Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kutoa pongezi nyingi kwa hotuba nzuri ya Waziri wa Elimu, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wakurugenzi wote wa Taasisi ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukweli, safari hii kazi nzuri sana imefanyika, ninawapongeza kwa usimamizi wa kazi zote zilizofanywa katika taasisi. Uboreshaji na ujenzi umefanyika kama alivyosema Mheshimiwa Sima, na hasa maeneo ya vyuo vikuu, majengo mapya yamejengwa kwa ubora. VETA nazo zimejengwa ziko 64, lakini nawaomba sasa muiangalie ile VETA ya pale Mabwepande. Tulipoenda, niliona kama mwendelezo wake hauridhishi, labda mngeenda pale mwangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la mikopo. Safari hii wanafunzi wengi wamepata mikopo, malalamiko ya mikopo yamepungua. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa kuongeza fedha kwenye eneo la mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Taasisi hiyo ya NECTA kwenye mitihani, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, sisi tuko kwenye ile Kamati ya Elimu. Sasa hivi mitihani inatungwa kwa kufuata umahiri, hakuna tena yale maswali ambayo wengi wanafikiria yalikuwepo, yale ya kuchagua (multiple choice). Maswali yale yameondolewa, sasa hivi hata hesabu zinakwenda kwa kukokotoa. Kwa hiyo, hilo niwatoe wasiwasi ni kazi nzuri imefanyika kwenye NECTA. Sasa hivi mitihani inatungwa kwa kufuata umahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limefanyika, kwenye hii amali tunayokwenda sasa hivi, assessment (wanafunzi kutahiniwa) watakuwa wanafanya kama zamani, tulikuwa tunaita continuous assessment. Kwa hiyo, nafasi kubwa itachukuliwa kwa kazi anazozifanya mwanafunzi akiwa pale shuleni. Tofauti na zamani, mtihani wa kuandika unachukua 60%. Sasa hivi 60% ni kazi za kila siku, continuous assessment. Kwa hiyo, hiyo ndiyo itafanyika katika amali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa usambazaji wa vitabu. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Grace, kwamba, vitabu vimesambazwa kote. Kama alivyosema Mheshimiwa Sima, sasa hivi ratio ni kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu. Pia, TET iko katika mpango wa kuhakikisha kwamba, vitabu vitakwenda moja kwa moja katika shule, siyo tena kupitia kwenye halmashauri. Kwa hiyo, hizi taasisi sasa hivi zimejipanga vizuri na tumeiagiza TCU pia ichunguze na kuangalia wakati wote yanayotendeka katika vyuo vikuu yanafuata Taratibu au Miongozo ya Vyuo Vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye hii Sera mpya ya Elimu. Tunapoanzisha sera mpya au jambo lolote likiwa jipya ni lazima kunakuwa na changamoto. Ndiyo maana katika hii sera mpya, na hasa upande wa amali, tumeanza na shule chache, ili tuone tunakwenda namna gani? Kwa hiyo, shule chache zimeanza na kama nilivyosema, wakati mwingine haya mabadiliko huwa yanaleta changamoto ya uelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi kwa Wizara ya Elimu, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Jambo la msingi ni hii elimu ya amali haijaeleweka vizuri kwa jamii, na hasa kwa wazazi. Kwa hiyo, Wizara ya Elimu jambo la kufanya ni kuwaelimisha, amali italeta faida gani kwa vijana wakishamaliza form four? Serikali itumie vyombo vya Habari; television, kuelezea manufaa ya amali, mtoto akimaliza form four ataweza kujiajiri, ataweza kuajiri na kuajiriwa, ndiyo hiyo isemwe. Kwa hiyo, tukisema hivyo, wazazi na jamii itaelewa kwamba, hii amali inaanza, lakini pia ili kufanya tathmini, ni lazima tujipe muda. Wazazi wanauliza, hii ina faida gani? Au imefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo kwanza tumeanza. Kwa hiyo, ni lazima waeleweshwe kwamba, baada ya miaka miwili au mitatu ndiyo tunaweza kugundua kwamba, amali imetuletea faida gani? Kwa hiyo, ni vizuri mkashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, mjue kwamba, hii Sera ya Amali tukiifanya vizuri, hawa wanafunzi wakimaliza Kidato cha Nne, wataweza kupewa mikopo kwa sababu, tayari watakuwa na ujuzi na ni wafanyakazi. Kwa hiyo, tujipange kabisa, hawa watoto waweze kupata mikopo wakimaliza ile form four, kwa sababu, tayari hawa ni wajuzi na wanaweza kujitegemea. Pia tukiendelea na amali, uboreshaji utaendelea kwa sababu, wakati wote tunapotengeneza curriculum tunaifanyia uboreshaji au evaluation wakati inaendelea kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliseme leo kwa Mheshimiwa Waziri, ni kwamba baada ya miaka 30 watoto wetu watatucheka. Watatumia maneno ya ajabu sana kwamba, hivi Mheshimiwa Prof. Mkenda ndio alikuwa Waziri wa Elimu? Mheshimiwa Jenista ndio alikuwa Waziri wa Afya? Halafu wanahakikisha kwamba, vyuo hivi au vyuo vyetu vinavyoendesha elimu ya afya havina teaching hospitals! Watatushangaa na watatuita majina ya ajabu, watasema hii mijitu ilikaa inafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, haya mambo mawili yafuatiliwe yafike mwisho. Turudishe Teaching Hospitals kwenye vyuo vinavyohusika; MUHAS pamoja na UDOM. Kama hamwezi kurudisha kabisa, angalau 80% imilikiwe na chuo chenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Waziri ile proposal iliandikwa na Mheshimiwa Prof. Pallangyo, ambaye ndiye mwenye MUHAS wakati ule, sasa wao wamekaa hapo mpaka wananyang’anywa, wamekaa, kweli! Sasa hili walishugulikie kuhakikisha kwamba, hivi vyuo vinapewa Teaching Hospitals zake. Narudia hii ni mara ya tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe taarifa, Madaktari wote wazuri wa Tanzania wamesoma kwenye vyuo vyenye Teaching Hospitals; Norway, Sweden, Harvard, wamesoma huko. Mheshimiwa Prof. Mkenda analifahamu hilo.

