Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa, kwa dhati ya moyo wangu naomba nimpongeze Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa anayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona ni Wizara pekee ambayo imeleta reforms nyingi sana na ni kwa ajili ya maboresho na maisha ya Watanzania, hongereni sana. Ndiyo maana utaona kwamba katika malengo ya millennia Tanzania tulifanya vizuri sana katika lengo la pili, kwa sababu kila mtoto aliyezaliwa Tanzania alipata haki ya kusoma elimu ya msingi na tumefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakubaliana na watu kwamba Tanzania tunahitaji uwekezaji na bajeti ya kutosha katika Wizara ya Elimu. Kwa kuwa elimu, kusema ukweli ndiyo key factor katika kuleta mabadiliko, tunapambana na maadui watatu toka tumepata elimu, lakini tukiweza elimu vizuri, nafikiri ndiyo itakuwa rahisi kupambana na magonjwa na umaskini na mengineyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ni kuhusu shule za sekondari za kata na mchango wangu nauelekeza kuhusu ulazima au umuhimu wa sekondari za kata kuwa na mabweni au hosteli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo yenye jiografia ngumu kabisa, kwa mfano Manyara. Manyara ukiangalia wilaya za Kiteto, na Simanjiro, kuna watoto ambao bado wanatembea kilomita 10 – 15 wakienda shuleni. Wanaamka usiku maeneo yale pori kwa pori hatari ya Wanyama, mvua ikinyesha ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imekuwa ni sababu ya watoto kutokufanya vizuri kwenye ufaulu na imekuwa ni sababu kubwa ya dropout ya wanafunzi wengine kutokumaliza shule. Kuna maeneo mengine ambapo form four na form six wanabaki jioni kwa ajili ya kipindi wanachoita prep ili wa-discuss na wenzao, wanabaki mpaka saa nne usiku na imekuwa adha kwa wazazi kuwasubiria na kuwafuata wanafunzi hawa usiku, ukizingatia maeneo mengine usafiri wana namna hiyo hakuna, na hakuna anayeweza kumudu kuwalipia pikipiki kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naipongeza Serikali na waasisi waliokuwepo kufikiria kuwa na shule za kata. Hizi shule za kata imekuwa ni sababu ya watoto wa Tanzania kupata elimu ya sekondari. Pengine zisingekuwepo na wasingepata elimu ya sekondari, na kwa sasa hivi tunaona kwamba kata kwa zaidi ya 98% zina sekondari na nyingine zina sekondari moja mpaka nne. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri mchango wangu ni kwamba, tunahitaji quality ya elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatufikirii tena kuwa na madarasa mengi, na kuwe na shule nyingi. Sasa ili tuwe na quality na kuongeza ufaulu; naomba kabisa kwenye hizi za kata kuliko kuendelea kuongeza shule, sasa hivi twende kwenye kujenga mabweni (hostel). Kuna shule chache zimejenga hostel kwa ajili ya watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sahihi kabisa kum-protect mtoto wa kike kwa sababu madhara makubwa na mabaya yalikuwa yanabaki kwa mtoto wa kike. Kama ni mimba, whatsoever itaonekana kwa mtoto wa kike, hata kama ni ya mwanafunzi mwenzake au ni ya Mwalimu, lakini ukweli ni kwamba hata watoto wa kiume wanaharibika. Watoto wa kiume tunawategemea ndio Taifa la kesho, ndiyo wababa wa kesho na vichwa vya kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huku katikati watoto wanavuta bangi na kujifunza tabia nyingi mbaya. Kwa hiyo, tusibaki kusema kwamba hostel ni za watoto wa kike, wote wanastahili hostel. Naomba tu kabisa kwamba sasa hivi Tanzania tubadilishe mfumo wetu na maoni kuona tu kwamba ikishakuwa shule ya sekondari iwe hostel (bweni) ili watoto sasa twende kwenye exposure. Mtoto anasoma shule ya msingi hapo hapo, anakwenda sekondari, watu hao hao, anajifunza exposure ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bora sasa kama tuna hostel, mtoto wa wilaya moja anaweza kwenda wilaya nyingine, lakini kwenye shule hizi kuwe na maabara pia. Tunawashawishi watoto wetu wasome sayansi na sayansi ni vitendo. Hivi ni vitu gani kwa watoto wa Tanzania vinavyowavutia wasome sayansi?

