Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze kuwapongeza Mawaziri pamoja na Katibu Mkuu Profesa Carolyne pamoja na Mheshimiwa Profesa Mkenda na Naibu Waziri, Mheshimiwa Kipanga kwa kazi ambayo wanaendelea kuifanya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati na tumekuwa tunafanya nao kazi wakati wote na tunaona willingness yao kuhakikisha kwamba tunasogea katika upande wa elimu, tunafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia watumishi/watendaji wa Wizara tumekuwa nao kwenye kazi kipindi chote hiki tangu hii Kamati mpya, kwa sababu hii ni Kamati mpya, sasa hivi inashughulika na masuala ya elimu zaidi. Kwa hiyo, tumejadili mambo mengi kwa kina. Kuna mambo mengine ambayo wakati mwanzo haikuwepo hii Kamati, maana yake kuna vitu tulikuwa hatuvijui, lakini tangu imekuwepo, tumechakata mambo mengi sana kwa ukaribu, na kwa kina kwa muda wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia maeneo machache sana. Waheshimiwa Wabunge wamechangia, nami pia naunga mkono maoni na mapendekezo ya Kamati kuhusiana na mambo kadhaa ambayo tumeyajadili. Yote ni sisi tumejadili na tumekubaliana kama Kamati kwa niaba ya Bunge, lakini mimi nitachangia upande wa ubora wa elimu kwa sababu katika vile vipaumbele, Serikali imeweka kipaumbele cha kuboresha elimu ya awali, msingi na sekondari pamoja na upande wa amali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukizungumza ubora wa elimu, kuna vitu vingi ambavyo tunaviangalia na kwa sababu hii ndiyo bajeti ya mwisho kwa miaka hii mitano tangu tumeanza kujadili nitaomba niongee mambo kadhaa. Jambo la kwanza, tunapoizungumzia Tanzania, tunazungumza mambo matano ya msingi. Tunazungumza maeneo matano ya kisekta ya msingi ambapo mengine yanaingia humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiizungumzia Tanzania, sekta ya kwanza, tunazungumzia kilimo; tukiizungumzia Tanzania tunazungumzia logistics; tukiizungumzia Tanzania tunazungumzia extractive industry (sekta ya uziduaji); na pia tukiizungumzia Tanzania tunazungumzia utalii, vilevile tukiizungumzia Tanzania tunazungumzia trade and industry (viwanda na biashara); na tukiizungumzia Tanzania kitu kingine ambacho kina-cut across hizo sekta zote ni human capital development (maendeleo ya watu).

Mheshimiwa Naibu Spika, walipata kuandika waandishi wa vitabu mahiri duniani wakieleza kwamba maendeleo ya nchi yoyote duniani ni lazima yawe people centred development (maendeleo ambayo yanafungamanishwa na watu). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiizungumzia human capital development unazungumzia elimu, afya na sekta nyingine. Hata hivyo, elimu kwa upekee wake, hizi sekta zote nilizozizungumza ambazo ndiyo ukiizungumza Tanzania unazizungumza, hizi sekta zote zinategemea kuwa informed na mfumo wa elimu kwenye nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huwezi kuzungumza sekta ya utalii kama unataka kuifanya vizuri bila kuwekeza kwenye elimu ya watu wake. Huwezi kuzungumza sekta ya uziduaji kwa mafanikio yake makubwa bila kuzungumza elimu ya watu wa nchi husika zote hizi nilizozitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba kama ni kweli tunazungumza lugha moja kwenye hiki, kuna vitu vinatakiwa viachwe. Mwisho ni mwaka huu tunaomaliza kwenda kwenye uchaguzi, kuna baadhi ya vitu ambavyo vinakwamisha elimu yetu kwenda mbele, vinatakiwa visiwepo kabisa kabisa katika Hansard za Bunge, na hotuba za Wizara. Kwa mfano, kuna mambo kadhaa nimeyaandika hapa na nimeyaona kwa sababu ili Mheshimiwa Waziri Wizara yake ifanye vizuri, lazima mfumo wake wa utoaji wa elimu, watu wote wapate elimu katika mazingira yaliyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza lugha ya alama, bado siyo somo. Yaani watoto wetu hawajifunzi lugha ya alama ili wawasiliane na watoto wengine wenye changamoto za mawasiliano, lakini pia hakuna walimu wa lugha ya alama kwenye shule zetu. Maana yake umeondoa kipengele muhimu cha mawasiliano katika utolewaji wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa natamani tukirudia tena bajeti ya mwakani tuwe tumeshapata ufumbuzi wa jambo linalohusu lugha ya alama kwa sababu ni means of communication kama tunavyozungumza Kiswahili na Kingereza. Sisi sote humu Bungeni tunatakiwa tujue kuzungumza kwa lugha ya alama kwa sababu hao watu wapo kwenye jamii, na sisi ni watumishi ambao tunatumikia watu kwenye majimbo yetu ambao wana changamoto za usikivu na kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima sisi sote tulitakiwa wakati tunapita huko shule tuwe tumesoma somo la lugha ya alama. Tunaweza kuwasiliana na wao wanaweza kuwasiliana na sisi na hilo ni jambo la kutoa tu mwongozo, Mheshimiwa Waziri anajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ninachotamani kisiwepo kabisa katika kukwamisha utolewaji wa elimu nchini, leo bado tunazungumza uhaba wa matundu ya vyoo shuleni. Yaani kitu kidogo kama choo bado tunajadili tujenge matundu mangapi ya vyoo? Natamani ufike muda tumalize. Tena viwe vyoo vya kisasa kwa sababu tuna teknolojia, mifumo, vipaumbele na tunafanya planning. Kwa nini tusimalize haya mambo? Yaani liishe tu iwe imebaki maintenance ya hizo system?