MHE. BALOZI BASHIRU A. KAKURWA: Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, inatokea wapi? Mheshimiwa Balozi Bashiru.

TAARIFA

MHE. BALOZI BASHIRU A. KAKURWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji, na nilishawahi kumpa taarifa kwenye jambo hili hili. Suala hili liko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, suala hili kutotekelezwa ni kutotekelezwa kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Kwa kweli, wakati mwingine inasikitisha, yaani inashangaza, huo ni Mwongozo wa Kimataifa, lakini pia, kwenye Ilani ipo. Tunaona tabu gani sisi kutoa hizi Teaching Hospitals kuwaachia wale na walishazianzisha?

Mheshimiwa mwenyekiti, hebu ona sasa hivi Benjamin wanafanya vizuri kwa sababu, tayari kuna ushirikiano mzuri na UDOM. Tufanye hicho kitu kiishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka alimalize safari hii, nimezungumza kuhusu mafao ya Wakuu wa Vyuo na leo ninalizungumza kwa mara ya mwisho kwenye Bunge hili Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi. Atakapokuja hapo, naomba aniambie, kwa maana walisema liko Mezani, liko kwenye Meza, naomba aniambie limefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulisema, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Gwajima na Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua waliyoichukua mara moja waliposikia wanafunzi wa vyuo vikuu wamedhalilishwa na wale sijui niwaite nani wale? Wamechukua hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba Waziri na Taasisi zote, wale wanaojifanya wao ni mashuhuri sana, wanajifanya wao sijui ni mabalozi wa sehemu mbalimbali wa taasisi, mhakikishe kwamba, wanafukuzwa mara moja kwenye huo ubalozi, akiwemo huyo Mwijaku, watolewe huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mtu mashuhuri ufanye vitu vya maana, lakini unakuwa mashuhuri, unajiita mashuhuri, unafanya vitu vya ajabu! Waondolewe kwenye ubalozi, vijana wote au watu wote waofanya vitu vya ovyo katika jamii, waondolewe huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nimalizie, naomba sana shule zote zenye majina ya viongozi hebu tuzifuatilie.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Dakika moja nimalizie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufuatilie zile shule zenye majina ya viongozi, unakuta shule ina jina la Dkt. Thea Ntara sijui, lakini mimi sina shule; au jina la mtu yeyote mashuhuri au kiongozi wa Taifa, lakini tuangalie discipline ya hizo shule na elimu zao. Yaani ni namna gani wanafanya? Siyo unakuwa na jina kwenye shule, lakini ina-perform vibaya na nidhamu mbaya, ni aibu kwa Serikali. Kwa hiyo, nilitaka niliseme hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwa leo inatosha. Ahsante sana. (Makofi)