Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nampongeza Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda kwa kazi kubwa. Nampongeza pia Naibu Waziri, Omari Qs Kipanga; Katibu Mkuu, Dada yetu Profesa Carolyne Nombo; Naibu Katibu Mkuu na timu nzima kwa kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, na nifanye rejea ndogo ya hotuba yake ambayo aliiwasilisha hapa Bungeni Tarehe 22 Aprili, 2021 kuhusu mambo ya elimu. Naomba nisome, ninukuu, Mheshimiwa Rais alisema, “Serikali itajielekeza kufanya mapitio ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 na kufanya marekebisho kwa mitaala iliyopo ili ielekezwe kwenye kutoa elimu ujuzi. Tunataka mitaala yetu ijielekeze kwenye kutoa elimu ujuzi kulingana na mazingira ya nchi na soko la ajira.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameyaishi kwa vitendo. Hivi tunavyozungumza, tunao mtaala mpya ambao pia umeanza kazi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunayo sera mpya, Marekebisho ya Sera ya Mwaka 2023 ambayo pia yeye mwenyewe aliyazindua. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuishia hapo, sasa hivi tumejenga miundombinu ya shule. Tumejenga shule mpya za sekondari na msingi ili kukidhi mahitaji ya sera hii na kukidhi mahitaji ya mtaala huu. Hakuishia hapo pia, sasa hivi tunazungumza, na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema, zinajengwa shule za amali zaidi ya 103, shule 29 ni za uhandisi pamoja na shule moja iko Singida Mjini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa sana ambalo tulilizungumza na tumelizungumza kwa nguvu ni juu ya vitabu. Tumesikiliza na hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa kwamba, sasa uwiano utakuwa ni kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. Hili ni jambo ambalo hatukulitarajia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni mafanikio ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekujanayo na yamenifanya niweze kukumbuka na kufanya rejea ndogo ya mwanasiasa nguli, Margaret Hilda Thatcher aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke na ndio Waziri Mkuu aliyekaa kwa muda mrefu hapo Uingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Margaret Thatcher alisema, “If you want something said, ask a man, but if you want something done, ask a woman.” Kwa tafsiri yangu, ukitaka taarifa ya maneno mwulize mwanaume, lakini ukitaka taarifa ya vitendo mwulize mwanamke. Sifa hizi anazipata Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, Nelson Mandela naye alisema. Nelson Mandela aliamua kugusa kwenye eneo la elimu. Napenda pia ninukuu kwenye eneo lake ambalo Nelson Mandela amezungumza. “Education is the most powerful weapon which you can use to change the world.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hii ya ujuzi ambayo tumeianzisha, ndiyo elimu ambayo tunaitumia kama tool ya kuwafanya vijana waweze kujitegemea. Nataka niendelee kuipongeza Serikali, katika kipindi chote hiki ambacho sisi tulitaka kuwepo na mabadiliko ya elimu, iwe elimu ya ujuzi na imeweza kutekeleza jukumu hili. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kumpongeza Mheshimiwa Waziri. Nimesoma hotuba yake, nimesikiliza vizuri na nimeisoma randama vizuri, nimeona kwa kweli ameandaa hotuba nzuri na randama imeshiba. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo machache ambayo natamani kuishauri Serikali. Moja, ni uhaba wa walimu. Taarifa yetu inatueleza tunao uhaba wa walimu zaidi ya walimu 268,000, siyo jambo jepesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa karibuni tumeajiri walimu 14,000. Moja ya eneo ambalo nami lilinipa masikitiko makubwa, tumeenda kuwaajiri walimu kwa kuwapa mtihani, ambapo unampa mwalimu ambaye amesoma methodology. Mwalimu anapaswa apimwe darasani. Hawezi kupimwa kwa mtihani ambao anapewa ili apate marks hizo. Eneo hili kwa kweli hata mimi sikuwa nimelipenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali nini? Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Juni, 2023 walitoa mwongozo wa ajira ya kujitolea, kwa watu kujitolea, lakini mwongozo huu mpaka sasa haujatekelezeka. Kwa nini hautekelezeki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia baadhi ya maeneo, la kwanza ni mkataba ambao umewekwa wa mwalimu huyo anayejitolea anaingia mkataba na nani? Kwa sababu pale kwenye mwongozo inaonesha mkuu wa shule ama mwalimu mkuu. Pia, unaonesha Kamati ama bodi ya shule. Tayari unamweka mwalimu ana-hang, lakini anatakiwa alipwe posho na nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake tunasema, moja ya chanzo ni mapato ya ndani ya halmashauri. Chanzo kingine tumesema wazazi, na chanzo kingine ni wadau mbalimbali. Tukiliweka hivi, tutakuwa hatuna nia njema ya kuhakikisha walimu hawa wanaojitolea wanaweza kutusaidia na kupata hicho kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuishauri Serikali kwenye eneo hili. Mkataba unapaswa uingiwe na Mkurugenzi. Mwenye kutangaza ajira ya walimu kujitolea, anapaswa kutangaza Mkurugenzi kwani ndiye mwajiri wa watumishi na ndiye anayewasimamia walimu walioko huko wawe wanajitolea au hawajitolei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi ndio atangaze nafasi na ndio aingie mkataba. Ukiingia mkataba tayari unatoa fursa ya mapato ya ndani na sisi Baraza la Madiwani kujua katika bajeti yetu, tunao walimu kadhaa ambao wamejitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, rudi nenda ukarekebishe mwongozo huu wa walimu kujitolea. Msingi wa kufanya hivi, maana yake kundi hili la walimu walioko mtaani zaidi ya 200,000 wapate fursa ya kwenda kujitolea. Tupunguze hili gap la watumishi shuleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunataka kufanya hivyo? Hii itatusaidia. Leo tunayo PEPMIS ambayo inasaidia watumishi walioajiriwa. Mkurugenzi atatengeneza utaratibu wake wa kuwaingiza waliojitolea kwenye mfumo. Hii itawasaidia Wizara ya Utumishi, badala ya kuja kutoa mtihani kwa mwalimu ambaye ni professional, maana yake itakachofanya sasa ni kuangalia performance ya walimu waliojitolea kwenye shule na kuweza kuwaajiri kwa wepesi badala ya kutumia huu mfumo ambao tunautumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sasa hivi tumewekeza kwenye ufundi ambalo ni jambo jema sana. Nami nataka kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Tunajenga shule 103 za amali, VETA zaidi ya 64 na 65 kwa maana ya VETA ile ya Songwe. Pia, nimeona kazi ni nzuri, ametenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya VETA. Ni jambo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi fedha ni kwa ajili ya ufundi, uendeshaji na ni kwa ajili ya watumishi. Hili jambo ni zuri. Hata hivyo, ukifanya mchanganuo wa bajeti nzima kwenye hili eneo la ufundi ni asilimia 13 tu ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya uendeshaji wa vyuo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hii ni ndogo sana. Nataka kuiomba Serikali, kama kweli sisi tumeweka dira ya maendeleo yetu iwe kumwandaa kijana kuwa na ujuzi, ni lazima tuongeze fedha kwenye eneo hili ili liweze kutoa mwongozo, usaidie kupata walimu wa kutosha na tupate vifaa vya kutosha. Pia, fedha hii iliyopo ni lazima itoke kwa wakati. Shule zinajengwa, zinaisha, lakini mpaka sasa tunavyozungumza hakuna vifaa na hakuna walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi sasa mmeenda kule Mtwara mmeona kwamba sasa tuanzishe kile chuo kiwe chuo kikuu na watu waweze kusoma pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili ndiyo msingi wetu wa