Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NG'WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi kwa kupata nafasi kuchangia katika Wizara yetu ya Elimu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara yote kwa ujumla kwa kazi kubwa na nzuri ambayo tumeifanya ndani ya muda huu wa miaka minne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu mapinduzi yaliyoshuhudiwa na sisi vijana na Watanzania kwa ujumla katika sekta hii ya elimu kwa miaka minne ni makubwa. Tunazungumzia ndani ya miaka minne ongezeko kubwa sana la bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kwa vijana. Pia tunazungumzia ongezeko kubwa sana la fedha ambalo limekwenda kuongeza wigo wa elimu bure kuishia kidato cha nne mpaka kidato cha sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea ongezeko kubwa sana la bajeti ambalo limekwenda kuongeza wigo wa mikopo kuishia katika vyuo vikuu peke yake, mpaka kwenye baadhi ya vyuo vya kati. Tunazungumzia kipindi ambacho mabinti waliokuwa wamekatisha elimu zao kwa sababu za kupata ujauzito, wamerudi shuleni sana, sasa wanaendelea na elimu zao. Ni kipindi ambacho tunazungumzia mabadiliko ya Sera ya Elimu ambayo yametuletea mabadiliko makubwa sana ya mitaala ambayo yamekuwa yanapigiwa kelele na Waheshimiwa Wabunge katika Bunge hili, lakini na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu pamoja na ukinara alioonyesha katika sekta nyingine, lakini amekuwa kinara mkubwa sana wa mabadiliko katika sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu leo utajikita katika mabadiliko au Sera mpya ya Elimu ya Mwaka 2023 na mabadiliko ya mitaala ambayo imekuja kutuongezea mtaala mpya wa elimu ya amali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo imekuwa inapigiwa kelele na walio wengi ni kwamba vijana wengi cha kwanza wanakosa ajira kwa sababu elimu wanayoipata katika mfumo wetu wa elimu haikidhi au haimpi kijana weledi wa kutosha kufanya kazi zinazotakiwa. Pia sekta binafsi zimekuwa zinazungumza kwamba vijana wanaotemwa na vyuo vyetu vikuu hawakidhi mahitaji ya soko la ajira lililopo nje. Leo hii majibu ya changamoto hizi, yapo katika mabadiliko haya ya mtaala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumzia elimu hii ya amali ni vizuri sana watu wakaelewa. Baba yetu wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kitabu alichoandika mwaka 1967 Education for Self-Reliance au Elimu ya Kujitegemea alizungumzia elimu ambayo leo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Mheshimiwa Waziri na Wizara yake ya Elimu ndio wameirudisha. Kwa hiyo, tukizungumzia kwamba Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anasimamia misingi ya Taifa hili tangu linapata uhuru, hiki ndicho tunachomaanisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hii ya amali inakwenda kumsaidia kijana anapoingia kuanzia form one mpaka form four, pamoja na kujifunza masomo yake ya darasani, lakini anakwenda kupewa ujuzi wa vitendo unaomsaidia. Hata akiishia form four, kwanza anapewa cheti chake cha elimu, lakini pia anapewa cheti au certificate ya ujuzi aliopokea. Kwa hiyo, kijana huyu anakuwa na uwezo wa kuchagua aidha aishie form four, anaweza kabisa kwenda kupambana na mazingira yake na kufanya kazi, lakini pia hata akienda chuoni haendi kuanzia kama kule ambapo anaanzia mtu mpya, anakwenda akiwa na cheti chake cha ujuzi. Aidha, Diploma au form five na six mpaka vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wanaanza kujifunza elimu ya vitendo kuanzia form one na elimu hii ya amali inaendana na mazingira husika. Kwetu sisi Mwanza watu wanafanya uvuvi. Maana yake ni kwamba kijana watashuariana sasa mwanafunzi na mzazi husika, kwamba apate ujuzi upi? Je, ajifunze uvuvi kuanzia form one mpaka form four? Maana huyu kijana akitoka hapo form four, hata akiingia ziwani kuvua hatalingana na yule ambaye hajasoma au hatalingana na yule ambaye amekwenda chuo cha VETA kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamaanisha tunakwenda kuzalisha vijana watakaokwenda kulikomboa Taifa hili. Tukizungumzia suala zima la mapinduzi ya viwanda, majibu yapo katika elimu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niipongeze sana Serikali kwa sababu majibu ya changamoto za Taifa hili, kwangu mimi ukiniuliza ninakwambia majibu yapo kwenye mtaala huu. Tutakapoanza kupata matokeo ya mtaala huu kuanzia mwaka 2027 wote tutarudi ndani ya nyumba hii tutakubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwaambie na kuwatia moyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Mheshimiwa Rais yote anayoyafanya washauri wakuu ni Bunge hili na ni ninyi Waheshimiwa Wabunge. Ninaamini kwa mabadiliko haya ambayo mmeyafanya, hii kazi mliyoifanya ni kwa ajili ya Watanzania wote, kwa ajili ya vizazi mnavyofuata, kwa ajili ya wote. Ninaamini wanaona kazi mliyoifanya na sina mashaka mwezi wa 11 tutakutana hapa kuapa tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hii ya amali pamoja na kwenda kutengeneza competence ya vijana wetu tunaokwenda kuwachukua na kuwaweka kwenye jamii zetu, tuangalie nchi mbalimbali ambazo leo hii zimeendelea. Mfumo huu Wizara yetu imeuchukua kwa kuu-pin point maeneo mbalimbali. Tumechukua elimu ya Ujerumani, tumechukua elimu ya India, tumechukua elimu ya China, tumechukua elimu ya Canada, tumechukua elimu ya Switzerland, zote tumezileta kupata mfumo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiongelea nchi kama China ambazo zina mapinduzi makubwa sana ya viwanda wanafanikiwa kwa sababu moja, kwamba vijana wao wana ujuzi wa muda mrefu wa vitendo wa kufanya kazi. Vitu vingi tunavyo-import hapa ni vitu ambavyo vimetengenezwa kwenye viwanda vidogo vidogo vinavyoendeshwa na vijana hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mataifa mengine ya wawekezaji wenye mitaji wanakwenda kuwekeza kwenye nchi hiyo wakiamini kwamba kuna teknolojia ya kutosha ya kuzalisha vitu hivyo. Kwa hiyo, siyo tu kwamba tunakwenda kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wetu, lakini tunakwenda kuifungua nchi yetu kwa uwekezaji mkubwa sana kwa sababu vijana watakuwa na uwezo wa kuzalisha kinachotakiwa, na vilevile tutakuwa na uwezo wa kupambana na mazingira yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyepo Njombe atafundishwa namna bora zaidi ya kulima miti. Aliyepo Geita atafundishwa namna bora zaidi ya kuwa mchimbaji madini, aliye na weledi mkubwa na wa muda mrefu. Kila kijana kwenye mazingira yake hata akiishia katika elimu yake, Taifa hili litakuwa limepunguza mzigo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, cha kwanza, pamoja na mtaala huu mzuri sasa tuliouweka, amekuwa akishauri Baba yangu Mheshimiwa Kishimba kwa muda mrefu kwamba mwanafunzi anayefundishwa na Profesa ni tofauti anayejifunza mtaani. Sasa kwenye hili tumelipatia majibu kwa sababu hawa vijana wanaenda kuanza kujifunza kwa vitendo kuanzia akiingia form one.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa, Serikali iangalie uwezekano, kuna watu ambao wameshakuwa wabobezi wa muda mrefu kwenye kazi hizi. Nitoe mfano mdogo, kwenye elimu yetu sisi ya Law School tunasoma darasani, lakini tukitoka kuna wale mawakili au wanasheria nguli waliokaa muda mrefu kwenye practice, wanakuja kutufundisha madarasani. Kwa utambuzi wangu, nchi hii ina wazalendo wengi sana. Tuangalie, kwenye hizi amali kama kuna uwezekano wa kupata watu walio-practise muda mrefu wakafundishe wanafunzi wetu, kwa sababu kuna tofauti ya kufundishwa elimu ya darasani na ile ya ujuzi kutoka kwa yule aliyefanya kwa muda mrefu, basi tufanye hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, pamoja na kwamba tumeweka mfumo huu wa amali, sasa ni wakati vyuo vyetu na vyuo vikuu vianze kujiwekea tathmini ya mitaala yao ili nao watengeneze mitaala yenye malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunavyozungumza hapa, ni ukweli usiopingika kwamba nchi hii haiwezi kuajiri vijana wote. Mataifa yaliyoendelea au yanayofikiria kwa muda mrefu yanatengeneza mazingira ya kuweza kuchukua watu wake na kuwapeleka kwa ajili kuajiriwa katika mazingira au nchi za watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo hii tunahitaji vyuo vyetu, kama ambavyo tumeanzia ngazi za chini kutengeneza mitaala ambayo unakwenda kumsaidia kijana, basi vyuo vyetu na vyenyewe viangalie upya programu zake, ziwe zina malengo international, ya kidunia, ili kijana anayetoka kusoma katika chuo chetu aweze kwenda kufanya kazi sehemu yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza hapa baba yangu Mheshimiwa Mwijage wakati anachangia kwamba, ni muhimu kwa vijana wetu, na kuna fahari ya kwenda nje ukakuta kwamba kuna Watanzania wengi wanafanya kazi kule kwa kuwa wana uelewa wa kutosha kutoka katika mifumo yetu ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri. Leo hii suala hili la bajeti limepigiwa kelele siyo na Waheshimiwa Wabunge peke yake, lakini na Watanzania kwa ujumla. Tulipiga sana kelele juu ya suala zima la mitaala, na sasa naipongeza Serikali kwa sababu imeongeza sana bajeti, kutoka shilingi trilioni 1.9 mwaka uliopita hadi 2.4 kwa mwaka huu. Ongezeko hili kubwa limekwenda kupelekwa moja kwa moja kwa sababu ya huu mtaala mpya. Yaani kwenda ku-fund huu mtaala mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme tu kwamba hii ni ajenda yetu ya Kitaifa. Tumepiga kelele kwa muda mrefu juu ya suala hili la elimu. Sasa limefika, tupo tayari kufunga mikanda kwenye vitu vingine ili tuweke fedha kwenye mtaala huu ili shule nyingi zaidi za amali ziweze kuongezwa na kwa wakati mfupi vijana wengi zaidi waendelee kupata elimu hii na kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya changamoto ya bajeti, sasa hivi tumeanzisha shule chache sana za amali, lakini mimi nafikiri tuendelee kuangalia namna ya kuongeza bajeti ili shule hizi ziwe nyingi na vijana wengi zaidi sasa waweze kupata elimu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)