Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hanang'
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwanza kwa kuweka msukumo mkubwa kwenye mapitio ya mitaala yetu ili mitaala iboreshwe iweze kuendana na hali halisi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Samia Scholarship ambapo vijana waliofanya vizuri wanapata scholarship ya Mheshimiwa Rais, wanasoma bure na tunapata wataalamu. Vilevile, nampongeza kwa kuanzisha Samia Innovation Fund ambayo itatoa mikopo ya riba nafuu kwa watafiti ambao watazibiasharisha bidhaa zao ambazo zimetokana na utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Prof. Mkenda; Naibu Waziri, Mheshimiwa Kipanga; na Katibu Mkuu, Prof. Nombo, kwa kusimamia maono mapana ya Mheshimiwa Rais katika kuimarisha elimu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashukuru, niliomba sana kujengewa VETA pale kwangu Hanang, ujenzi umeanza. Pia, Mheshimiwa Waziri anakumbuka nilikwenda kwake nikilia kwamba idara ya ukaguzi haina usafiri (gari) na alinipatia lile gari. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache ya kushauri. Tumekuwa na hili suala la mitaala. Jana baadhi ya Wabunge walikuwa wakilalamika kwamba masomo gani watu wasome na masomo gani yasisomwe. Nafikiri yote haya tunahangaika na tuna watoto wengi ambao wamesoma na vijana wapo mtaani hawana ajira, na ukiitisha tu nafasi kwa sasa hivi maelfu kwa maelfu ya watu wanajitokeza kwa sababu hawana kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri sasa ni wakati mwafaka kozi zetu tunazozifundisha na aina ya elimu tunayoitoa tuangalie mahitaji ya nchi, siyo tunatoa tu elimu. Tunao walimu wengi mtaani: wa Historia, na wa Jiografia ambapo wenye degree sasa wanapelekwa shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeandaa walimu, lakini hawana nafasi ya kuajiriwa. Hebu tuangalie kweli zile kozi tunazozitoa, vyuo vinachukua ada, sawa, wanajitengenezea kipato. Hao vijana tunaowapa elimu, wana sehemu ya kwenda kufanya kazi? Nafikiri hilo tuna sababu ya kuliangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuwaelimishe Watanzania, tunapowaambia kutafuta taaluma au kutafuta knowledge tunamaanisha nini? Ili hatimaye kila mtu kwenye ndoto yake ndiyo atafute taaluma. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa sababu sasa tumeanza kuwekeza zaidi kwenye elimu ya ufundi na elimu ya amali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa ya watoto wetu kuacha shule. Amechangia Mheshimiwa Rahhi hapa sasa, kwamba kikubwa ambacho kinahitajika kwa sasa kwa shule tulizonazo, tujenge mabweni kwa sababu kinachowafanya watoto waache shule ni mazingira magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengine wanatembea zaidi ya kilometa 18 kuifuata shule. Akihangaika hivyo mpaka aweze kutoboa, mwisho ataacha shule katikati. Watoto wa kike watapata ujauzito kwa sababu ya mazingira magumu na wengine wamepangisha geto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumejenga shule, tuangalie namna ambavyo tunaweza kuboresha mazingira ya watoto wetu kujifunza na mazingira ya watoto kusoma. Kingine badala ya kujenga shule, inawezekana maeneo mengine tunafikiria kujenga shule mbili za kata. Tuangalie namna ya kuchanganya zile shule. Maeneo ya watoto ambao wanatoka mbali tuhakikishe angalau wanapata mabweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo kata sasa hivi unakuta kata moja inakimbilia kujenga shule tatu. Tuna changamoto ya walimu kukidhi mahitaji ya walimu kwa shule nyingi, hivyo ni ngumu. Kwa hiyo, ili angalau kuziba tofauti hiyo ya mahitaji ya walimu kwa kila shule ambayo inajitokeza, kwa sababu tukijenga shule nyingi tutahitaji walimu zaidi badala yake tuangalie namna ya kuboresha miundombinu iliyopo na namna ya kuwaweka watoto vizuri ili kuhakikisha kwamba wanasoma na wanapata elimu kwenye mazingira ambayo ni mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la elimu ya vyuo vikuu hasa kwenye eneo la mikopo. Wanafunzi wengi wa vijijini wana changamoto ya kupata mikopo ya elimu ya juu. Hii inatokana na utaratibu ambao tumejiwekea kwamba mtoto akisoma shule za binafsi, nafasi ya kukopeshwa inapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazazi wengi kwa mazingira ya elimu ilivyo sasa anapambana wakati mwingine wazazi wanauza mashamba kuhakikisha angalau mtoto wake anafaulu kwenye elimu za sekondari aweze kuingia chuo kikuu. Anapofika chuo kikuu, vigezo ambavyo vinaangaliwa vinawaacha watoto ambao wazazi wao wamehangaika kuhakikisha kwamba wanasoma kwa kuuza rasilimali za familia.
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto hao sasa vigezo vinawatoa kwa sababu wao wamesoma shule binafsi. Hili eneo naomba liangaliwe kwa sababu anayeomba mkopo kama inawezekana akopeshwe na mazingira ambapo watoto hawa wamepita tuyaangalie.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao watoto wengi wanakuja kwa Wabunge kwamba, “nimeomba mkopo nimekosa”. Pia, wako watoto ambao wamebaki nyumbani kwa sababu ya kukosa ada ya kulipa chuo kikuu. Tuangalie eneo hili tuweze kuliboresha. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa kuongeza fedha za kuwakopesha watoto wetu, lakini sasa vile vigezo tuviangalie. Kuna wengine wanakwama kwa sababu ya mazingira ambayo walipitia kabla ya kuomba mkopo wa chuo kikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nimejaribu kuangalia ni eneo la utafiti. Kitu kikubwa ambacho nilikuwa naangalia, ni kwamba kuna fedha kiasi gani kwenye eneo hilo. Nchi yetu ili tuweze kujitegemea na ili tuwe na teknolojia ambazo watu wetu watazipenda ni lazima ziwe zimetafitiwa na hatimaye ile finishing ya products zetu ziwavutie wanunuzi wa hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufikia huko, ni lazima tuweke fedha. Nimeangalia kwenye eneo hili la utafiti, fedha pekee niliyoona ni Samia Innovation Fund shilingi bilioni 2.3. Hizi ni fedha kidogo. Tukitaka kulitengeneza Taifa letu na tukitaka kuendeleza eneo la utafiti, hii itatufanya maprofesa wetu wahangaike kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili waweze kuendesha maisha yao badala ya kubaki maabara, wafanye utafiti na hatimaye waweze kuja na teknolojia mbalimbali zitakazosaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, niseme naunga mkono hoja ili Mheshimiwa Prof. Mkenda akapambane na akaboreshe elimu yetu, ahakikishe kwamba elimu ya Watanzania inaendana na mazingira yao. Ahsante sana. (Makofi)