maendeleo. Tunataka vijana waingie darasani na waweze kupata ufundi. Sasa kama hatujajiandaa kuleta vifaa mapema, tutakuwa tumeshindwa kutekeleza wajibu huu kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, sijaona projection ya Serikali hapa ya tunakoelekea. Mwaka 2028 tutakuwa na vijana wa form one ambao wametoka darasa la sita na waliotoka darasa la saba. Mikondo yote miwili inaingia form one 2028. Sasa ikiingia form one mwaka 2028, ni yapi maandalizi ya Serikali ya kuongeza miundombinu ya madarasa na kuongeza watumishi? Yako wapi maandalizi hayo ya Serikali? Hatujayaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, projection inatakiwa ifanyike leo. Tukisubiri baadaye, tutarudi kama tulikotoka huko. Tunaanza kutumia nguvu kuanzisha madarasa na shule na matokeo yake tutashindwa kufikia malengo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, mwaka 2025 umeisha, huu tunaenda 2026 na mwaka unaofuata tuweke maandalizi mazuri ya 2028 tunawapokeaje hao watoto waliomaliza darasa la sita na waliomaliza darasa la saba wasije wakaenda kwa wingi halafu wakakuta bado tuna tatizo lile lile la walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tuna walimu zaidi ya 268,000 ambao wanatakiwa waingie. Ukifika huko inawezekana walimu wakafika zaidi ya 500,000 mpaka 700,000 hawawezi kufundishika na itakuwa tumetoa elimu ambayo haina msingi wa kuwasaidia hawa watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mradi, katika hii miradi yetu mikubwa; tuna Mradi wa BOOST, tuna Mradi wa SEQUIP na tuna Mradi wa EP4R (Lipa Kulingana na Matokeo). Miradi hii sehemu kubwa kwenye halmashauri imefanya vizuri, lakini zipo halmashauri ambazo miradi hii haijafanya vizuri na haijafanya vizuri kwa sababu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ina fedha nyingi, isipofanya vizuri, maana yake ni kwamba tunapoteza fedha nyingi za wafadhili na hii inatusaidia, kwa nini haijafanya vizuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mdondoko wa wanafunzi, wanafunzi ambao hawajamaliza shule. Ukichukua takwimu za 2023 – 2024, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaofika zaidi ya 500,000 hawajamaliza shule. Serikali inatakiwa ije ituambie ni nini sababu ya mdondoko wa wanafunzi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linatuweka kwenye wakati mgumu. Nataka kuiomba Serikali ihakikishe inatuambia mdondoko wa wanafunzi unasababishwa na nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia halmashauri zetu zitengeneze bajeti ambayo itahakikisha miundombinu ya shule na kujenga madarasa, itusaidie, ili kupata fedha hizi. Leo tumekosa fedha zaidi ya shilingi bilioni 124 kutoka kwa wafadhili, zingetusaidia ku-cover hili eneo. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha kipaza sauti, lakini nilikuwa nataka nimalizie. Bado nina dakika zangu kama mbili, tatu hivi za Mheshimiwa Rashid Shangazi, najua naye atachangia...
MWENYEKITI: Malizia sekunde zako.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo moja la mwisho ambalo ningependa niishauri Serikali ni kuhusiana na tulitembelea DAT. Hiki Chuo Kikuu kinatarajia mwakani 2026kurusha satellite. Moja ya eneo ambalo tulitaka kulijua sisi Wajumbe wa Kamati ni kwamba, tunarusha satellite ku-collect data gani? Wakasema wao wameshawasiliana na watu wa TAWA na nini? Maana yake ni kwamba wanataka ku-collect taarifa za wanyamapori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi changamoto yetu kubwa hapa ni eneo la kilimo na eneo la mazingira. Tunataka warushe satellite watupatie taarifa ya maeneo ambayo tutafanya kilimo chetu kiwe bora, na sisi tukaangalia eneo la mazingira. Tusirushe satellite kwenda kwenye eneo dogo linalohusiana na wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi