Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Newala Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika sekta ya elimu. Tunampongeza sana kwa maono yake na malengo mazuri ambayo ameyaona katika kulisukuma Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri wake wa Elimu na wasaidizi wake wote kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais na kuwakwamua wananchi katika sekta hii ya elimu. Tunawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote katika haya mabadiliko ya mtaala mpya ambao umekuja mbele yetu. Mtaala huu ni mkombozi mkubwa. Niungane na wenzangu wote waliotangulia kusema kwamba ujuzi ndiyo njia pekee ambayo itatutoa katika hali hii tuliyonayo sasa hivi, ya kuhangaika na bahasha kwa vijana wetu. Wanamaliza ofisi miaka inapinduka, inakwenda kwa sababu elimu ambayo waliipata, wengi wao haikuwa na ujuzi ambao ungewawezesha kujiajiri wao wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala huu wa amali ambao tunaenda kuutekeleza sasa, nina uhakika kabisa kwamba wanafunzi watakapokuwa wamemaliza watakwenda kujiajiri wao wenyewe na Serikali itapunguza ule mzigo mkubwa wa kuhangaika kuwatafutia nafasi za kazi wahitimu ambao watatoka kwenye mfumo huu wa amali. Kwa hiyo, nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kile ambacho mlikifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wanamtwara ni wanufaika wakubwa wa mfumo huu mpya wa amali. Tunashukuru sana Serikali na tumeendelea kuishukuru kwa sababu wakati wa utekelezaji wa MEM, SEDP pamoja na PEDP 2002 sisi Wanamtwara tuna chuo chetu cha ualimu kawaida ambacho kilikuwa miongoni mwa vyuo vitatu ambavyo Serikali ili-repoint kwa ajili ya kuendeleza walimu wa sayansi ili warudi kule chini wakafundishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatukupata bahati hiyo tangu hapo, vikaenda chuo cha ualimu cha Dar es Salaam ambayo sasa ni DUCE na kule MUCE Iringa, Mkwawa lakini Mtwara kilibakia kwenye maandishi. Nashukuru juhudi za Serikali sasa hivi kitakuwa ni chuo ambacho na chenyewe kimechukuliwa, pamoja na kile Chuo cha Mtwara cha Ufundi ambacho sisi tunaita Mwasandube.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunashukuru sana kwamba vyuo hivi sasa vitatumika kwa ajili ya mafunzo ya amali. Ni kama Campus ya Chuo Kikuu cha Mbeya cha kufundishia watu kwa ajili ya mafunzo ya amali. Wanamtwara tunasema ahsante sana Serikali, kwa sababu siyo kwamba ujuzi tu ule ambao vijana wetu wataupata, kuwepo kwa vyuo hivi, Mtwara kawaida na Mtwara ufundi kama campus ya Chuo Kikuu cha Mbeya cha Ufundi ni kwamba itabadilisha mandhali ya Mtwara. Sura ya Mtwara itakuwa nzuri sasa kwa sababu uwekezaji mkubwa utafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wanamtwara watapata fursa nyingi kupitia uwepo wa vyuo hivi. Kwa hiyo, tunawashukuru sana, sana. Tunaishukuru sana Serikali kwamba Wanamtwara na sisi sasa tumeonwa. Uwepo wa vyuo vikuu vingi katika maeneo yale utachagiza wananchi wa kule nao kupata mwamko kwa sababu wanaona vyuo vikuu vipo pale. Kwa hiyo, itakuwa ni hamasa kubwa kwa wazazi kupeleka wanafunzi wao katika shule mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali, tuna furaha sana kwa hiki ambacho wamekifanya. Nashauri sasa, kwa sababu vyuo hivi ni vya muda mrefu, vimechoka, nashukuru kwamba bajeti kwa ajili ya maboresho ya vile vyuo imetengwa. Tumesoma kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri, lakini maboresho haya naomba sana Serikali isiishie tu kuboresha madarasa, iende pia hadi kwenye nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za watumishi ambazo zilikuwa zinatumika na wakufunzi wetu pale Mtwara TTC pamoja na Mtwara ufundi zimechoka. Naiomba Serikali kupitia bajeti yake ione namna ambavyo itaboresha mazingira mazuri kwa wale ambao watakuwa wanafanya kazi chuoni ili nao wapate sehemu nzuri ya kuishi ili wakafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na ninaishauri pia Serikali kwamba uwepo wa vyuo hivi ni kitu kigeni kule, basi redio za kijamii za kule zitumike kuelimisha wananchi kuhusiana na kitakachoendelea katika maeneo yao ili nao wapate uelewa wa mambo ambayo Serikali yao inayafanya katika maeneo yao. Pia, kwa kuwa ni vyuo vipya, na mafunzo yanayoenda kutolewa pia ni mapya, naomba basi karakana zote zinazotakiwa kwa