Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Kumba Ndulane

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu. Awali ya yote, nitangulie kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa ambao ameufanya katika Sekta hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tangu alipoingia madarakani mwezi Machi, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Kipanga kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusimamia miradi yote, lakini pia kusimamia mageuzi makubwa ambayo yamefanyika katika Wizara hii ya Elimu. Kwa kweli wamefanya kazi kubwa, wamefanya mapinduzi makubwa katika sekta hii ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu mingi tumeona imeboreshwa kwa kushirikiana na Wizara rafiki au iliyo jirani nao ya TAMISEMI tumeona shule nyingi zimejengwa, madarasa, vyuo vya kati vimejengwa vingi ikiwemo vyuo vya VETA, na sisi wana Kilwa kwa kweli tunashukuru kwa sababu ni miongoni mwa maeneo ambayo yamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Kilwa kuna shule tano ambazo zilikuwa shule shikizi. Kutokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanyika katika shule zetu za Namandugutungu, Kitope, Mbelenje pamoja na Masaninga sasa zimegeuka kuwa shule kamili za msingi na zimesajiliwa, sasa zinatoa elimu ya msingi, tunashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye miradi ya SEQUIP wameisimamia vizuri kwa kushirikiana na TAMISEMI kiasi kwamba tumeweza kujengewa shule tano katika Wilaya ya Kilwa. Kuna Shule ya Sekondari ya Ngome, Mavuji, Somanga, Namandugutungu na sasa tuko katika hatua za umaliziaji katika Shule ya Sekondari ya Mtekimwaga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunayo shule ya amali katika kata ya Rihimaliyao katika Kijiji cha Kisongo, iko katika hatua ya awali ya utekelezaji wa ule mradi. Kwa ujumla, SEQUIP plus, mradi huu wa Shule ya Amali tayari tumeshaletewa zaidi ya shilingi bilioni tatu. Kwa hiyo, yote hayo yanatufanya tuishukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa ambayo imefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumejengewa shule kamili kule Kinywanywa. Baada ya kuwa shule yetu iko katika hali mbaya, Serikali ililiona hilo tulipowasilisha hoja yetu kwao na ile shule imeshakamilika, na sasa inafundisha wanafunzi zaidi ya 300 pale, shule yenye equipments zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme, tuna chuo cha VETA, nasi ni miongoni mwa wanufaika wa vyuo 64 vya VETA vinavyojengwa hapa nchini. Progress yake ni nzuri, na kinaendelea kujengwa. Ni matumaini yetu katika msimu ujao wa masomo, basi kitaanza kudahili wanafunzi kwa ajili ya masomo ya ufundi stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru kwamba branch ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inajengwa pale Lindi Mjini. Ni matumaini yetu kwamba ndani ya muda mfupi ujao kitakamilika na tutaweza kupata manufaa ya kuwepo katika chuo kikuu cha kwanza katika Mkoa wetu wa Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunawapongeza, kwani mtaala mlivyoubadilisha unakwenda na wakati. Hivyo, nilikuwa na mambo yafuatayo ambayo nafikiri nikiishauri Serikali, basi yataweza kusaidia kuboresha zaidi sekta yetu ya elimu. Kwanza ningependa muendelee kuangalia namna ambavyo tutaboresha hii mitaala ili iwe bora zaidi na iendane na wakati na siyo tu kwa elimu ya msingi na sekondari, basi pia tuangalie hata kule kwenye elimu zetu za vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu kuna mambo ambayo yanahitajika, kwa mfano teknolojia na kadhalika. Teknolojia inabadilika kila siku, inahitaji kufundishwa katika hivyo vyuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la ajira. Kumekuwa na utitiri kila siku wa