Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia hii Wizara muhimu katika mustakabali wa nchi hii. Nina mambo manne ya kuongea kabla sijachangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya malengo makuu matano ya Dira ya Taifa 2025 ni kuwa na jamii iliyoelimika na yenye uchu wa kujifunza. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Kagera alitupatia blank cheque, hundi ambayo haikujazwa tarakimu, akatuambia Wanakagera niwapatie nini mfurahi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipowauliza wananchi katika mambo matatu makubwa, ambayo Wanakagera waliyapa uzito, mojawapo ilikuwa ni ujenzi wa chuo kikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kama alivyosema Father Kamugisha, “anayeshukuru anakumbuka.” Tunakumbuka Kagera tulivyohangaika kupata chuo, lakini anayeshukuru anathamini. Tunathamini zawadi aliyotupatia Mheshimiwa Rais, tunathamini kazi mliyoifanya nyie wasaidizi wa Mheshimiwa Rais mkiongozwa na Profesa. Kipekee anayeshukuru anaomba tena. Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu wa zamani, unajua Wanakagera chuo kwao ni pamoja na ukubwa. Ukijenge kiwe kikubwa zaidi, uongeze majengo na faculties nyingi kusudi Wanakagera wapate chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la tatu, kwenye Hotuba ya Waziri amezungumzia Chuo cha VETA cha Ndolage, namshukuru ameniheshimisha. Tuliomba karakana; karakana tunayoiomba ni ya Food and Beverages Production, Food Science ya vitendo, na ya pili, tunaomba karakana ya upishi, mapambo na ulimbwende. Yaani dunia sasa hivi imeshakuwa dunia ya huduma. Hata mtu akifariki unakuta gharama ya mapambo inachukua fedha nyingi na gharama ya chakula. Sasa hiyo ndiyo sekta tunayotaka kuishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne, kwenye aya ya 90 na ile ya 95 ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ameeleza kuhusu kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali. Nakubaliana, lakini amesema Tanzania Educational Authority watawezesha upanuzi wa shule 55 za sekondari, ili ziweze kuwa Shule za Amali.
Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu, Wilaya ya Muleba, Jimbo la Muleba Kaskazini, tuna shule tatu zinazo-qualify. Sasa nakuomba uniwekee wepesi, shughuli ya mwaka huu unaijua, uchukue zote tatu au uchukue moja, nitakunong’oneza, uchukue zote tatu au moja iwe Shule ya Amali, iko kwenye Ibara ya 90 na 95.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango na Bajeti ya Wizara hii, naomba nitamke kwamba, naunga mkono hoja ya Waziri. Sasa ninaanza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie dhana ya Shule ya Ufundi na Amali, na Doctor aliyenitangulia amelizungumzia. Dhana ya Shule ya Ufundi na Amali, niwaelezee nikiwapeleka kwenye ufundi katika Shule za Kilimo. Ufundi siyo kuchomea, ufundi siyo useremala, ufundi ni pamoja na kujenga ujuzi na uthubutu. Mmezungumzia mambo ya Ifunda na Dar Tech kwamba, mnataka shule za namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali katika Shule za Amali tufikirie kuanzisha Shule za Kilimo; kilimo kwa mapana yake. Kwa mfano, ile iliyokuwa Kilosa, iliyokuwa Ruvu, iliyokuwa Kibiti na kidogo ilikuwa Nyakato Secondary. Tunataka mwanafunzi apelekwe pale, asisomeshwe masomo mengi, Kiingereza iwe ni lazima au Lugha na Hesabu. Yaani hesabu haiepukiki, mwenye macho haambiwi tazama. Hata Baba Mtakatifu aliyeteuliwa juzi, ana Degree ya Hesabu; Makamu Mwenyekiti Baba Askofu Mwijage, Msaidizi wake Vicar General ana Degree ya Hesabu na Civil Instructor Engineering.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uwafundishe hesabu hawa vijana halafu uwafundishe kilimo kwa ujumla, yaani kuanzia crops, aquaculture, floriculture, pisciculture, mechanical atomization, kusudi mtoto anaporudi akiwa na ujasiri na uthubutu anaweza akatumika katika hiyo field. Unapomwambia kwamba, ni animal husbandry, unapomwambia artificial insemination, unapomwambia resembling, unapomwambia embryo planting, mtoto wa darasa la 12 na 13 aweze kufanya hizo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie, nguvu ya kiushindani na kilinganishi ya hili Taifa iko kwenye Sekta ya Kilimo na hatutaikimbia. Hamwikimbii kwa miaka 40 ijayo. Dkt. Adesina alisema, billionaire anayekuja kesho yuko kwenye kilimo. Sasa sisi tunatoka kwenye kilimo tukakwenda wapi kwingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Akili Mnemba unaweza ukaitumia kwenye kuua wadudu shambani. Kwa hiyo, Mheshimiwa naomba, nitakuja kukushauri, tunataka hicho kilimo, nami nina faida katika Wilaya ya Muleba. Mkoa wa Kagera tuna eneo la kutosha, nusu ya land yote ya NARCO, ranch zote, zaidi ya nusu ziko Kagera, Ziwa Viktoria 30% iko Kagera, leta hiyo, nami