Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Urambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwa kifupi hoja iliyoko Mezani. Kwanza, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Daktari Samia na Serikali yake anayoiongoza, kwa jinsi ambavyo ametilia mkazo sana suala la elimu na maisha ni elimu, kila kitu ni elimu halafu mengine yote yanafuata. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wote ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa jinsi ambavyo wameishika hii Wizara. Tunaamini kabisa elimu itaimarika nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda niliopata wa dakika tano, naomba nijikite zaidi kwanza, kwa niaba ya Wananchi wa Urambo, kuishukuru Serikali kwa kutupa VETA. Sisi wananchi wa Urambo tuliona mafunzo ya ufundi ni muhimu sana maishani, hasa vijana wetu, ili waweze kujikita katika maisha yao, wajiendeleze wenyewe kiuchumi kwa kupitia mafunzo ya ufundi. Ndiyo maana tukachelewa kungojea majengo mapya, tukatumia majengo yaliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo, tunaishukuru Serikali kwa kukubali ombi letu, lakini tunarudi kuiomba Serikali itusaidie kuongeza majengo zaidi ili tuongeze study zaidi kuliko zile tulizonazo kwa sababu, tuna upungufu wa karakana, mabweni na majengo mengine. Kwa hiyo, tutashukuru sana Serikali ikifikiria kutuongezea majengo pamoja na walimu, ili vijana wetu wa Urambo wapate mafunzo ya kuwasaidia maishani mwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo haya yanayozungumziwa, ya ufundi ya amali, ni muhimu sana nchini kwetu, lakini unapozungumzia elimu yoyote, iwe ya ufundi, nadharia, jambo muhimu la kuwaza ni walimu. Kwa hiyo, tunaomba kwa heshima na taadhima kabisa Wizara itakapokuwa inakamilisha hotuba yake, basi ituelezee mpango mzima wa kupata walimu kwa sababu, ukisema tu elimu, lazima walimu namba moja na mengine yanafuata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kujua suala la kupata walimu na sasa hivi hili zoezi lililopita, la kupata walimu kwa kweli, naona kidogo Serikali ingeliangalia upya. Walimu hawa wamesoma miaka minne, miaka mitatu kule waliko pia, wakapitishwa kwenye mtihani. Naiomba Serikali ione kweli, kulikuwa na umuhimu wa kuwapitisha kwenye mitihani tena?
Mheshimiwa naibu spika, kwa hiyo, nafikiria watu waliohitimu tayari, bado wanarudishwa kwenye mitihani? Nafikiri ni jambo ambalo Serikali ingeliangalia kwamba, je, kuna umuhimu wa kuwapitisha tena walimu kwenye mitihani ile baada ya kukaa vyuoni?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nafikiria kwamba, kwa sababu hivi vyuo vya ufundi na amali, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, ni muhimu sana, naomba tuangalie kwamba, kutokana na mahitaji makubwa ya walimu, je, Serikali haiwezi kuja na mpango wa posho fulani, kama vile wanavyopata walimu wanapojitolea kwenye shule sasa hivi kabla hawajaajiriwa? Je, Serikali inaweza kufikiria mpango wa kupata posho ili walimu wale tunaowahitaji kwa sasa hivi wapate posho wanapojitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, watakapotangaza ajira, hawa walimu wanaojitolea ndio wawe wa kwanza kuajiriwa. Sasa tunaomba Serikali ione, kama je, iko tayari kupata posho kwa hawa walimu wanaojitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la muhimu sana kutokana na mafunzo ya ufundi, kulikuwa kuna kitu kinaitwa Skills Development Levy. Je tunaitumiaje? Kwa sababu, Skills Development Levy ililetwa, kwa ajili ya kukuza mafunzo hayo. Ndiyo tunaitumiaje? Sheria ilivyosema ndivyo inavyotumika sasa hivi? Nafikiri ni jambo ambalo lingeangaliwa sana, je, tumewaandaa wenye viwanda wawe tayari kuwapa nafasi wanafunzi kufanya majaribio wakati vyuo vinapofungwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi nyingine wameweka sheria ya kuwataka wenye viwanda kutoa nafasi kwa vijana wanaojifunza mafunzo haya wafanye majaribio wakati wanapokuwa likizo. Kwa hiyo, nafikiri ni jambo la msingi sana kukubalika, kupewa nafasi ya majaribio kwenye viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana vyuo vya VETA, mafunzo yanayotolewa yalenge sana mahitaji ya maeneo. Kama watu wanachimba dhahabu au nini, basi mafunzo ya VETA yalenge kupunguza changamoto za maeneo yanayohusika kutokana na ujuzi wanaoupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nawapongeza sana Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kazi kubwa wanayofanya. Ahsante sana. (Makofi)