kuanzisha kozi mpya katika vyuo vyetu vikuu na baadhi ya kozi ambazo zinaanzishwa zinaonekana hazina tija kwenye soko la ajira. Vijana wengi wamekuwa wakihitimu, lakini mwisho wa siku wanaishia mtaani, ajira za kujiajiri hazipatikani, ajira za kuajiriwa na Serikali au taasisi binafsi hazipatikani, ajira za kuajiriwa na Serikali au taasisi binafsi hazipatikani kutokana na nature ya zile kozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningefikiri hapa Serikali ijaribu kuona kama inaweza ikaunda Tume ya kuchunguza hizi kozi zisiwe zinaundwa tu na vyuo bila kuzingatia mamlaka ya kiserikali na soko la ajira. Hii Tume ishirikiane na waajiri katika kubaini taaluma au kozi nzuri zinazoweza kutolewa ambazo zinaendana na ajira kulingana na mazingira tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ningeomba vyuo vyetu vya VETA uwekezaji uendelee ili yale matunda tuliyokuwa tunayakusudia ya vijana wetu kupata elimu ya ufundi stadi ikiwemo Wilaya yetu ya Kilwa pale Njianne basi vianze kazi mapema na hivyo viwe na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tuko katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa hivi vyuo, na hapa katikati vilisimama simama, basi Serikali iongeze msisitizo wa kupeleka fedha ikiwezekana msimu ujao wa masomo kozi zianze kutolewa, na zitolewe katika ubora na yale majengo ya hatua ya awali ambayo yanagarimu shilingi bilioni 3.8 yaweze kukamilika na nchi nzima kwa kweli tuweze kukombolewa katika hili eneo na vijana wetu kuweza kupata hizo taaluma za ufundi stadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tuone ajira zetu ambazo Serikali kwa miaka mfululizo imetoa, na hivi karibuni ilitangaza ajira 14,000. Tunaomba ajira ziendelee kutolewa, lakini katika eneo hili kwa sababu tuna malaki hapa, Mheshimiwa Mtanda alitoa takwimu za wilaya yake tu peke yake, nilikuwa nahesabu hapa, ana upungufu wa walimu wasiopungua 400, Kilwa tuna upungufu wa walimu wasiopungua 500. Kuna shule nyingine unakuta mwalimu ni mmoja anaweza akawa ni mwalimu wa arts au wa sayansi, sasa masomo mengine yale ya michepuo mingine sijui yanafundishwaje!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri katika eneo hili, tuangalie vilevile ukubwa wa tatizo ili tuone ni lini tutamaliza hii changamoto, kwa sababu shule zimefunguliwa nyingi za msingi maradufu, lakini pia zimefunguliwa shule za sekondari nyingi vyuo vya kati vingi, vyuo vikuu vingi, lakini kasi ya ajira haiendani na idadi ya ongezeko la wanafunzi sambamba na shule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba eneo hili liangaliwe, walimu waendelee kuajiriwa, na pia tuangalie maslahi ya walimu pamoja na wadhibiti ubora. Naishukuru Serikali kwa wadhibiti ubora ilisikia kilio ambacho mimi na baadhi ya Wabunge tulizungumza kwa miaka mitatu mfululizo. Wameweza kupewa ile posho ya Madaraka, wameanza kupewa, lakini imetolewa kwa ubaguzi baguzi hivi. Wanataka lazima uwe na sifa sijui ya Master’s ya Education, lakini tayari wameshapewa vyeo vile vya kuwa wadhibiti ubora wa wilaya, na wa mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningefikiri criteria iwe cheo alichotunukiwa. Kama ameshatunukiwa cheo, anastahili kupewa haki zake zote. Kwa hiyo, na wale walimu basi tuwaangalie nyumba, tuangalie na mazingira ya shule. Tumefungua shule mpya, zina vyoo vya kisasa, zina madarasa ya kisasa, lakini unakuta kuna baadhi ya maeneo hakuna maji. Huduma ya maji haipo. Tupeleke huduma kama hizo, tupeleke huduma kama za umeme ili hata wale wanafunzi ambao wanafundishwa TEHAMA waweze kujifunza kweli kweli, isiwe tu TEHAMA imeandikwa kwenye theory na kwenye mitaala yetu lakini practically haifanyiki. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)