nitakuwa mshauri, tuipeleke Kagera tuwaoneshe kwamba, hata kwenye kilimo, hata kwenye mifugo, hata kwenye uvuvi kuna ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kidogo kuhusu Bajeti ya Wizara. Mwanzoni nilipowaeleza kwamba, moja ya malengo ya dira ilikuwa ni kujenga jamii iliyoelimika na yenye uchu wa kujifunza. Ina maana ni uwekezaji katika Sekta ya Human Capital. Nimemsikia Mwenyekiti wa Kamati anazungumzia kutopatikana kwa pesa na mtiririko usioweza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiambia Serikali yangu Tukufu kwamba ni lazima tuwekeze fedha nyingi katika elimu. Katika vita ya biashara ya China na Marekani, China na Marekani Mchina amempiku Mmarekani kwa sababu ana jeshi kubwa lililoelimishwa, kuanzia fundi mchundo kuja fundi mwenyewe kwenda hata wenye Degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwekeze kikubwa, iwe kipaumbele. Huu ni mradi wa kimkakati. Unapozungumza elimu (education), unamaanisha mradi wa kimkakati utangulie, mengine yafuate. Huwezi kujenga uchumi imara, huwezi kujenga maendeleo ukiwa na watu ambao hawana elimu. Huwezi kuwa na amani, huwezi kuwa na mshikamano na upendo na watu wasiokuwa na elimu. Mtu ambaye hana elimu, uwezo wake wa kutafuta na kujiongezea kipato ni mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo nikinukuu taarifa za Kamati. Mwanangu, Mheshimiwa Mwenyekiti aliyoyasema ni kweli. Ni lazima fedha zipatikane kikiwa kipaumbele. Fikiria wewe mtunga sera, wewe mfanya maamuzi, kama mwanao asingekuwa na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie bodi ya elimu. Imezungumzwa kwamba tuna mahitaji ya walimu 268,000 ili tujiulize. Tujifungie tujiulize, kama tukiajiri walimu 268,000 nini kitatokea? Tuna walimu 268,000, na siyo ajabu tunao mtaani. Tukiamua kama Taifa kwamba tunakwenda kuwaajiri, tutakosa nini? Tukae kwenye vipaumbele vyetu, vingine tuache tuajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fikiria unapeleka mtoto kwenye shule ya kulipia, mtoto anarudi baada ya miaka minne anakwambia sikusoma hesabu, sikusoma biology, nilikuwa ninacheza, nilikuwa ninakula; anarudi amefura mashavu, haya amenenepa, lakini miaka yote hakupata walimu waliotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufanye maamuzi magumu kama Taifa. Call it a project, walimu 268 wote waende waajiriwe, tuangalie. Pesa zina tatizo, tunazitoa wapi? Kuna nchi moja sitaki kuisema, iliwahi kukopa World Bank kulipa mishahara ya walimu; lakini leo wanatesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye mkutano mmoja Vienna. Nilipohutubia, baada ya kuhutubia umati wote ukatikisika. Nikaona watoto wawili wanakuja kando yangu, walinisalimia kikwetu. Yaani wale watoto kwa kuniangalia, wakanisalimia kikwetu, kumbe nchi yao imewaandaa. Ma-ushers waliokwenda kwenye mikutano ya European Union, African Union ma-ushers wote wanatoka nchi ile, na anakuangalia sura. Yaani Kiingereza changu waliponiangalia wakasema hiki kinatoka mahali fulani. Akanifuata mtoto akazungumza kikwetu. Tunataka Watanzania wawe namna hiyo. Tutengeneze Watanzania wa namna hiyo waivamie dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi ninapoangalia, mnatengeneza madereva, yaani masharti ya dereva eti atapewa na chakula bure. Hiyo ni kazi kweli hiyo! Mtu eti tunatafuta madereva, utapewa kazi bure na Jumapili, na siku ya sikukuu au anafanya kazi siku zote. Ni lazima tuwekeze hapo, lakini suala la msingi kwa Serikali yangu, tukiajiri walimu 268,000 tutazimia? Kipi kitakwama? Is not a priority! Hili ni jeshi, ni jeshi la kuikomboa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora nizungumze hilo, nami hilo ndilo la kwenye bodi ya elimu. Bodi ya elimu tumeizungumza hapa, kama siyo Bunge la Kumi na la Kumi na Moja, ni copy from Zimbabwe. Zimbabwe wana bodi ya elimu, ukimaliza ualimu unapewa certificate na unafanya mtihani. Ngoja niwaambie; mbona kuna bodi ya uhasibu hatujalalamika! Mbona kuna bodi ya mainjinia hatujalalamika! Hupewi kazi bila kuwa na certificate ya bodi. Waende kwenye bodi. Tunaangalia upande mmoja, kuna walimu wengine ukikutana nao darasani unasema yala! hawa watoto tunaowaleta tunawalisha sumu siyo elimu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda shule moja nikaingia darasani nikamkuta mwanamama mmoja mwalimu amefunga dera, nikasema watoto wana kazi hapa. Unafunga dera darasani? Haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bodi ya elimu ni lazima, na tuna-copy Zimbabwe. Hatuvumbui jambo jipya, na bila bodi ya elimu hatufiki popote. Kwa sababu ya muda, nimeandika andiko zito, nitampa rafiki yangu wa siku nyingi kusudi liweze kuwaongoza.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa mara ya nne. (Makofi)