Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Rais wake wa Awamu ya Sita Mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kufanya maboresho makubwa sana katika sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba toka tumeingia humu ndani tatizo letu kubwa lilikuwa ni namna gani mitaala yetu inabadilishwa? Nilizungumza kwamba kule Mwanza kulikuwa na kongamano la vijana. Siku hiyo Waziri, Mheshimiwa Prof. Mkenda pamoja na Mheshimiwa Rais walikuwepo. Katika Kongamano la Vijana niliwaambia vijana someni mkitambua mnasoma ili mwelimike na mkielimika mjiajiri wenyewe. Hii ndiyo message niliyoipeleka mwaka 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka Waziri, Mheshimiwa Prof. Mkenda akaniambia umesema mambo makubwa sana yanatakiwa kufanyiwa kazi. Tuna vijana zaidi ya milioni 23 sasa hivi, na katika hao vijana milioni 23 na wao wanahitaji waje kuwa na maisha kama sisi baba zao, kama sisi wazazi wao, lakini ni lazima wafanye kazi ili waishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo moja ambalo linasumbua katika nchi yetu ilikuwa ni namna gani hawa wanafunzi wanaotoka katika vyuo vyetu wawe na uwezo wa kufanya kazi bila kutegemea kufanyishwa kazi. Kwa hiyo, yeye mwenyewe anajengeka kwamba natakiwa kuwajibika. Nifanye nini leo? Anapanga kazi zake za kufanya. Hawezi kupanga kazi zake za kufanya kama hajaandaliwa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaandaa hizi shule za elimu ya amali na biashara, lilikuwa kosa kubwa sana katika nchi yetu kuliacha hili somo la amali. Kama mtangulizi hapa alivyosema, hivi vyuo Tanga Technical, Moshi Technical, Arusha Technical, na Ifunda Technical, hizi sekondari zilikuwa zina maana kubwa sana. Wakati Baba wa Taifa anazianzisha katika nchi yetu, sasa tunaingia katika hii elimu ya amali kwa kasi kwamba tunaonesha tumechelewa na katika kuonesha tumechelewa tunatakiwa twende kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Waziri, mimi ninakuamini kabisa na katika maboresho makubwa haya unayoyafanya, tunakutana, tunazungumza na unatusikiliza, lakini inataka utusikilize katika angle moja hii ya kwanza. Ni kwamba hawa walimu wa hizi shule za amali na walimu wa shule za biashara, huu mtaala wa biashara ambao tunaoupeleka ni kwamba lazima upelekwe kwa shule zote, kuanzia shule za O-level na Advance, yaani uhakikishe walimu wa masomo ya biashara wapo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili hizi shule kwa ajili wa amali, je, umewaandaaje walimu wake? Ni kwamba lazima hawa walimu uwaandae, wapelekwe nje wakasome ili tuendane na hali inavyokuwa ya dunia. Hatuwezi kujifungia ndani hapa Tanzania tukaona kwamba tuna uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kama sasa hivi, tuna hizi treni za mwendokasi, hawa walimu huwezi ukawafundisha hapa. Niambie una chuo gani Tanzania cha kuwafundisha? Sasa ni lazima tuwapeleke watu wakasome halafu waje hapa kufundisha tupate madereva wengi wa kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupa mfano tu, leo kuna pump hizi za petrol station, sasa hivi hizi pump za petrol station niambie una chuo gani kinachotoa course za kuwafundisha mafundi wanaokwenda kuweka pump za petrol station, au kutengeneza hizi pump za petrol station? Hawapo. Watu wa vipimo hawana hawa mafundi, hao ma-technician hawapo, kwa sababu hatuna huo mtaala hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga majengo marefu, tunatakiwa tupate mafundi, ma-technician ambao watakuwa wanazi-run hizi lift. Unaweza ukakaa kwenye lift masaa mawili, wanatafuta mafundi. Unaweza ukakuta Mkoa mzima wa Dodoma fundi wa lift yupo mmoja tu. Sasa inaonesha kwamba tuko nyuma kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tupeleke mafundi wakasome nje. Mheshimiwa Waziri, hili najua kabisa liko ndani ya uwezo wako na tunavyopeleka hawa wataalamu warudi kuja kufanya kazi na mwaandalie malipo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kupeleka hawa tu peke yao bila Kitengo cha Mdhibiti Ubora. Huwezi kuwa na elimu ya amali bila kuwa na kitengo cha mdhibiti ubora. Hauko kwenye udhibiti ubora. Hawa wataalamu wakafundishwe kwa sababu huwezi kuweka Mdhibiti Ubora wa Wilaya ambaye anaenda kukagua hizi shule. zimekuja na mtaala mpya, wakati yeye haujui ule mtaala mpya. Hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Waratibu wetu wa Kata. Hawa Waratibu Elimu Kata ni lazima wapate mafunzo, huwezi kuwa na kitengo cha elimu ya amali unampeleka Mratibu wa Kata kule, yeye ni mwalimu, huyo mwalimu aliyepelekwa kule amesoma art na kule kwenye Kata yake kuna shule mbili za amali. Anaenda kufanya nini na amesoma masomo ya arts? Sasa kuna kazi kubwa sana. Kwa hiyo, haya ni mawazo ambayo nimeona nimshauri Waziri wa Elimu katika Kitengo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Mdhibiti Ubora. Hakuna mahali ambapo wadhibiti ubora wanaishi kimaskini na wako kwenye kitengo nyeti kabisa. Mdhibiti Ubora ni sawasawa na CAG wa elimu katika nchi yetu. CAG katika bajeti ya nchi anapewa siyo chini ya asilimia kumi au asilimia tano ya bajeti ya nchi ili aweze kufanya ukaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matokeo yake, mdhibiti ubora wetu, bajeti yako sasa hivi hapa 39% inategemea pesa kutoka nje. Haya, huyu Mdhibiti Ubora unakuja kumweka wapi? Unampa kwenye bajeti yako asilimia ngapi? Unaipeleka katika Kitengo cha Udhibiti Ubora? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la udhibiti ubora ni kwamba unavyobadilisha mitaala, na hawa watu wa udhibiti ubora lazima nao waingie kwenye mafunzo, na kule kwenye udhibiti ubora mwaandalie vifaa vya kufanyia kazi. Unakuta katika wilaya, mdhibiti ubora ana gari, lakini hilo gari lina miaka 15. Mdhibiti ubora atakwenda kukagua shule ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwenye jimbo langu tu nina shule karibu mia moja ishirini na kitu, lakini Mdhibiti Ubora gari halina tairi. Wewe Mbunge usipomnunulia Mdhibiti Ubora, basi inamaanisha kwamba hawezi kukagua shule, lakini lazima uje na makadirio kwamba Bwana Mdhibiti Ubora wa Kanda au wa Wilaya anatakiwa akague shule zote 120. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huku kwenye ukaguzi wa hizi shule, huwezi kufanya mabadiliko ya elimu katika nchi hii. Kama Mdhibiti Ubora hana vifaa, na wala hawezi kwenda kuzifikia hizo shule, akikagua shule Mdhibiti Ubora wa Wilaya atakagua shule zilizoko pale pale Makao Makuu ya Wilaya tu, lakini kumfanya aende kilomita 160 akakague shule, Mdhibiti Ubora atapata wapi bajeti ya kumpeleka kule?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikuta Mkurugenzi ambaye anakiona kile kitengo kiko kushoto, siyo cha kwake, hawezi kabisa kutoa bajeti yoyote kwenda kule kwa Mdhibiti Ubora. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati anakuja hapa kufanya majumuisho yake atueleze wadhibiti ubora anakujaje kukiimarisha hiki Kitengo cha Udhibiti Ubora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo nataka kushauri Mheshimiwa Waziri ni sehemu ndogo sana. Limezungumzwa hapa hili suala la walimu wa kujitolea na walimu kufanyiwa mitihani. Mimi ni mdau wa elimu, nilikwenda Ukerewe katika ziara zangu za kawaida nikamkuta Mwalimu anafundisha tuition ya English. Yule Mwalimu nikamuuliza unafanya kazi gani? Akasema anafanya kazi ya uvuvi, ni mkokozi tu hapa, nafanya kazi ya uvuvi naloa, basi napata riziki yangu, lakini ni Mwalimu wa English.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikampa na nauli aje Sengerema. Alipokuja Sengerema, kitengo changu mimi pale shuleni nikamwambia mfanyieni mtihani kama anaweza kufaulu huyu aje kama Mwalimu wa English hapa. Nimemkuta anafundisha wanafunzi Ukerewe. Baadaye naletewa matokeo naambiwa yule Mwalimu hana uwezo kabisa, tumempa mtihani amefeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu amepigwa jua kijijini, amekwenda kuloa, mtu analima bustani, mwalimu amesoma miaka mitano anatafuta kazi, unakuja kumpa mtihani wa form four. Nikawauliza, mmempa mtihani gani amefeli? Tumempa mtihani wa form four wa mwaka juzi. Nikawaambia haya ndiyo matatizo makubwa waliyonayo watu wetu. Nikasema aajiriwe hivyo hivyo. Baada ya miezi sita wananiambia bwana huyu Mwalimu ni bingwa, mwalimu ni mzuri sana, bahati nzuri amepata kazi nzuri Serikalini yuko Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hiki cha kuja kuwapa mitihani walimu ambao wamechomwa jua miaka mitano, miaka sita, miaka saba amekata tamaa bado unakuja unampa mtihani, basi tukifute hiki kitengo na hii kozi ya ualimu ifutwe katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna shida ya walimu kwenye maeneo yetu. Nchi nzima ina shida ya walimu, halafu unakuja kuwaajiri, unakwenda kuwafanyia mtihani. Ukamfanyie mtihani, anataka kufaulu aende wapi? Kwa sababu yeye ni Mwalimu, anatakiwa kuja kufundisha darasa la kwanza na darasa la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie tu jambo moja la msingi sana. Kuna vyuo vyetu vya ufundi na vyuo hivi ambavyo vilikuwa vya maendeleo ya jamii. Hivi vyuo vimetengwa katika wilaya. Hebu tujaribu kubadilisha sera yetu ya nchi. Ni kwamba hawa-appear mahali popote katika wilaya. Wewe Mbunge usipokumbuka kwamba kuna chuo kwenye wilaya yako, upite kwenda kumtembelea yule Mwalimu ha-appear halmashauri, siyo kwa Mkuu wa Wilaya, hebu angalieni sasa nao waanze kupeleka taarifa mwaweke karibu na halmashauri ili matatizo yao yaende katika halmashauri, yapite kule kwenye Kamati za Elimu, Afya na Maji ili nao kila quarter watoe taarifa zao na matatizo yao yaweze kujulikana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)