Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi na nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema na kuweza kuijadili hoja hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa aliofanya katika sekta ya elimu, na pia kwa mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika sera hii ya elimu. Hakika tunampongeza na tunaona dhamira yake ya dhati ya kuweza kumkomboa mtoto wa Kitanzania kuhakikisha anapata elimu iliyokuwa bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kujenga vyuo vya VETA katika wilaya zangu zote za Singida, lakini changamoto kubwa iliyoko vyuo hivi, bado havijakamilika ujenzi wake. Kwa mfano, Wilaya ya Iramba tuna chuo chetu kizuri kinachoendelea kujengwa, lakini bado hakijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iweze kukamilisha chuo hiki kwa sababu mahitaji ni mkubwa sana. Hata hivyo, kiko chuo cha VETA Manyoni, nacho pia hakijakamilika. Naiomba Serikali iweze kuleta fedha za kutosha ili chuo hiki kikamilike kwa sababu kukamilika kwa chuo hiki ni mkombozi mkubwa sana kwa vijana wetu kujikomboa na kujiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa namna ambavyo wameendelea kusisitiza shule zetu za sekondari kusoma kwa njia ya TEHAMA, lakini changamoto kubwa ninayoiona katika shule hizi, kweli wameshaanza kusoma, lakini hakuna vifaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuja ku-wind hapa, atuambie ni mkakati upi ambao amejipanga kuhakikisha kwamba vifaa vya TEHAMA vinapatikana katika shule zetu za sekondari, lakini pia katika vyuo vyetu vya VETA?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia tathmini iweze kufanyika kwa vyuo vya VETA kwa sababu vyuo hivi vipo, vimejengwa vizuri, lakini vina uhaba mkubwa wa walimu, vitendea kazi katika karakana zetu yakiwepo magari. Kwa mfano, Chuo cha VETA cha Ikungi kina changamoto kubwa sana ya uhaba wa vifaa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri tupate vifaa katika chuo hiki, chuo ni kizuri, chuo kinapendeza, lakini hakina vitendea kazi katika karakana na walimu wa kutosha hakuna. Kwa hiyo, naomba suala hilo lichukuliwe kwa kipaumbele kikubwa. (Makofi)
Hapa, Naibu Spika (Mhe. Mussa A. Zungu) Alikalia Kiti
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulichangia, naomba Serikali ifanye tathmini ya vyuo vyote vya VETA nchini kwa maana ya ubora na mahitaji, kwa sababu kila Mbunge aliyesimama hapa amechangia uhaba wa walimu; kama siyo uhaba wa walimu, basi vitendea kazi. Kwa hiyo, maana ya uwepo wa vyuo hivi, ni vitendea kazi, walimu pamoja na ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulichangia ni walimu waweze kutengewa fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo kazini ili sasa tuendane na teknolojia iliyopo. Kwa sababu walimu wengi wanafundisha, lakini changamoto kubwa wanakuwa wanafundisha kutokana na jambo la kipindi cha zamani. Ninaamini kwamba endapo watapata fedha za kutosha kwa ajili ya mafunzo, wataweza kwenda kufundisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)