrefu inakuwa bora zaidi. Kwa hiyo, hata professors, yaani jinsi wanavyokuwa wametumika muda mrefu, ndiyo wanapata uzoefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwingine unakuta anachelewa kufikia hiyo ngazi ya kupata Uprofesa, halafu anatumikia kidogo anaambiwa astaafu. Kwa hiyo, tuendelee hapo, lakini vilevile tuwe na mikakati ya kupeleka hawa madaktari na wale wenye Masters kwenye masomo ya mbele zaidi ili tuweze kuwa na staffing ya kutosha kwa ajili ya vyuo vikuu vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie hata eneo la kuwezesha vyuo vikuu kifedha ili waweze kufanya tafiti nyingi zaidi, na zile tafiti zinaweza kuwa na manufaa pia kwa Serikali, wakashirikiana na Tume ya Mipango na Wizara mbalimbali. Hii itakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa. Kwa hiyo, siyo vibaya tukiendelea kusimamia ile asilimia fulani ya pato letu la Taifa (mapato ya nchi) iende kwenye maeneo ya tafiti na tuweze kushirikisha vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tuangalie hata maslahi ya hawa watumishi wa vyuo vikuu ili kusiwe na wengi wanaokimbilia nchi nyingine kwa ajili ya kwenda kufanya kazi kwa kutafuta mafao mazuri zaidi. Tunatamani kuona hawa wahadhiri, maprofesa, madaktari, watoke maeneo mengine warudi vyuoni kwenda kufundisha. Hili litawezekana tu iwapo Serikali itaongeza kulipa thamani eneo la taaluma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongea hapa Mheshimiwa Hasunga, amesema Sekta ya Elimu ndiyo inazalisha wataalamu kwa ajili ya sekta nyingine zote. Kwa hiyo, lazima tuangalie pia maslahi yao kuhakikisha kwamba watu wanatoka maeneo mengine na hawakimbii nchi yetu kwa ajili ya kwenda kufanya kazi maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, hata eneo la kusimamia maadili kwenye vyuo vikuu, kudhibiti rushwa, ili wale wanafunzi waweze kufundishwa kwa misingi ambayo inakubalika na waweze kupata elimu ile ambayo itawafanya wawe wabunifu, wawe na ujuzi wa kutosha, lakini siyo ile kufaulu kutokana na njia nyingine ambazo ni kinyume na maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni eneo la mikopo ya elimu ya juu. Naipongeza sana Serikali. Nilikuwa naangalia ukurasa wa 35 Mheshimiwa Waziri amezungumzia hapa kwamba, “ongezeko la mikopo ya elimu ya juu kufikia shilingi bilioni 787.4 mwaka 2024/2025, kutoka shilingi bilioni 570 mwaka 2021/2022”. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii kwa kweli ni mapinduzi makubwa sana, Serikali imeweza kuyafanya. Kwa hiyo, natoa pongezi nyingi na ninaipongeza pia kwa kuanzisha mikopo kwa wale wanaosoma ngazi ya cheti na diploma, hasa kwa kozi zile ambazo zina uhitaji mkubwa kwenye jamii na kwenye soko la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia wale watu wa Bodi ya Mikopo, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameongeza sana hizi fedha, vile vigezo vyao hasa vinavyowaondoa wale waliosoma shule binafsi kuanzia shule ya msingi na sekondari. Hii inaumiza watoto wengi ambao walipata ufadhili wa muda au walikuwa wana wazazi wenye uwezo, baadaye labda mzazi kafariki, sasa, wale wanaangalia historia badala ya kuangalia hali halisi ya mtoto wakati anaomba mkopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshuhudia hata kule Jimboni kwangu Ludewa, kuna watoto walikuwa wamesaidiwa na Ma-father (Mapadri) kwa ajili ya kwenda kusoma na walisoma shule binafsi, lakini baadaye wanavyokuja kuomba mikopo mfumo unawakataa. Kwa hiyo, naomba sana hili eneo tuweze kuliangalia vizuri ili watoto waweze kupata masomo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mbunge mwingine ameelezea hapa, Mheshimiwa Issaay, amezungumzia kwamba kuna watoto pia ambao wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo. Serikali ingeshirikiana na Wakuu wa Wilaya katika eneo hili kuweza kuwatambua wale watoto ambao walisoma kidogo na kukatisha masomo yao kutokana na kukosa mikopo au kupata asilimia ambazo hazikuwawezesha waweze kubaki masomoni wakati wote. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kamonga, kengele ilishalia mara ya pili, malizia. (Makofi)

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Vilevile, naomba miundombinu ya barabara kwenye shule za sekondari. Serikali iangalie checklist hasa maeneo ya pembezoni, kwa sababu TARURA wanasema siyo barabara zao, halmashauri mapato hafifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kule Mundindi, kupeleka mtoto akipata dharura inakuwa changamoto. Kwa hiyo, naomba Serikali ifanyie kazi na hili kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kupewa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia zote. (Makofi)