Mheshimiwa Naibu Spika, maabara hamna, kuna vyumba vya madarasa vilivyobaki ndiyo tunasema hiki tutafanya maabara ya Physics, Chemistry na Biology. Wanasoma nini hakuna vifaa kule? Nafikiri sasa ni mabweni, tuongeze maabara, library na mabwalo ili sasa tuwe na elimu iliyo bora kwa wanafunzi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni juu ya shule za watoto wenye mahitaji maalum. Naipongeza sana Serikali kwa kujenga hizi shule za watoto wenye mahitaji maalum. Zamani ilikuwa tabia wazazi wanawaficha hawa watoto hawawezi kuwatoa. Sasa imeleta ahueni kubwa kwa sababu wanawapeleka hawa watoto kwenye hizi shule na ndiyo maana wanafunzi wanaosoma kwenye hizi shule za mahitaji maalum, shule ikifungwa wanalia kurudishwa nyumbani. Anajua akirudishwa nyumbani bado ataenda kufungiwa ndani ili mama aende kwenye ujasiriamali au shambani. Kwa hiyo, napongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba, wapatikane au waajiriwe walimu wenye uwezo mkubwa wanaoweza kukaa na hawa watoto kama walezi na walimu. Kingine ni hivi vifaa vya kuwasaidia hawa watoto. Wamechangia wenzangu kwamba hivi vifaa vinasambazwa na Serikali pamoja na taasisi zisizo za kiserikali, vipelekwe shuleni moja kwa moja. Pia, tumesikia gharama yake ni kubwa sana ndiyo maana tumeomba pengine unafuu wa kodi au kupewa ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na ushauri kwamba, tuna taasisi zetu za ndani; kuna KMTC, SIDO na CAMARTEC, hizi zina uwezo mkubwa sana wa kutengeneza hivi vifaa. Ndiyo maana tumeomba vitengenezwe hata vifaa vya hospitalini. Ni kwa nini tusijenge internal capacity tukawapa kazi hawa wakatengeneza hivi vifaa vya kuwasaidia watoto kusoma ili hata vijana wetu wanaomaliza shule za ufundi wapate ajira huku? Inakuwa demand driven, tunavihitaji hivi vitu na vijana wapate ajira na pengine vikapatikana kwa bei ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri sana, KMTC ni wabunifu wazuri na wana uwezo mkubwa sana wa kuvitengeneza hivi vitu. Tuwape kazi watutengenezee kuliko tunavyo-order vingi vinatoka nje kama China na kwingine, na ni kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine mchango wangu ni kuhusu vyuo vya kati na vyuo vikuu. Vyuo vya kati na vyuo vikuu kwa kweli vina uchakavu wa kutosha. Naipongeza Serikali, tumefanya ukarabati wa kutosha kwenye shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nyingine za msingi na shule shikizi, ukiziona utafikiri ndiyo chuo kikuu, maana ina madarasa mazuri, yana tiles, gypsum board na vingine, lakini ukienda vyuo vya kati vimechakaa. Hata njia ya kwenda kwenye hivyo vyuo huwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafikiri kwamba vile vyuo vina fedha zao za ndani za kuweza kukarabati, lakini vinazidiwa. Naomba Serikali iangalie hilo, iwasaidie. Nami kwa Mkoa wa Manyara, naomba Mheshimiwa Waziri atujengee chuo kikuu. Tulishatenga eneo la ujenzi wa chuo kikuu katika Wilaya ya Hanang, kwa hiyo, tunaomba sana, na Mkoa huo ni mpya uwe na chuo kikuu ili kwamba kwenye chart ya dunia watuone tu kwamba tunafanya vizuri, nami napendekeza kiwe chuo cha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kuhusu kasi ya kuweka vyuo au shule za amali. Kusema ukweli kutokana na changamoto kubwa ya ajira ya vijana wetu tuliyonayo, mtazamo wa kuanzisha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)