ajili ya utoaji wa mafunzo haya zikajengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia hapa Mheshimiwa Mwijage anachangia kuhusu suala la elimu kupitia kilimo. Sisi tulikuwa na shule Ndanda, tulikuwa tunalima sana, kwa hiyo, hayo mazingira yawekwe kama ni watu wa kilimo, watafutiwe eneo ambalo wataenda kujifunza kulima, watakaoenda kwenye upishi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, miundombinu yote ambayo itawafanya wanafunzi kujifunza kwa ufasaha ikajengwe na kusimikwa katika maeneo haya ili wanafunzi watakaomaliza pale wawe wameiva, sio wanafunzi ambao walikuwa hawajaiva sawasawa. Waive ili waweze kwenda ku-implement vizuri kile ambacho watakuwa wamekisoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuongelea ni suala la uhaba wa walimu. Ili ufundishaji na ujifunzaji ufanyike vizuri, ni lazima walimu wawepo katika madarasa yetu. Kupitia taarifa ya TAMISEMI, 2024 imebainisha namna upungufu wa walimu ulivyo katika maeneo yetu Kitaifa, lakini pia hata ukienda kiwilaya. Kwa mfano, kwenye Shule za Awali kulingana na taarifa ya TAMISEMI 2024, Shule ya Awali walikuwa na mahitaji ya walimu 71,652, lakini waliyopo ni 16,559, upungufu ni 85.9%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Msingi mahitaji yalikuwa walimu 298,687 waliopo ni 124,826 upungufu ni 41.8%. Sekondari kadhalika. Matarajio ni kuwa na walimu 177,136 lakini waliopo ni 82,517 upungufu ni 46.5%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inasababisha wanafunzi kutopata vizuri masomo ambayo wameyaendea shuleni. Pia hali hii inaathiri utoaji wa elimu hata katika Jimbo la Newala Vijijini. Kwa mfano, ukienda Shule za Msingi za Jimbo la Newala Vijijini, Halmashauri ya Newala DC, mahitaji yalikuwa ni walimu 787, lakini waliopo ni 382 tu, sawa na 49%. Ukienda Sekondari, hali siyo nzuri kabisa. Tulihitaji walimu 482, lakini waliopo ni 185, asilimia ya upungufu ni 57. Tena ukienda kwenye masomo ya sayansi, tulihitaji walimu 203 wa sekondari; waliopo ni 81, upungufu ni 122.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii siyo tu kwamba inasababisha wakati mwingine hata ule mdondoko ambao umeoneshwa kwenye taarifa. Kuna mdondoko mkubwa. Wakati mwingine mdondoko unachagizwa na upungufu wa walimu, kwa sababu wanafunzi wanaenda shule wanatarajia wakutane na walimu, wapate elimu, lakini wanafika shuleni wanazunguka siku ya kwanza hawamwoni Mwalimu; siku ya pili, kesho, wanakata tamaa, wanakaa nyumbani, mdondoko unaanzia hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali, naungana na wote ambao wamesema tuwekeze katika kuajiri walimu, tukiwekeza katika kuajiri walimu wengi hata ile human capital tutaipata kwa sababu tutakuwa na wajuzi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwa sababu ya upungufu wa walimu, wazazi wanachangia kupata walimu wa kufundisha watoto wao. Kwa hiyo, tunawapa mzigo. Sawa, elimu inatakiwa kuchangiwa na kila mmoja wetu, lakini mzigo unazidi. Mzazi mwingine ana watoto wawili au watatu, anatakiwa achangie walimu kwa ajili ya ufundishaji wa Watoto, inakuwa ni kero kidogo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MAIMUNA S. MTANDA Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba suala hili Serikali iliangalie, nasi wananchi wa Newala DC tuangalieni tupate Walimu wa kutosha ili wanafunzi wetu watoke pale wakiwa wameiva na kwenda kulitumikia hili Taifa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni ombi. Kule nyuma kulikuwa na kitu kinaitwa Teaching Allowance kwa walimu. Walimu walikuwa wanafanya vizuri sana. Nafahamu ni suala la kibajeti, lakini sasa hivi Teaching Allowance imeondolewa kwa walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule pamoja na Waratibu Elimu Kata wanapata posho ya Madaraka, lakini pia tuwaangalie hawa walimu ambao wanaingia madarasani, mazingira yao siyo rafiki. Basi turudishe ile Teaching Allowance ili walimu wetu wapate moyo, iwe kama motisha kwao, wakapate kutufundishia watoto wetu vizuri. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele yako imelia zamani.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii, naunga mkono hoja. Pia naipongeza Wizara kwamba sasa hivi mafunzo kwa vitendo kwa walimu tarajali yamerudi miezi mitatu, hongereni Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)