Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Latifa Khamis Juwakali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti hii ya Wizara ya Elimu. Kwanza, naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan, kwa mapinduzi na maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Wizara yetu hii ya Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nampongeza pia, Waziri wetu wa Elimu, Naibu Waziri wa Elimu, viongozi wote na watendaji wote wa Wizara ya Elimu. Kutokana na muda, mchango wangu naomba nijielekeze katika maeneo matatu. Eneo la kwanza litakuwa ni Mikopo ya Elimu ya Juu; eneo la pili ni Vyuo vya VETA na eneo la tatu ni Udhibiti wa Ubora.

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba Mheshimiwa Rais amefanya maboresho na mapinduzi makubwa katika miundombinu, ikiwemo kujenga shule mbalimbali na kujenga matundu ya vyoo. Nataka nizungumzie hili suala la mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wetu wa elimu ya juu. Tunajua kwamba, sasa hivi wanafunzi wetu wengi wanapata mikopo ya elimu ya juu tena kwa wakati unaostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba, nchi nyingine ambazo zimeendelea huko, elimu ni service na tunamshukuru Mheshimiwa Rais, mbali ya kuwa kunatolewa mikopo ya elimu ya juu, fedha zinakwenda, tunajua kwamba, kuna Samia Scholarship. Serikali waendelee kulichukua hili kwamba, kwa sababu tumefanya maboresho makubwa katika mikopo hii na ninaiona dira, ninaona mwelekeo na ninaona kiu ya Mheshimiwa Rais ya kuendelea kuwasaidia wananchi na vijana ambao ni maskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo haja ya kuwasaidia hao wanafunzi wetu ambao wanatoka katika familia maskini, angalau basi wapatiwe hata elimu bure katika vyuo vikuu. Hii itaweza kuwasaidia wao, lakini kuwa wanafunzi wa mfano wa kuendelea kuisemea Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niendelee katika suala hili la vyuo vya VETA. Sisi tunafahamu kwamba, sasa hivi Serikali yetu inajiandaa katika kumalizia vituo vyetu hivi vya VETA katika nchi nzima. Nataka niipongeze Serikali kwa sababu, katika bajeti zilizopita tulilizungumzia sana katika Bunge lile lililopita, ili kuona tunafanya maboresho na marekebisho ya mitaala ya elimu. Kimoja ambacho tulikuwa tunakizungumzia, ni kuona kwamba, tunaboresha vituo vyetu vya VETA ili wanafunzi waweze kupata ujuzi, waweze kujiajiri na kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali yangu kwamba bora tuchelewe, lakini tufanye vitu kwa uhakika na ninaomba hili tulichukue. Tufanye vitu kwa uhakika, tumeshajenga VETA, tutafute hata vituo vya VETA 63 hata nusu ya vituo vya VETA tulivyovijenga, lakini tuhakikishe mahitaji ambayo yanahitajika katika vituo vile yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya maboresho makubwa na imetoa fedha nyingi sana. Haitapendeza kwamba, tunaenda katika vituo hivyo vya VETA, mwanafunzi anaenda kujifunza kutengeneza magari, lakini katika kituo hicho cha VETA hakuna karakana. Naamini kwamba, tutakuwa bado hatujawasaidia na hatutaweza kufikia lengo tulilokusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kwa haraka haraka, naomba nimalizie na hili suala la udhibiti ubora. Hawa wadhibiti ubora wanaajiriwa au wanasimamiwa na Wizara ya Elimu, lakini cha kushangaza hawa wanafanya kazi kwenye halmashauri. Huwezi kufanya kazi ipasavyo, kama mtu ambaye unamsimamia, ndio ambaye anakulipa au ndio anaku-supervise.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara, hili walichukue. Hao wadhibiti ubora waendelee kuwasimamia wao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mengine utamwandikia Waziri.

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: ...na ruzuku zao zitoke kwao wawapelekee moja kwa moja, ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)