Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie Wizara hii ya Elimu, Wizara muhimu sana ya Sayansi na teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na pongezi. Nakupongeza sana Mheshimiwa Profesa Mkenda na Wizara yake yote kwa kufanya kazi kubwa sana ya kuleta mageuzi ya Sera hii ya Elimu ili kuingiza Mtaala huu kwa Amali. Kabla ya hapo nieleze, mimi ni mfaidika wa elimu ya amali. Nimesoma Moshi Technical na baadaye Technical College.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nieleze kwamba kazi zote za kiufundi zinazofanyika hapa nchini zina mazao ya amali, kwamba aidha, walisoma Moshi Technical, Ifunda Technical, Mtwara Technical au Tanga Technical. Hawa ndio wanaoleta mageuzi katika sekta ya ujenzi, lakini ndiyo wanaoleta mageuzi katika sekta ya amali ambao wanafanya kazi za kujitegemea. Liko tatizo dogo ambalo nafikiri ni muhimu sana.
Mheshimiwa Profesa unisikilize. Tatizo kubwa neno, amali halieleweki, tutaanza kupata fundi wa amali. Halieleweki kabisa duniani kote, na hatutoki nje ya gurudumu hili, lazima kuwe na fundi mchundo, lazima kuwe na fundi sanifu na lazima kuwe na mhandisi. Elimu hii ya amali itoe hao watu watatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililotokea ni zuri sana. Sasa ndani ya bahasha hii ya amali kuna makundi hayo, lakini vyuo vyote viko tofauti. Wanaofundisha msingi wa kwanza kabisa wa ufundi yaani fundi mchundo ni VETA, lakini kulikuwa na mvurugano watu hawaelewi VETA inatoa mafundi gani? Pia wanaotoa wanafunzi au wataalamu wa Full Technician Certificate (FTC), hawa wanaitwa fundi sanifu, ni kutoka elimu ya sekondari ya amali halafu chuo cha ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeeleza itajenga vyuo vingi vya VETA, haiongelei vyuo vingi vya ufundi, tulikuwa na chuo kimoja tu cha ufundi (Technical College) pale Dar es Salaam ambacho sasa ni Chuo cha Elimu ya Juu, hakitoi lile kusudio lililokusudiwa la watu wa chini. Tatizo hili likiendelea tutawapoteza wananchi wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, waajiri wanapata taabu maana tutasema wametoka wanafunzi chuo cha ufundi, kumbe VETA; wanafunzi wametoka chuo cha ufundi, kumbe technical college. Kumbe anataka kuajiri fundi sanifu, yaani full technician certificate person, anataka kuajiri mtu wa VETA, mambo haya ni mazuri sana kuelezwa mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kuleta elimu ya kujitegemea, nami nina imani tulishakaa mara nyingi sana kuelezana suala hili, lakini nikisoma kwenye hizi taarifa zako, na leo nilikuwa napitia hii taarifa, wananchi wangu kijijini hawaelewi fundi amali ni nani? Waajiri wanataka kuajiri technician (fundi sanifu), waajiri kutoka wapi? Fundi amali! Wanataka kuajiri mtu wa kada ya chini, fundi bomba wa kuzibua bomba na kadhalika, fundi mchundo waajiri kutoka amali!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimefurahi sana, taarifa ya Mheshimiwa Waziri ni nzuri ya kujenga. Moja, kufufua chuo cha ufundi na pia kujenga vyuo vingine vya VETA. Ni sawa kwa sababu katika kila ujenzi mkubwa wa construction yoyote kutakuwa na Fundi Sanifu, Fundi Mchundo na Mhandisi, na hawa lazima watokane na elimu yetu ya amali. Kwa hiyo, amali hii itafsiriwe zaidi kuchambua watu hawa watatu. Tukifanya hivyo, tutakuwa na mafanikio makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nilitaka niongelee mambo mengine machache kuhusu ufanisi wa mafundi ambao tunafikiri kwamba watafanya kazi vizuri na mafunzo mazuri. Tulipoanza na nina-quote, Mheshimiwa Profesa Mkenda alisema kwamba, “Hatuwezi kwenda wakati mmoja pote paa, tukaenea. Tutaanza.” Ninavyoona anataka kuacha lile wazo lake zuri kwamba tuanze taratibu, anataka kuanza pamoja, haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa Moshi Technical, nikitembelea Ifunda Technical tulikuwa na sekta zote za ufundi; ufundi magari, ufundi machenical, electronic, ufundi umeme lakini ufundi wa ujenzi kwenye shule moja, na kulikuwa na karakana zote. Hatuwezi Vyuo vya VETA 200 low carder, lakini shule nyingine zile za amali zikawa na vifaa vyote hivyo, haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipange kwa Kanda. Kanda hii tuna shule kumi za amali, zina kila kitu ndani yake; Kanda hii ina shule kumi za amali, ukiingia ndani ya shule ile kuna karakana ya machenical, kuna karakana ya umeme, kuna karakana ya civil, kuna karakana ya electronics. Zimekamilika. La sivyo, tutaenda kutoa watu wa nadharia (theories), hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimeenda Moshi Technical zile karakana hazipo na ndiyo ilikuwa shule kubwa kabisa ya ufundi. Hakuna Lance Machines upande wa mechanical, upande wa umeme vitu havipo, lakini inaitwa shule ya ufundi. Hii tutapiga pancha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa alikuwa na wazo zuri kwamba bora tuanze, lakini nashauri sana, aoneshe kwa vitendo anaanza, siyo anaenea kila mahali, haiwezekani. Nami nakuamini na hata Mheshimiwa Rais hakutegemea atafanya makubwa namna hii. Bajeti yake inajenga shule 200, itapata wapi vifaa vya kujaza kwenye hizo shule? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, darasa moja la Shule ya Ufundi; Moshi Technical au Ifunda au Tanga, inagharimu bilioni za pesa, sasa 200 zitapatikana wapi? Kwa hiyo, nashauri arudi kwenye wazo lake la kwanza alipotushawishi Wabunge tumuunge mkono kwamba anaomba tuanze, aanze na shule chache za amali au shule za ufundi na neno la ufundi litumike sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, asiache kanuni kwamba ufundi lazima uanze kwa hatua, lakini watu pia wafafanuliwe mtoto wa VETA anapata nini? Mtoto wa form one mpaka Form Four Secondary School anapata nini? Anapokwenda Technical College anapata nini? Tukiweka vizuri haya, pongezi sana. Hongera sana Profesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naunga mkono sana hotuba yake, ahsante sana. (Makofi)