Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee ninaomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National Competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua elimu katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miezi kumi ya mwaka wa 2024/2025, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI, imesimamia kwa uadilifu na ufanisi mkubwa masuala yote ya elimu hasa kuboresha ufaulu na hata miundombinu ya madarasa na mabweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imeendelea kupitia kipindi kigumu cha changamoto za kuporomoka kutoka kuongoza kimkoa katika ufaulu wa elimu ya sekondari. Pia ufaulu kwa shule za msingi unapitia katika changamoto kubwa hasa kutokana na mazingira ya shule za vijijini ikiwemo upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja kuwa ni jukumu jumuishi kwa wazazi, bado kunahitaji uharaka wa kupitia sera ya elimu kuweza kuboresha taaluma kwa shule za vijijini ambazo kwa kiasi kikubwa hazifanyi vizuri ukilinganisha na shule za mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu bado wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu kwa kukosa majengo ya nyumba za kuishi. Napendekeza Serikali kupitia TAMISEMI na Wizara ya Elimu kuendelea kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa nyumba za walimu iende sambamba na ujenzi wa maboma na pia madawati kwa wanafunzi wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu kuhakikisha motisha kwa walimu ili kuboresha taaluma iwe ya kiushindani kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na hata Afrika. Napendekeza pia Serikali itoe kipaumbele kwa kulipa madai ya malimbikizo kwa walimu, ili kupunguza muda wa kufuatilia malipo yao na badala yake waelekeze muda zaidi kwenye kufundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi hiki tunapopambana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yakiwemo magojwa ya kansa, shinikizo la damu, figo, moyo na kadhalika, narudia tena kushauri Serikali kuweka kipaumbele cha kuboresha elimu ya afya, ikiwemo upanuzi wa ujenzi wa ndaki ya Sayansi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mbeya College of Health and Allied Sciences (UDSM-MCHAS). Serikali itoe kipaumbele cha ujenzi wa chuo hiki kutoka kwa eneo la iliyokuwa Tanganyika Packers Ltd., Mbalizi Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwezesha uwekezaji na uendelezwaji wa viwanda endelevu, Tanzania inahitaji kuzalisha watalaamu wengi na hasa ujasiriamali na taaluma ya ufundi ngazi za kati na chini ambapo mahitaji ni makubwa. Pamoja na kujiwekea malengo ya kuongeza viwanda, nashauri Serikali iweke mkazo suala la uwepo wa nguvu kazi (vijana kupata mafunzo ya ufundi na ujasiriamali) ya kutosha na itakayowezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko mbalimbali hasa ya kisayansi na kiteknolojia na hata kiuchumi, yanayoendelea duniani, napongeza hatua ya Serikali kwa kuchukua hatua za kuboresha mitaala ya elimu kuwa ya kisasa zaidi ili kuendana na mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka kadhaa iliyopita Tanzania imeshuhudia mafundi mchundo wengi wakiongeza (upgrade) ngazi za utaalamu wao kwa kusomea kozi za uhandisi wakati idadi ya mafundi mchundo wanaofuzu masomo ya ufundi mchundo ikipungua huku mafundi wa kawaida (artisans) wanaoongeza utaalamu wao ikiwa haiongezeki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii imepelekea kupungua kwa kasi idadi ya mafundi mchundo pamoja na mafundi wa kawaida na hivyo kuathiri utendaji wa viwanda na sekta nyingine kwa kuwa hawa ndio wanaotenda kazi kwa mikono. Ukizingatia kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda, hali hii inabidi irekebishwe haraka kwa kuongeza idadi ya mafundi husika ili kukidhi mahitaji ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa uwiano wa wahandisi/mafundi mchundo/mafundi wa kawaida upo chini sana na hautaweza kuisaidia Tanzania kufikia malengo tarajiwa. Hata ukilinganisha wataalamu wa juu wa stadi mbalimbali za Taifa na wenye stadi za kati na za chini uwiano wake siyo mzuri ukilenga uwezo wa kusimamia viwanda vya kisasa kiasi cha kuhitaji marekebisho ya uwiano kama Mpango wa Taifa wa Kuendeleza Stadi Unavyotegemea (National Skills Development Strategy).

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali iongeze msukumo kwenye mafunzo ya amali, mafundi mchundo na mafundi wa kawaida na pia elimu yetu ilenge mafunzo ya ujasiriamali. Hii pia ishirikishe elimu ya kujitegemea toka elimu ya awali na hata kutumia watalaamu wetu wa kilimo, mifugo na uvuvi kuanzisha mashamba darasa mashuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.