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine cha tatu, kuna kundi kubwa la watoto wa kike ambao wanakosa kuhudhuria masomo eti kwa sababu wamekosa taulo za kike. Yaani una Wizara ambayo ndani yake kuna VETA na SIDO, umesema unaenda kwenye mfumo wa amali na una karakana za nchi ambazo ziko kwenye vyuo, lakini bado umeshindwa kutatua hili? Nchi nyingine wanatushangaa, unaenda eti unatafuta mwekezaji ili akusaidie taulo za kike ukawapelekee watoto shuleni kama vile ni kitu tumekianza jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, enzi na enzi tunajua binti akifika umri fulani lazima ataingia kwenye hiyo hatua. Hivi kweli tumeshindwa kama nchi kutatua hili jambo? Mpaka leo bado tunazungumza kwamba, hakuna taulo za kike! sijui tuliondoa kodi, imeshindikana kupunguza bei, hivi tumeshindwa kuwaambia VETA waje na solution?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna pamba kwenye nchi. Tunaweza ku-import materials tukatengeneza sisi, TAMISEMI wakatusaidia, vyuo vya VETA vikawa vimetatua kabisa hilo jambo likawa limeisha. Natamani lisiwepo kwa sababu, linakosesha watoto wetu kupata elimu. Kuna watu wengine ambao wako kwenye kaya maskini hawawezi ku-afford, ni gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni vifaa vya watu wenye ulemavu. Serikali imeweka mwongozo wa elimu jumuishi, lakini tuna changamoto kubwa ya vifaa vya watu wenye ulemavu, hasa wanafunzi. Tanzania tunazalisha asilimia tano tu ya vifaa ambavyo vinatolewa kwenye hii nchi, lakini 70% na zaidi vinatoka nchi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza pia Waheshimiwa wengine hapa, yaani tunashindwa kuelewa kwa sababu, VETA iko chini ya Wizara hiyo hiyo, hawa wanafunzi wanasoma Wizara hiyo hiyo, yaani tumeshindwa kufanya roll call kujua ni watoto wangapi wenye uhitaji, ili tutumie mifumo yetu ambayo tuna-inject fedha kule, ili tutatue hili jambo?

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri anatakiwa ajue miongoni mwa vitu ambavyo vinasababisha elimu katika Wizara yake isitolewe katika mazingira yanayostahiki ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya watu wenye ulemavu. Kwanza kwenye ulemavu kuna unaoonekana na usioonekana. Hata watoto kutokuwa na utulivu darasani wakati wanafundishwa, wakaelewa kirahisi pia ni ulemavu usioonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna vituo 12 Tanzania vya kupima ulemavu usioonekana kabla watoto hawajaenda shuleni. Mwongozo wa elimu jumuishi unasema kwamba, kila halmashauri inatakiwa iwe na kituo. Labda hapa niongee taratibu, yaani watoto kabla hawajaenda darasani kusoma wanatakiwa wapimwe ili waonekane wanasikia vizuri, wanaona vizuri au ni ADHD.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, kuna watoto wengine wanachelewa kuelewa, kwa hiyo, huwezi kum-treat kama wengine. Ndiyo inasababisha unaweka Form One A, Form One B, Form One C, yaani wale C ndio wale wa mwisho kule, halafu hawa A ndio wenye akili, unaanza kuwabagua tangu kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri hivi vitu vinatakiwa viangaliwe ili kuhakikisha kwamba, elimu yetu inatupeleka mbele.

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mengine mwandikie Mheshimiwa Waziri.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)